Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 09 30Article 560509

Maoni of Thursday, 30 September 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Msimdanganye Fei Toto

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Msimdanganye Fei Toto UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Msimdanganye Fei Toto

NI vigumu sana kumkosea mchezaji anayependwa na Watanzania, hakuna atakayekuelewa. Feisal Salum ‘Fei Toto’ ni mchezaji anayependwa na Watanzania.

Mashabiki wa Yanga wanampenda, mashabiki wa Simba wanampenda pia, ni mmoja kati ya wachezaji wazuri mwenye kipaji cha hali ya juu. Utapenda mpira ukiwa kwenye miguu yake, utapenda kuona mashuti yake ya umbali wa mita 20.

Ni mchezaji mbunifu anaweza kupita katikati ya mabeki wa timu pinzani bila kupoteza mpira wake, kumekuwa na changamoto ya namna anavyotumika uwanjani. Wapo makocha ambao wana amani kuwa Fei Toto anafanya vizuri akicheza kama mshambuliaji namba mbili.

Wapo wengine pia wamekuwa wakimtukia kama kiungo mkabaji, kocha wa sasa wa timu ya Taifa, Kim Poulsen na Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi wamekuwa wakimtumia kama mshambuliaji namba mbili lakini bado kuna jambo moja silioni kwa Fei Toto.

Sifa kubwa ya mchezaji anayecheza nyuma ya mshambuliaji ni kufunga na kupiga pasi nyingi zinazozalisha mabao, bado Fei Toto haiwezi vizuri kazi hiyo, pale Yanga hivi karibuni alipita Ibrahimu Ajibu, alicheza pia kwenye nafasi hiyo hiyo.

Ajibu alifanya vizuri sana, alikuwa miongoni mwa wachezaji waliofunga mabao kila kukicha, alikuwa miongoni mwa wachezaji walitoa pasi cha mabao kila kukicha.

Bado simuoni Fei Toto akifanya hivyo, labda ni suala la muda acha tuendelee kumtazama.

Hapo nyuma kidogo, Yanga waliwahi kuwa na kiungo Thabani Kamusoko kutoka Zimbabwe, alikuwa fundi kweli kweli wa mpira.

Alicheza eneo lile lile la Fei Toto, alifunga mabao mara kwa mara, alionekana mara nyingi sana kwenye pasi zilizozalisha mabao.

Hiki ndicho kinachokosekana kwa Fei Toto anafanya kila kitu lakini bado anawastani mdogo sana wa kupiga pasi za mwisho, anafanya kila kitu lakini bado ana uwezo mdogo sana wa kufunga mabao.

Kwa bahati mbaya sana huyu ni mchezaji kipenzi cha Watanzania na pengine haambiwi ukweli.

Aliyewahi kuwa Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike aliwahi kusema Fei Toto ana uwezo hata wa kucheza FC Barcelona. Sijui kama alikuwa anamaanisha Barcelona hii aliyowahi kucheza Xaiv Hernandez na Andres Iniesta au Barcelona ya Chake Chake pale Pemba, Fei Toto akianza kufunga mabao kama kiungo mshambuliaji. Akianza kupiga pasi za mwisho kama kiungo mshambuliaji, kila mtu atamuimba nchi hii, lakini kwa sasa, kina kitu anakosa.

Nimemwona Fei Toto akiwa timu ya Taifa akicheza dhidi ya Congo DR ugenini na dhidi ya Madagascar nyumbani, nimemuona dhidi ya Zanaco FC Wiki ya Wananchi, nimemuona mechi zote mbili dhidi ya Rivers United ya Nigeria.

Nimemwona pia Fei Toto mechi ya juzi dhidi ya Simba, ni kweli ni mchezaji mzuri lakini amepiga pasi moja tu kwenye mechi zote hizo sita iliyozalisha bao dhidi ya Zanaco.

Fei Toto alifunga bao moja tu mchezo dhidi ya Madagascar, wastani wa kuchangia bao moja kwenye mechi sita na sifa anazopewa ni vitu viwili tofauti.

Mchezaji anayecheza nyuma ya mshambuliaji, anatakiwa kuwa na takwimu zinazombeba, unatarajia kumuona akiwa na pasi zilizozalisha mabao walau 10 kwa msimu.

Unatakiwa kumwona akiwa na mabao kuanzia saba hadi 10 kwa msimu.

Hizi namba mara ya mwisho Ligi Kuu Bara zilionekana kwa Iddi Suleiman Nado pale Azam, zilionekana kwa Clatous Chama pale Simba, Luis Miquessone pia pale Simba amewahi kuwa kwenye namba hizo.

Fei Toto bado ana kazi kubwa sana, kuna watu wengi naona wanaendelea kumdanganya eti ana kiwango cha kucheza Barcelona na wengine wanakwenda mbali zaidi na kusema anaweza kucheza pale Manchester United.

Huu ni utani wa kiwango cha Dunia, kiungo mshambuliaji anayeweza kufunga bao moja na kupiga pasi moja ya bao, ni Kiungo wa kawaida sana.

Huu ni muda wa Fei kuonyesha utofauti, huu ni muda wake wa kuwa injini ya timu.

Kwa mahali anapocheza kwa sasa, anatakiwa ama kufunga bao 10+ au pasi za mabao 10+, najua Fei Toto ni kipenzi cha Watanzania lakini bado kuna kitu anakosa, huu ni wakati wake wa kuongeza thamani ya kile anachokifanya uwanjani.

Sifa zimekuwa nyingi sana kwake lakini nadhani bado hajafikia huko, mahali anapocheza kwa sasa pale Yanga, ndiyo mahali alipocheza sana Chama akiwa Simba.

Ukitazama namba za Chama na kulinganisha na zile za Fei Toto ni mbingu na ardhi.

Mkiendelea kusema anastahili kucheza Barcelona wakati msimu uliopita hakufikisha hata mabao matano ya ligi Kuu mtakuwa mnamdanganya.

Mkisema anastahili kucheza pale Manchester United wakati msimu ujao hakufikisha hata pasi tano za mabao mtakuwa mnampoteza kijana wenu.

Fei ni mchezaji anayependwa sana lakini, bado ana kazi kubwa ya kufanya, bado hajawa mtu anayeibeba timu.

Kamusoko amewahi kucheza anapocheza Fei lakini alikuwa tegemezi Kwa timu, alikuwa anafunga mabao muhimu, pasi zake zilikuwa chache ya Donald Ngoma na Obrey Chirwa kucheka na nyavu.

Ibrahimu Ajibu amewahi kucheza hapo anapocheza Fei, alikuwa fundi wa pasi za mabao, alikuwa mtamu kwenye kufunga.

Kumdangaya Fei anaweza kucheza Barcelona au Manchester United hakutomsaidia kuwa mchezaji bora ndani ya timu yake.

Bahati aliyonayo ya kupendwa aigeuze kuwa deni kwake, ni muda wake wa kuibeba Yanga mgongoni, ni zama yake kuwa mfalme wa timu, akiendelea kudanganywa yeye ni mchezaji anayeweza kucheza Barcelona, atakuja kushtuka Fiston Mayele ameshakuwa staa wa timu.

Akiendelea kuamini tayari ana uwezo wa kucheza Manchester United, atakuja kushtuka Khalid Aucho kawa staa wa timu.

Fei ni mchezaji mzuri sana lakini anasifiwa kupitiliza. Bado ana kazi kubwa ya kulithibitisha hilo. Acha tuendelee kunywa mchuzi, nyama ziko chini.