Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 11 03Article 567751

Maoni of Wednesday, 3 November 2021

Columnist: www.habarileo.co.tz

Shime: tunataka ushindi kwa Ethiopia

Shime: tunataka ushindi kwa Ethiopia Shime: tunataka ushindi kwa Ethiopia

KOCHA Mkuu wa Timu ya soka ya Taifa ya Wanawake chini ya umri wa miaka 20, Tanzanite Queens, Bakari Shime amesema hawatobweteka na matokeo yaliyopita bali wanahitaji kupambana leo dhidi ya Ethiopia kuendeleza ushindi.

Tanzanite leo inatarajiwa kushuka uwanjani katika mchezo wa tatu wa michuano ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) inayoendelea Uganda.

Akizungumzia mchezo huo dhidi ya Ethiopia utakaochezwa saa 4:30 asubuhi, Shime alisema watahakikisha wanapambana kupata matokeo mazuri.

“Tuna mchezo na Ethiopia kikubwa tutahakikisha tunapata matokeo mazuri, tunaamini michezo hii itatufanya kuendelea kuimarika na kuona mapungufu yetu ili kujipanga zaidi,”alisema.

Tanzanite imetoka kushinda michezo miwili katika michuano hiyo yenye timu sita inayochezwa kama ligi na mwisho mwenye pointi nyingi ndiye atatangazwa bingwa.

Imeshinda mchezo wa kwanza dhidi ya Eritrea bao 1-0 na mabao 3-2 dhidi ya Burundi yote ikichezwa kwenye Uwanja wa FTC Njeru, Uganda.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu kwani Ethiopia wametoka kushinda michezo miwili iliyopita kuonesha ni bora.

Katika michezo hiyo iliyopita, Shime alisema bado hawakuwa wakicheza kwa ubora wao ndio maana benchi la ufundi limekuwa likipambana kufanya kazi usiku na mchana kuweka mambo sawa.

“Bado tunapambana turudi katika ubora wetu, tumekuwa tukicheza lakini mapito ambayo timu inapitia sisi kama benchi la ufundi tunafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha vijana wanarudi katika hali ya kawaida,”alisema.

Alisema anaamini watafika sehemu watarudi katika hali ya kawaida. Baada ya mchezo huo, itabakiza miwili dhidi ya Uganda na Djibouti itakayochezwa siku zinazofuata.

Wakati huohuo, wachezaji watano wa Eritrea wametoweka hotelini Jinja jana asubuhi.

Taarifa ya Cecafa jana ilisema, tayari taarifa imepelekwa Polisi na kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Uganda, (Fufa), wanafanya iwezekanavyo kupatikana kwa wachezaji hao