Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 10 12Article 562741

Maoni of Tuesday, 12 October 2021

Columnist: mwananchidigital

Sifa zilizombeba Jaji Siyani kuwa Jaji Kiongozi

Sifa zilizombeba Jaji Siyani kuwa Jaji Kiongozi Sifa zilizombeba Jaji Siyani kuwa Jaji Kiongozi

Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma, ametaja vigezo vilivyomfanya Jaji Mustafa Siyani kuteuliwa kuwa Jaji Kiongozi, kuwa ni pamoja na kuwa na uelewa mpana wa Mahakama na utamaduni wake.

Aliyasema hayo jana wakati wa hafla ya uapisho wa Mkoa wa Shinyanga, Sophia Mjema, Jaji Kiongozi Mustafa Siyani na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Omar Othman Makungu. Hafla hiyo ilifanyika jana jijini hapa.

Profesa Juma alisema Jaji Siyani ametimiza sifa zote za kikatiba za kuwa Jaji Kiongozi na sifa ya kwanza ni kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.

Alisema Jaji Kiongozi ni mshauri wa Jaji Mkuu, hivyo anabeba mzigo mkubwa wa kusimamia mahakama zote zilizopo nchini.

“Tume ya Utumishi wa Mahakama ilikuwa na vigezo mbalimbali. Iliangalia kati ya majaji 85 ambao wanastahili kuwa majaji viongozi, kina nani tupeleke majina yao ili mheshimiwa Rais aangalie,” alisema.

Alitaja sifa ya kwanza ni uelewa mpana na utamaduni wa ndani wa mahakama.

“Mambo mengi kuhusu taasisi huwa yamejificha, ni kama barafu siku zote unaona ncha, lakini uzito wa barafu huuoni, wewe unaifahamu mahakama utakuwa na nafasi nzuri sana ya kufanya kazi. Ilikuwa ni sifa ambayo wewe na wengine mliopelekwa kwa mheshimiwa Rais mlikuwa mmetimiza,” alisema.

Profesa Juma alisema Mahakama si kisiwa, watendaji wake wanapaswa kushirikiana kwa karibu na mihimili mingine kwa lengo la kujua nini kinatekelezwa na kwa wakati upi. Alisema pia waliangalia mtu ambaye lazima aelewe kuwa mahakama inakwenda wapi kwa sababu wakati mwingine majaji hukaa na kuandika hukumu, pasipo kuifahamu dunia inayowazunguka.

“Tunakuwa tumemaliza majalada yetu, kumbe kuna mambo mengine ambayo mahakama na nchi inakwenda unaweza kukuta watu wengi hawafahamu,” alisema.

Profesa Juma alisema hivyo ni jukumu lake kuwakumbusha majaji wapi nchi na mahakama vinakwenda kwa sababu asipofahamu nchi inakwenda wapi, atakuwa muda wote anakosoa yale yanayofanyika.

Profesa Juma alisema kigezo kingine ni uwezo wa kujenga umoja, kwa sababu katika taasisi huwa kuna mashindano

“Kuna kudharauliana, kada moja inajiona ni bora zaidi ya nyingine. Kazi yako ni kujenga umoja kwa sababu kila mmoja ni muhimu katika kufikia malengo ya mahakama,” alisema. Alisema anaamini akisimamia nguzo tatu zinazowaongoza katika mpango mkakati wa utawala bora, ikiwamo ya uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali, idara ya mahakama itafanikiwa.

Alitaja nguzo ya nyingine ni upatikanaji na utoaji wa haki kwa wakati na ya tatu ikiwa kuimarisha imani ya wananchi kwa chombo hicho cha kutoa haki.

Mawakili wamwagia sifa

Baadhi ya mawakili waliozungumza na Mwananchi, walisema kuwa ingawa jukumu alilipewa ni kubwa, wanaamini kuwa ataliweza na kwamba ana sifa zote za kumudu utekelezaji wa jukumu la nafasi hiyo muhimu kwa mhimili wa Mahakama.

Mawakili hao, Fulgence Massawe kutoka kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Alex Mgongolwa na Simon Vitalis wote kwa nyakati tofauti walimwelezea Jaji Siyani kuwa ni mtu mwenye hofu kwa Mwenyezi Mungu, mpenda haki na mchapakazi.

Wakili Massawe ambaye alisema kuwa alisoma na Jaji Siyani, alisema kuwa ingawa wakati alipoapishwa na Rais (Hayati Magufuli alimtolea mfano kama jaji kijana, lakini amepanda harakaharaka huku akitaja sifa zinazombeba kuwa ni pamoja na ucha -Mungu, uchapakazi na uadilifu.

Alisema kuwa baada ya kuapishwa alipangiwa kituo cha kazi Mwanza, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, lakini baada ya muda mfupi tu alihamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma ambako alipandishwa na kuwa Jaji Mfawidhi.

“Jaji Siyani mimi nimesoma naye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alikuwa ni miongoni mwa watu wenye kumcha Mungu, mchapakazi na mwadilifu. Kwa hiyo akitumia vitu hivyo vyote, vitamsaidia katika uongozi wake,” alisema Massawe.

Kwa upande wake, wakili Mgongolwa, alisema alimfahamu Jaji Siyani tangu akiwa Hakimu Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu ambapo alipata kufanya kazi mbele yake na kwamba alivutiwa na namna alivyo mtulivu wa kusikiliza na kufanya uamuzi.

“Nilimpenda kwa hilo. Mara zote nilizo-appear kwake (kuwa na kesi mbele yake) alinionyesha kuwa ana ukomavu wa kusikiliza na kufanya maamuzi yanayohusiana na haki. Ana mtizamo wa kihaki. Ni rafiki katika mfumo wa haki. Si mtu wa jazba,” alisema Mgongolwa.

Naye Wakili Timon Vitalis alisema kuwa hajafanya naye kazi akiwa jaji, japo aliwahi kukutana naye kikazi alipokuwa hakimu na kwamba anamfahamu kama mchapakazi, mwadilifu na mtu wa haki.

“Kwa hiyo sifa anazo ukiachilia mbali hilo tu ambalo wengine wanaweza wakalisema kwamba mdogo na hana muda mrefu, kwa sababu wapo majaji waandamizi wengi, lakini Katiba haisemi kuwa Jaji Kiongozi lazima awe jaji mwandamizi,” alisema wakili Vitalis.