Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 07 05Article 545485

Maoni of Monday, 5 July 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

TUONGEE KISHKAJI: Chawa wanateleza, wasanii wanatelezeshwa

TUONGEE KISHKAJI: Chawa wanateleza, wasanii wanatelezeshwa TUONGEE KISHKAJI: Chawa wanateleza, wasanii wanatelezeshwa

ZUNGUMZA na washikaji wawili watatu wanaopiga mishe za online TV watakwambia ukweli kwamba moja ya video zilizotazamwa sana kwenye chaneli zao ni zile walizomhoji Baba Levo.

Ukiwauliza kwanini watakwambia kwa sababu Baba Levo anachekesha.

Ni kweli Baba Levo anachekesha sana, lakini hajaanza kuchekesha leo, alianza kitambo tangu kwenye ‘clip’ zake zilizopewa jina la Fix za Baba Levo, ukiinga Youtube utazikuta.

Kwenye hizo clip anatania kitambi cha Peter Msechu, mahipsi ya Linah Sanga, penzi la Shilole na Nuh Mziwanda, rasta na upara wa Mrisho Mpoto, mdomo wa Diamond, kithembe cha Ney wa Mitego, miguu ya Wema Sepetu, Weusi kuishi watu nane ghetto moja, yaani habakishi mtu.

Baba Levo alianza uchale chale kitambo hadi mwaka 2014 alialikwa na Millard Ayo kwenye kipindi chake cha Amplifaya cha Clouds FM, na kipindi kizima kikawa ni vichekesho vya Baba Levo tu, na wakafanya hivyo zaidi mara moja, anapiga mastori ya uongo, watu wanacheka mbavu nyang’anyang’a.

Lakini kwanini amekuwa dili sasa hivi? Kwa sababu, kwa sasa Baba Levo sio tu mchekeshaji na muimbaji, bali pia ni chawa.

Wanaojiita chawa mjini wamekuwa wengi na maarufu sana siku hizi. Wanaojiita chawa wanaishi kama anavyoishi mdudu chawa, wanamsifia mtu mwenye pesa na maarufu ili nao wajipatie aidha umaarufu au pesa. Lakini ukiwatazama kwa jicho zuri huoni chawa, unaona kujichafua kwa wasanii wenye chawa. Kwanini? Kwa sababu chawa hawana adabu, hawana stara, hawana heshima.

Chawa anaweza kuamka akaamua leo nitamsifia mtu wangu kwa kuwatukana mashabiki wa mpinzani wa msanii wangu, upinzani ni mzuri lakini ukishafikia kiwango cha uadui huko ni kuvuka mipaka.

Na inaonekana wasanii wenye chawa wao wanapenda mchezo mzima unavyoenda, inaonekana kama wanawatumia chawa kuzungumza mambo ambayo wao hawawezi kuyasema kwa midomo yao.

Tukirudi kwenye matokeo, chawa anapanda, anapata umaarufu japo wa kijinga, lakini msanii anapoteza watu wa maana, anapoteza mashabiki, hata kama itakuwa ni kwa idadi ndogo lakini bado ni mashabiki.

Mfano rahisi kumbuka moja ya maoni yaliyopata umaarufu juzi kwenye mitandao ya kijamii baada ya Diamond kukosa tuzo ya BET, yalikuwa yanasema; “Bora Diamond alivyokosa tuzo, maana angeshinda, chawa wake wangetukomesha.”

Yaani kwa sababu ya chawa tu, Mtanzania anaona bora Mtanzania mwenzake asishinde tuzo kubwa ambayo Tanzania hatujawahi kuipata.

Ukitaka kuwaelewa chawa, msikilize muigizaji Daudi Micheal ‘Duma’, anasema; “Nimefanya utafiti, nimegundua watu wengi wanaojiita chawa ni watoto wa kiume, pia ni watu ambao maisha yao yaliyumba kwa hiyo wanatafuta njia rahisi ya kujiweka sawa.”

“Na isitoshe kazi ya kuwa chawa ina ukakasi sana, inahusisha kusifia, kwahiyo unakuta mtoto wa kiume anamsifia mwanaume mwenzie mpaka unaogopa, hadi unajiuliza, inakuwaje hawa watoto wa kiume wanasifiana hivi, wanafanya nini hawa?”