Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 06 20Article 543508

Maoni of Sunday, 20 June 2021

Columnist: www.habarileo.co.tz

Tupambane kuibadilisha sekta ya kilimo

Tupambane kuibadilisha sekta ya kilimo Tupambane kuibadilisha sekta ya kilimo

MAENDELEO katika sekta ya kilimo ni muhimu hasa katika kukuza uchumi wa Taifa na kuleta msukumo kwenye ukuaji wa sekta ya viwanda.

Ukuaji wa sekta una umuhimu mkubwa katika kuzalisha chakula cha kutosha kuhakikisha uwepo wa usalama wa chakula na lishe kwa wananchi wakati wote.

Kiukweli, sekta ya kilimo kwa miaka ya karibuni inachangia takribani asilimia 29.1 ya pato la taifa, asilimia 65 ya ajira, asilimia 65 ya malighafi inayotumika katika sekta ya viwanda na asilimia 30 ya pato la bidhaa zinazouzwa nje ya nchi.

Kutokana na ukweli huo, hatushangai kushuhudia wabunge katika Bajeti Kuu ya Serikali wakishauri kuongezwa kwa bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka Sh Bilioni 200 zilizotengwa kwani hiyo ni sekta nyeti katika muda huu ambao nchi ipo katika uchumi wa kati wa chini.

Wabunge hao wameona mbali kwa kuwa, kwa kuwezesha kutekeleza mnyororo wa thamani, wakulima wadogo watakuwa wanaongeza kipato chao, kuwa na uhakika wa chakula na pia kuwezesha kufanya kilimo biashara.

Kwetu sisi, mambo yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, tunaona yanafungamana na Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) ambayo inakusudia kuendelea kuimarisha sekta ya kilimo kwa kasi ili kuifungamanisha na ukuaji wa viwanda na soko lenye uhakika wa bidhaa za wakulima.

Kinachofurahisha zaidi kwa sasa ni kuona kwamba wakati majadiliano ya Bajeti Kuu ya Serikali yakiendelea bungeni huku wabunge wengi wakipigia debe sekta ya kilimo iongezewe fedha katika bajeti yake, serikali pia nje ya Bunge imekuwa ikikutana na wadau mbalimbali yakiwamo mataifa ya nje, kutafuta mwendelezo wa mapambano ya kuongeza tija katika sekta ya kilimo.

Kwa kuwa Programu hiyo yenye lengo la kuleta mageuzi ya sekta ya kilimo (kilimo, mifugo na uvuvi) ili kuongeza uzalishaji na tija na kufanya kilimo kiwe cha kibiashara, inaendelea kutekelezwa huku juhudi zikiendelea kuvuta wawekezaji wakubwa, tunachotaka kusema ni kuitafadhalisha serikali kuhakikisha kwamba kila kitu kinachofanywa katika sekta ya kilimo kinaenda kugusa maslahi ya mkulima mdogo.

Kwa kuwa asilimia 65 ya Watanzania wameajiriwa katika kilimo, tunaamini bila mkulima mdogo kunyanyuka na kuendelea mbele, kilimo cha Tanzania kitabaki kuwa cha kujikimu na hata kilimo biashara hakitakuwepo hasa kwa kuangalia ukweli kuwa tunakumbwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Pamoja na kuyaalika mataifa ya nje na wawekezaji kutoka nje,serikali inatakiwa kuhakikisha kwamba inatumia vyema ASDPll ambayo imefanya sekta mtambuka katika kuimartisha kilimo na sekta yenyewe ili kasi inayotarajiwa katika kuinua sekta ya kilimo iende sambamba na uwepo wa viwanda vidogo na vikubwa na masoko kwa bidhaa zinazozalishwa na wakulima hao.

Katika awamu ya pili ya uchumi wa viwanda ni vyema kuhakikisha kwamba fedha nyingi zinapatikana kuwabadili wakulima wadogo waweze kuwa msaada mkubwa katika uzalishaji wa mali ghafi na hivyo kuibuka kwa viwanda vidogo na vya kati, hatimaye kuwa na viwanda mbalimbali vinavyowezesha kilimo na mnyororo wake wa thamani.

Kama ASDP II imeandaliwa kwa kuzingatia mikakati yote ya taifa: Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025; Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu (2012-2021); Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016- 2021); Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo (2015) na Mpango wa Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo ( TAFSIP 2011), maana yake kwa wadau wote ni rahisi kufanya uratibu na kujua sekta ya kilimo inatolewa kutoka eneo moja hadi jingine.

Kutokana na nchi kuingia katika uchumi wa kati wa chini, miaka ya karibuni na kwa kuwa takwimu za Wizara ya Kilimo za mwaka 2019/2020 zinaonesha asilimia 90 ya ardhi ya Tanzania hulimwa na wakulima wadogo, uwekezaji mkubwa unastahili kufanyika kuleta mageuzi ya sekta ya kilimo na kuchangia katika pato la taifa.