Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2022 01 06Article 583747

Maoni of Thursday, 6 January 2022

Columnist: Mwanaspoti

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Bado malaika wa heri anatembea na Ibrahim Ajib

Ibrahim Ajibu Ibrahim Ajibu

Miezi mitano iliyopita nilieleza hapa kwamba, Ibrahim Ajibu amepata bahati kubaki Simba. Simba walimpoteza Clatous Chama na Luis Miquissone pasipo kutarajia, lakini ghafla wakajikuta wanamhitaji Ibrahim Ajibu.

Kabla ya Chama kuondoka Simba waliliweka jina lake ‘kwenye kilengeo’ kwamba Ajibu lazima aondoke. Waliamini Ajibu anawaibia. Kwa miaka mingi Simba waliishi wakiamini Ajibu ana uwezo mkubwa na waliamini ipo siku watafaidi kipaji chake.

Haikuwa hivyo, Ajibu alitumia muda mwingi kukaa benchi na jukwaani kuliko uwanjani. Ndipo Simba waliamua kulifutilia mbali jina lake. Hata walipoenda kujiandaa na msimu (pre-season) kule Morocco hawakwenda naye.

Ndipo ghafla walijikuta wanamhitaji tena baada ya kuondoka kwa Chama. Ikawa bahati kwa Ajibu. Baada ya kupata bahati ya kusalia Simba, Ajibu hakubadilika. Maisha yaliendelea kuwa yaleyale.

Ajibu aliendelea ‘kuishi kifaza’ akijua kwamba ana mkataba wa miaka miwili. Simba walichoka kumvumilia. Wakafikiria kumtoa kwa mkopo katika dirisha hili la usajili. Ghafla Azam FC wakakorofishana na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na wenzake. Wenzake wakarejea klabuni, Sure Boy akakataa na kuomba kuondoka.

Ndipo hapo Azam wakajikuta wakihitaji kuziba nafasi ya Sure Boy. Azam wakapiga hesabu ya kwenda nje ya nchi kuleta kiungo wa kucheza nafasi ya Sure Boy. Wakagundua hawawezi kumpata kiungo mzuri kwa haraka. Ndipo wakalazimika kufikiria kumtafuta kiungo hapa nchini. Ndipo hapo jina la Ajibu lilipotokea Chamazi. Simba walilipokea ombi la Ajibu kuvunja mkataba kwa mikono miwili. Hawakupata walichokitarajia kutoka kwake. Mwanzoni walifikiri labda uwepo wa mastaa wengi ndani ya Simba unamnyima nafasi ya kung’ara.

Lakini hata mastaa mawili wakubwa walipoondoka bado Ajibu hawakuchomoza na kulishawishi benchi la ufundi kwamba anahitaji nafasi katika kikosi cha Simba. Matokeo Simba wakajikuta wakimtumia zaidi Hassan Dilunga na Dennis Kibu kwa sababu walikuwa wakijituma zaidi.

Ndiyo maana lilipokuja ombi la Azam FC, Simba wakamuachia Ajibu aondoke kwa moyo mweupe. Waliamini Ajibu alikuwa akiwaibia na alikuwa anakula mshahara wa bure. Kwa Simba waliona Azam wamekuja kuwatua mzigo waliokuwa wakitembea nao kwa shida.

Kichekesho zaidi cha uhamisho wa Ajibu ni jinsi Azam wenyewe walivyoonyesha hawana imani na mchezaji wao mpya. Azam wamempa Ajibu mkataba wa mwaka mmoja. Hapo unafikiria, mchezaji mwenye umri wa miaka 25 anapewa vipi mkataba wa miezi 12? Mkataba wa muda mfupi hivi wanapewa wachezaji wazee ambao watatumika kwa muda mfupi. Unakuwa na mpango nae wa muda mfupi kisha baada ya hapo unamruhusu aondoke. Kwa mfano Simba wanaweza kumpa Pascal Wawa mkataba wa mwaka mmoja kutokana na umri wake. Ndani ya huo mwaka watajitahidi kumtumia kadiri wawezavyo kisha baadae wamuache aondoke. Kwanini Azam wamempa kijana mdogo mkataba mfupi kiasi hicho kama ni mkongwe wa miaka 37? Ni Imani tu. Hawaamini kama Ibrahim Ajib atakuwa katika ubora mkubwa kwa muda mrefu. Hawataki kutumbukia katika mtego wa Ajib waliotumbukia Simba miaka mitatu iliyopita.

Lakini hapo hapo Azam wanajua hata kama Ajib ataonesha uwezo mkubwa akiwa na jezi yao hawatakumbana na usumbufu mkubwa wakitaka kumpa mkataba mpya. Ajib ameshapita Simba na Yanga, na kwa inavoonekana wale jamaa hawapo tayari kumrudia tena. Azam hawatakumbana na upinzani mkali kutoka kwa Simba na Yanga kama watahitaji kumuongezea mkataba.

Kikubwa sasa hivi kwa Ibrahim Ajib ni kuhakikisha anakamata makali yake akiwa na jezi ya Azam kama anataka kuendelea kusalia katika klabu kubwa nchini. Hizi bahati anazokumbana nazo hazirudi mara nyingi. Kwasasa ni kuhakikisha anaingia katika kikosi cha kwanza cha Azam na kuhakikisha anakuwa staa wa timu. Baada ya Azam siioni timu nyingine kubwa ikijihaingaisha naye. Maisha ya Namungo hayawezi kufanana na Azam au Simba.

Kuhusu yeye kukaa benchi Simba na kupata nafasi Azam havina uhusiano. Labda Azam wanafahamu jinsi ya kumtumia na pengine watafaidika na kipaji chake. Hata Patrice Vieirra hakuwa na namba AC Milan lakini alienda kuwa staa mkubwa sana Arsenal na ligi kuu ya England.