Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 08 16Article 551731

Maoni of Monday, 16 August 2021

Columnist: Mwanaspoti

TUONGEE KISHKAJI: Amapiano kali, ila tuipumzishe wanangu

Msanii wa Bongo fleva, Marioo Msanii wa Bongo fleva, Marioo

Mpaka tukimaliza mwezi huu tutakuwa na ngoma zaidi ya 30 za wasanii wa Tanzania zilizoimbwa kwa mtindo wa amapiano - muziki ambao asili yake ni nchini Afrika Kusini. Na ishu zaidi ni kwamba wasanii wote wa Bongo wanaoimba amapinao wanaimba kwa kuiga kila kitu kama kinavyofanywa na wasanii wa Sauzi.

Tukisema kila kitu tunamaanisha kila kitu - kukopi na kupesti yaani kuanzia mdundo, aina ya mashairi na upangiliaji wake, utamkaji wa maneno na pia hata uimbaji. Kama hiyo haitoshi mpaka video tunatengeneza kama wasanii wa amapiano wa Sauzi wanavyotengeneza.

Yaani kama humjui Diamond na hufahamu Kiswahili ikipigwa ngoma yake ya Iyo ambayo ni amapiano unaweza kudhani ni wimbo wa msanii kutoka kwa Madiba.

Sipingi amapiano ni muziki mzuri sana hasa ukipigwa sehemu za starehe na sehemu zenye amsha popo, lakini sioni kwanini wasanii wa Bongo wanatumia nguvu kubwa kuusukuma muziki ambao sio mali yao. Kwanini?

Inaeleweka msanii ana uhuru wa kujaribu vitu tofautitofauti pia, lakini ikifika kwa kiwango cha wasanii wetu wanavyoijaribu amapiano inakuwa ni kupita kiasi.

Kwa mfano, Harmonize pekee ana ngoma za amapiano si chini ya tano. Diamond anazo, Marioo anazo, Lava Lava anazo, Mbosso anazo na nyingine nyingi kutoka kwa wasanii tofautitofauti zinakuja - kwanini?

Wasanii wangeeleweka zaidi kama wangechukua muziki wa amapiano wakaongezea maujanja na kutengeneza muziki mpya ambao haujawahi kusikika sehemu nyingine. Wangetisha sana kwa sababu kwa kawaida miziki yote duniani hutengenezwa hivyo - kwa kuchanganya aina zaidi ya moja ya muziki.

Bongo Fleva tunayojivunia leo ni mchanganyiko wa Hip Hop, R&B na Pop iliyotiwa ladha ya Kitanzania. Hii ni kwa mujibu wa wasanii waliobuni muziki huo kina P Funk. Hata muziki wa taarab unaompa mzee Yusufu pesa ya kula leo ni zao la muziki laini wa Misri uliotiwa ladha za Kiswahili. Mambo ya kufuata trendi yanapoteza umakini kwenye kuukuza muziki. Kama tunataka kuvuka mipaka vizuri inabidi twende na vitu vyetu. Wanaijeria hawajatawala hapa Bongo kwa kuimba Bongo Fleva, hapana, walikuja na vitu vyao vikateka soko.

Wasauzi hawakuleta amapiano yao hapa Bongo kupitia Bongo Fleva. Walikuja na amapiano yao tukaipenda ikatrendi. Kama na sisi tunataka kwenda kwao na kupokewa vizuri inabidi tupeleka bidhaa zetu, tupeleke muziki wetu. Na hata kama tulijaribu na kuona haupenyi basi labda tulipaswa kutumia muda huu kuangalia kwanini haupenyi.

Huwezi kwenda Sauzi ukawashangaza kwa kuimba amapiano ni muziki wao, hakuna cha ajabu hapo - hakuna jipya.

Narudia tena, amapiano ni muziki mzuri sana lakini hakukuwa na sababu ya wasanii wa ndani kutumia nguvu kubwa kuutangaza. Sisi tungekomaa na muziki wetu.