Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 11 16Article 571669

Maoni of Tuesday, 16 November 2021

Columnist: www.tanzaniaweb.com

Tulitaka twende Qatar 2022 tukacheze na nani?

Kikosi cha Tanzania, Taifa Stars Kikosi cha Tanzania, Taifa Stars

Tulizikosa pointi sita za Benin tukazipata tatu tu, wakiwa na timu nyepesi. Uwezo wetu ndiyo umeishia hapo. Na ukweli siku zote unauma ingawa ukifanyiwa kazi huwa ni tiba ya kudumu.

Kama tulishindwa kuwafunga Benin hapa kwetu, huko Qatar tulikuwa tunataka kwenda ili tukafanye nini?

Ureno wameshindwa kufuzu moja kwa moja, wanalazimika kusubiri mtoano, hawa wetu kina John Bocco na wadogo zake huko Qatar walikuwa waende wakatembee au!

Mpira ni kazi ya watu siku zote tutasema maneno hayo bila ya kuogopa maoni ya watakayoyasikia.

Tulikuwa bado hatujaiva kuweza kushiriki michuano ya Kombe la Dunia. Ikiwa ushiriki wetu wa michuano ya Afrika ‘AFCON’ ni wa kusuasua, kama ni kwenda World Cup basi ingekuwa ni kwenda kubebeshwa mzigo wa magoli.

Tuna washambuliaji wawili tu wanaocheza mpira wa kimataifa, wakizuiliwa hao, Taifa Stars inakuwa na unyonge muda wote wa mechi.

Kushindwa kwetu kusituumize sana tukajawa na unyonge. Kim Poulsen na wasaidizi wake wamefanya kazi kadri walivyoweza. Tuwaamini na kuendelea kuwapa muda, kuna timu inajengwa na ndani ya mwaka mmoja au miwili itakuwa imeshajengeka.

Kweli kabisa tulitaka jina la Tanzania liwe pamoja na ya kina Brazil, Argentina, Ujerumani na wababe wengine wa soka la dunia hii?

Upo muda unakuja tutakuwa na shauku ya kweli kabisa ya kutaka kushiriki michuano hii, lakini haujafika bado. Tusichoke hata kidogo, tuendelee na kuandaa wachezaji wenye ubora.