Uko hapa: NyumbaniWallMaoniArticles2021 01 12Article 520934

Maoni of Tuesday, 12 January 2021

Columnist: HabariLeo

Shule zinazojengwa zisisahau mabweni kwa wasichana

Shule zinazojengwa zisisahau mabweni kwa wasichana Shule zinazojengwa zisisahau mabweni kwa wasichana

MUHULA wa masomo kwa wanafunzi wa sekondari umewadia. Shule nyingi kama si zote za sekondari nchini, zinafunguliwa leo. Hili ni jambo jema la kumshukuru Mungu na kuwapongeza wanaoendelea na waliochaghuliwa kujiunga kidato cha kwanza kwa mwaka huu wa 2021.

Hata hivyo, wakati shule zinafungliwa leo, baadhi ya wanafunzi waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari mwaka huu, hawataanza leo kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa jambo lililomfanya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuagiza kuwa ifikapo mwisho wa mwezi ujao (Februari), wanafunzi wote wawe wamepata nafasi kutokana na watendaji mbalimbali wakiwamo wa TAMISEMI kuwa wamehakikisha vyumba vya madarasa vimejengwa na watoto hao wanapata haki yao.

Napenda kutumia fursa hii kuwakumbusha wadau wote kuwa, juhudi za kujenga madarasa zinapaswa kwenda sambamba na ujenzi wa mabweni hasa kwa ajili ya wanafunzi wa kike ili wanaopanza masomo, ‘wamalize wote salama’.

Hili likifanyika litawawezesha wanafunzi wa kike wanachaguliwa kujiunga katika shule za kutwa, kuepuka vishawishi mbalimbali wanavyokutana navyo kutokana na mazingira yao ya kwenda na kutoka shuleni na hatimaye, kuishia katika ndoa na mimba za mapema jambo ambalo jamii sasa inalipiga vita.

Ikumbukwe kuwa, kwa kila siku wanafunzi kwenda na kutoka shuleni huku wengine wakitembea umbali mrefu, wanakumbana na vishawishi vikiwamo vya kupewa ‘lifti’ ambazo mara nyingine wahusika hutaka ‘zilipwe’ kwa njia inayohatarisha maisha na masomo ya wanafunzi hao wa kike kwa kubakwa au hata kusababishiwa ujauzito.

Kwa kuwa wengine hutoka mbalimbali, baadhi ya wanafunzi hulazimika kujiunga na kuishi ‘gheto’ ili kubana matumizi ya muda na pesa kwa kuishi wengi katika chumba kimoja na wengine, hufikia hata kushi kama mke na mume.

Kutokana na hali hii, ambayo pia huwafanya wanafunzi wengi wa kike kukosa muda wa kupumzika na kufuatilia masomo wawapo nyumbani, umefika wakati Watanzania wote wakiwamo wakazi wa maeneo ya shule za kata, waazimie kuwa, kuanzia mwaka kesho, walau kila shule iliyopo, au mpya inayojengwa, iwe na mabweni (hosteli) kwa ajili ya wanafunzi wa kike.

Kwa mfano, hata kama kwa mwaka huu tunaweza kuwa tumechelewa, basi maandalizi kwa ajili ya madarasa ya wanafunzi wanaokwenda kuanza kidato cha kwanza mwaka 2022 yanayopaswa kuanza sasa, yaende sambamba na ujenzi wa mabweni na hosteli hizo kwa ajili ya wasichana.

Nijuavyo mimi, kwa kuanzia wanafunzi hao wanahitaji hasa vyumba vya kulala, lakini mahitaji mengine, yanaweza kupangwa sawia na wazazi kupitia kamati zao kwa kushirikiana na uongozi wa shule ikiwa ni pamoja na uwezekano wa wazazi kuchangia vyakula.

Bila kuzingatia hili mapema, ujenzi wa madarasa unaweza usitoe tija tarajiwa kwa kuwa kuna hatari wanafunzi wa kike wanaoingia kidato cha kwanza ikawa kubwa, lakini idadi ya wanahitimu na kuchaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano, au vyuo vya kati, ikawa inashuka kila kukicha.

Ndiyo maana ninasema, ujenzi wa shule mpya na vyumba vya madarasa usisahau mabweni kwa wanafunzi wa kike.

Join our Newsletter