Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 12 23Article 580699

Maoni of Thursday, 23 December 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Dirisha la usajili linakuja na maswali mazito

Dirisha la Usajili limeshafunguliwa Dirisha la Usajili limeshafunguliwa

Kile kipindi kinachosisimua zaidi nchini kimewadia. Kipindi cha usajili. Rafiki yangu mmoja hupenda kutania kwamba Tanzania usajili unavutia zaidi kuliko ligi yake. Ni utani ambao ndani yake kuna ukweli mchungu ambao ni mgumu kuumeza.

Ni kipindi hiki ambacho timu nyingi hutamba kwa kusajili wachezaji na kuwaaminisha mashabiki kwamba wana uwezo mkubwa na wanakuja kukibadilisha kabisa kikosi chao.

Mara nyingi viongozi hutumia kipindi hiki kuwapoza mashabiki kwa kuwaleta mastaa wapya. Sisi mashabiki tunashawishika na kudanganywa na vitu vidogo sana. Tunakuwa wepesi kusahau matokeo mabovu yanayotokea uwanjani kwa kuletewa wachezaji tunaowahesabu kama mafanikio.

Tanzania ni kati ya nchi chache nazozifahamu ambazo usajili wa mchezaji huhesabika kama sehemu ya mafanikio ya timu, huku miundombinu na mataji huwekwa kando. Ukiona haya ujue umefika Tanzania.

Lengo kubwa zaidi la dirisha dogo la usajili ni kuimarisha kikosi kuelekea mwisho wa msimu. Hapa timu hufanya marekebisho kidogo kutokana na udhaifu ulioonekana wakati msimu unaelekea nusu. Dirisha dogo la usajili ni tofauti sana na lile dirisha kubwa la mwisho wa msimu. Dirisha kubwa timu inaweza kufanya ongezeko kubwa kikosini kwa sababu kocha atapata muda wa kutosha kukaa na wachezaji wakati wa maandalizi ya msimu (pre-season).

Ni tofauti na dirisha dogo ambalo unaingiza mchezaji mgeni wakati ligi inaendelea. Mchezaji na kocha hawapati muda wa kutosha kukaa pamoja kuelekezana. Ni kwa sababu hii timu zinahitajika kufanya maingizo kidogo vikosini.

Nilicheka niliposikia klabu fulani iliyopanda daraja inafikiria kuwachinjilia mbali zaidi ya wachezaji wake 15 kwa sababu hairidhishwi na viwango vyao.

Inadaiwa uwezo wao ni mdogo sana kucheza Ligi Kuu Bara. Unajiuliza, swali la kwanza inakuwaje wachezaji 15 kwa pamoja wakafeli ndani ya nusu msimu? Lazima yalifanyika makosa makubwa katika dirisha kubwa la usajili.

Swali la pili unajiuliza, unapata wapi wachezaji wengine 15 wa kuziba nafasi zinazoachwa na wanaokatwa? Unapofikiria pa kutafuta jibu linakuja swali lingine, unapopata wachezaji wapya unawaingiza vipi kwenye timu haraka wakati ligi inaendelea? Ni kichekesho.

Kichekesho kingine ni pale niliposikia timu moja kubwa nchini inasubiri ripoti ya benchi la ufundi ili ianze kusaka wachezaji wa kusajili.

Kichekesho hakipo kwenye kusubiri ripoti ya benchi la ufundi, ni muhimu kulisikiliza benchi la ufundi katika uamuzi wa kiufundi. Ambacho sikubaliani nacho ni kuanza kusaka wachezaji. Huwezi ukaanza kusaka wachezaji kipindi ambacho dirisha limefunguliwa. Kinachohitajika kipindi hiki ni kutekeleza kuwanasa wachezaji ambao klabu ilishajiridhisha kwamba wanapaswa kusajiliwa. Mchezaji anayesajiliwa kipindi hiki alipaswa kuwa amefuatiliwa muda mrefu na kiwango chake kilishawishi kwamba anapaswa kusajiliwa.

Huu sio muda wa kuanza kumfuatilia mchezaji - kuanza kumfuatilia mchezaji kipindi hiki na kumsajili unakuwa hatarini ‘kuinukia koroma’. Ni bora kutosajili kabisa kuliko kusajili mchezaji ambaye hauna uhakika na uwezo wake.

Upo ule ujinga unaofanywa mara nyingi na klabu kubwa nchini kwa kuleta wachezaji kutoka nje kuwafanyia majaribio ili kujiridhisha na uwezo wao. Haya ni matunda ya uvivu wa kufuatilia mchezaji kipindi anacheza katika klabu yake. Huwezi kumfanyia majaribio mchezaji ambaye una uhakika naye.

Lakini muda mwingine klabu hujikuta zinasajili ‘shingo upande’ hata kama hawajaridhika sana na kiwango cha mchezaji kwa sababu tu wamekosa mchezaji sahihi. Majaribio sio njia sahihi ya kufahamu ubora wa mchezaji. Kama unabisha waulize Yanga ilikuwaje wakamsajili Gnamien Gislain Yikpe maarufu kama Yikpe baada ya kumfanyia majaribio.

Ipo imani fulani duniani kwamba dirisha dogo sio dirisha sahihi la kupata mchezaji mzuri. Ni imani tu lakini ndani yake upo uongo na ukweli. Ukweli ni kwamba hakuna klabu inayojielewa ambayo ipo tayari kumuacha mchezaji wake bora asajiliwe katikati ya msimu. Lazima watakuwa na mipango naye ya msimu mzima.

Sababu pekee itakayowafanya wamuache mchezaji wao bora Januari ni kushawishiwa na kitita kikubwa cha pesa au kumuachia kwa pesa ndogo kwa sababu mkataba wake unaelekea mwisho na wana wasiwasi wa kumpoteza bure mwisho wa msimu. Ukiona mchezaji anaachwa kirahisi Januari unapaswa kujiuliza mara mbili.