Uko hapa: NyumbaniWallMaoniArticles2021 02 22Article 525754

Maoni of Monday, 22 February 2021

Columnist: HabariLeo

Tusipuuze tahadhari ya TMA mvua za masika

Tusipuuze tahadhari ya TMA mvua za masika Tusipuuze tahadhari ya TMA mvua za masika

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa angalizo la mvua kubwa zinazoweza kunyesha katika baadhi ya maeneo nchini msimu wa mvua za masika katika kipindi cha Machi hadi Mei, mwaka huu.

Mamlaka hiyo imetaja mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Dar es Salaam, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Kaskazini mwa Morogoro, Lindi na Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kutokea hali hiyo.

Athari zinazoweza kujitokeza zinatajwa kuwa ni baadhi ya makazi kuzungukwa na maji pamoja na ucheleweshwaji wa baadhi ya shughuli za usafirishaji.

Ikumbukwe kuwa, hali mbaya ya hewa, kuongezeka kwa joto, vipindi vya mvua kubwa ni matokeo za changamoto za hali ya hewa, hivyo wananchi wanatakiwa kuzingatia taarifa zinazotolewa kila siku kuhusu hali ya hewa ili kubaini changamoto zinazoweza kujitokeza.

Tunaisihi jamii na mamlaka nyingine zinazohusika na mazingira kuzingatia utabiri huo wa Mamlaka ya Hali ya Hewa kuhusu mvua za masika na kujiandaa kuzuia pale inapowezekana na kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.

Tunawasihi wananchi kila mmoja katika eneo lake kuchukua hatua za mapema kusafisha mazingira, kuzibua mapito ya maji pamoja na kusafisha mitaro ili mvua zitakapoanza kunyesha maji yaweze kupita kwa urahisi kuepuka mafuriko.

Kwa wale wanaoishi maeneo hatarishi kama vile mabondeni au pembezoni mwa mito, hiki ni kipindi cha kujiandaa kuondoka katika maeneo hayo badala ya kusubiri mafuriko yatokee kwani ni kuhatarisha maisha yao na mali zao.

Aidha, mamlaka kama vile halmashauri na manispaa zinapaswa kujipanga mapema kuhakikisha mitaro na mito iliyo karibu na maeneo ya makazi ya watu ipo salama na kuzibua maeneo yaliyoziba ili maji yaweze kutiririka bila kizuizi na kwenda kumwagika baharini.

Hata hivyo, wakati watu wengine wakijiandaa kukabiliana na athari za mvua hizo, tunawashauri wakulima kwao wazione ni neema.

Tunawashauri wakulima wajiandae kuzitumia vizuri mvua hizo katika shughuli zao za kilimo ili waweze kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali.

Pamoja na yote hayo, muhimu zaidi jamii inapaswa kuelimishwa kufuatilia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa kila siku ili iweze kukabiliana na hali mbaya zinazoweza kujitokeza na wakulima waweze kuzitumia vyema mvua za misimu na zisizo za misimu katika shughuli zao za kilimo.

Join our Newsletter