Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 12 27Article 581401

Maoni of Monday, 27 December 2021

Columnist: www.habarileo.co.tz

Shule kila kata, chakula suluhisho utoro shuleni

Shule kila kata, chakula suluhisho utoro shuleni Shule kila kata, chakula suluhisho utoro shuleni

Utoro ni jambo linalosababisha watoto wanaoandikishwa kuanza shule za msingi, kushindwa kumaliza kiwango hicho cha elimu nchini.

Makala haya yanaangazia tatizo hilo linavyoathiri maendeleo ya kielimu katika Mkoa wa Mara, mambo yanayochochea tatizo hilo na yanayoweza kufanyika ili kukabiliana nalo.

Mkuu wa Mkoa huo, Ally Hapi anasema utoro limekuwa tatizo sugu ambalo linasababisha wanafunzi wengi kuondoka shuleni huku wakiwa hawajamaliza darasa la saba.

Anarejea tathmini iliyofanywa kati ya mwaka 2017 hadi 2021 akisema inaonesha asilimia 10.8 ya watoto 310,000 ambao waliandikishwa kuanza masomo katika shule za msingi, hawajulikani walipo.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, inamaanisha takribani watoto 34,000 wa kada hiyo katika mkoa huo walioanza shule ya msingi, hawajahitimu na hawapo shuleni.

“Hawapo shule kwa maana ya kwamba hawapo kwenye orodha ya wanafunzi wanaohudhuria masomo na hawajahitimu, lazima tujue wapo wapi?” anasema Hapi.

Ni wajibu wa serikali kushirikiana na jamii husika kutafiti na kujua walipo watoto hao.

Itakuwaje ikiwa wamekusanywa na kupelekwa kwenye msitu ambako wanafundishwa mambo yasiyojulikana?

Zimebainika sababu zinazochangia tatizo hilo kuwa sugu. Mojawapo ni umbali kati ya makazi na shule hali ambayo husababisha watoto kusafiri mwendo mrefu wakati wa kwenda shule na kurudi nyumbani.

Hata hivyo, changamoto hiyo inaelekea kubaki historia kufuatia jitihada za serikali kuhakikisha hakuna kata isiyokuwa na shule ya msingi, hali inayogharimu kiasi kikubwa cha fedha katika ujenzi wa miundombinu hiyo.

Sababu nyingine imeonekana kuwa ni umaskini katika ngazi za kaya, hali ambayo husababisha baadhi ya watoto kwenda shule bila kula chochote na kufanya washindwe kuvumilia kubaki

shuleni. Changamoto hiyo pia imeanza kufanyiwa kazi na serikali mkoani humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa kwenye Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa, Novemba mwaka huu (2021) utoaji wa chakula cha mchana shuleni ni moja ya maazimio yaliyofikiwa katika kongamano la wadau wa elimu la mkoa huo.

Kongamano hilo lililofanyika katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Songe, Februari mwaka huu na kuundwa kamati ya wataalamu kwa ajili ya kutengeneza mpango mkakati wa mkoa wa chakula na lishe shuleni, sasa mpango huo umekamilika.

Licha ya lengo kuu la mpango mkakati huo kuwa ni kuimarisha upatikanaji wa chakula na lishe katika shule za msingi na sekondari mkoani humo ifikapo mwaka 2025, Hapi ameagiza utekelezaji wake uanze mara moja.

Anasema wakati hatua nyingine za kufanikisha mpango huo kama ilivyokusudiwa zikiendelea kufanyiwa kazi, maeneo ambayo utoro unaohusishwa na watoto kushindwa kuvumilia njaa shuleni, huduma hiyo ianze kutolewa.

Hapi ameasa uongozi wa shule zinazotekeleza mpango huo kutolazimisha wazazi kutoa michango hususani ya fedha, isipokuwa waelimishwe na kushawishiwa kutoa michango ya vyakula na vitu

vinavyohitajika katika kufanikisha mpango huo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye kikao hicho jitihada za kujenga uelewa kwa jamii zimeshaanza, hadi Desemba mwaka jana kati ya shule za msingi 796, shule 349 zilikuwa zinatoa huduma ya chakula shuleni hususani kwa madarasa ya mitihani.

Kwa upande wa shule za sekondari, inaelezwa kuwa mpaka wakati huo kati ya shule 199, shule 121 zilikuwa zinatoa huduma hiyo hususani kwa madarasa ya mitihani.

Chanzo cha kupatikana kwa chakula kinachotumiwa katika mpango huo kimeelezwa wazi na taarifa hiyo kuwa ni michango kutoka kwa jamii na wazazi, vikundi vya wakulima na mavuno au mapato katika mashamba ya shule husika.

Sababu nyingine inayochangia watoto kutomaliza masomo kwa upande wa wasichana ni changamoto mbalimbali zinazowakabili wale wanaofikia hatua ya kuingia kwenye hedhi.

Tukio hilo ni la kipaumbile ambalo haliwezekani kuepukwa na mtu yeyote mwenye jinsi ya kike, lakini katika baadhi ya kabila limekuwa likiendana na mila ambazo makala haya yameziangazia kuwa miongoni mwa mambo ambayo yanachangia watoto kutomaliza masomo.

Mathalani kabila la Wajaluo ambao kwa wingi hupatikana katika Wilaya ya Rorya, wana mila inayofahamika kwa jina la Nyumba ya Simba.

Hii ni mila ambayo hufanywa na familia ambapo binti anapovunja ungo (anapoingia kwenye hedhi kwa mara ya kwanza), pamoja na mambo mengine huhamishwa kwenye nyumba ya wazazi na kutakiwa

uishi ndani ya nyumba ambayo hujengwa jirani na lango kuu la kuingilia kwenye makazi husika.

Hiyo humaanisha kuwa binti huyo amepevuka, ana uhuru wa kutoka nyumbani na kurejea wakati wowote akiwa na yeyote bila kuonwa au kuulizwa na wazazi.

Mila hii imelalamikiwa na wadau mbalimbali wa elimu kuwa inachangia kwa kiasi kikubwa ndoa na mimba za utotoni pamoja na watoto kutoka shuleni kabla ya kuhitimu masomo.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Rorya, Lucy Mtesigwa ni miongoni mwa wadau wanaotaka hatua za kuhamasisha jamii hiyo kuacha mila na desturi hizo kutekelezwa.

Mkoa kuwa na watoto zaidi ya 30,000 ambao wanatakiwa kuwa shuleni lakini haifahamiki waliko haitakiwi kufumbiwa macho, inaweza kusababisha janga la kitaifa na hata kimataifa.

Haiwezi kushangaza miongoni mwa watoto hao wakakutwa wameingizwa kwenye makundi ya kigaidi, ujambazi, vibaka au wakaishia kuwa watu waliokosa malezi bora ya kifamilia na hivyo taifa kujikuta likigubikwa na matukio yenye kuhatarisha usalama na amani kwa ya jamii kwa ujumla.

Hapi ameagiza uongozi wa kila mtaa wa mkoa huo kufuatilia kaya yenye mtoto aliyetakiwa kuwa shuleni na hayupo ili ifahamike yuko wapi.

Kazi hiyo imetakiwa kufanywa chini ya uratibu wa maofisa tarafa ambapo wakuu wa wilaya wameagizwa kuwawezesha kufanikisha hilo na taarifa zipelekwe kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa kwa ajili ya hatua nyingine zitakazowezesha kukabiliana na hali hiyo.