Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 12 16Article 578941

Maoni of Thursday, 16 December 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Muda wa kumtazama Kibwana na Konoute baada ya Derby

Kanoute akigombea mpira na Kiungo wa Yanga, Fei toto Kanoute akigombea mpira na Kiungo wa Yanga, Fei toto

Mara ya kwanza kabisa nilimwona Sadio Kanoute katika pambano la Ngao ya Jamii kati ya Simba na Yanga. Kama iivyokuwa kwa watu wengi Kanoute hakunivutia sana, zilikuwepo sababu mbili za kutokuvutiwa na Kanoute.

Kwanza, alianza eneo la kiungo ambalo ndilo eneo Simba walilokuwa imara zaidi kwa miaka kadhaa iliyopita. Hivyo, mgeni kuja na kuingia kikosini moja kwa moja tena katika pambano kubwa dhidi ya Yanga ilishtua kidogo, wengi walitegemea afanye makubwa zaidi ya aliochukua nafasi yao lakini haikuwa hivo.

Sababu ya pili ilikuwa ni kiwango walichoonyesha viungo wawili wapya wa Yanga, Khalid Aucho na Yanick Bangala, baada ya Bangala na Aucho kuonyesha kiwango kizuri, wengi waliishia kumfananisha Kanoute na akina Aucho, Kanoute akaonekana mchezaji wa kawaida.

Nilimtazama tena Kanoute katika mechi za Ligi Kuu, kisha nikamtazama tena na tena, kisha nikamtazama Jumamosi katika pambano lingine la watani wa Jadi.

Jumamosi alikuwa Kanoute tofauti kabisa na yule aliyeonekana katika pambano la miezi mitatu iliyopita. Bila shaka alicheza mechi yake bora zaidi tangu aanze kuuvaa uzi wa wekundu wa Msimbazi Simba.

Alikuwa na utulivu mkubwa eneo la kiungo akishirikiana vema na Jonas Mkude kuulinda ukuta wa Simba.

Kilichonifurahisha zaidi ni jinsi alivyochagua kufanya mambo ya msingi uwanjani. Hana mambo mengi. Alipiga pasi nyingi salama na kuisaidia Simba kutunza mpira, muda mwingine huhitaji kufanya mambo magumu ili uonekane bora.

Muda fulani alijitwika ujasiri wa kusogea mbele kusukuma mashambulizi, hata nafasi pekee Simba waliyokaribia kufunga lilikuwa ni shuti lake lililofutwa vyema na raia mwenzake wa Mali Djigui Diarra.

Hapo ndipo nilikumbuka maisha ya Kanoute yalivoanza ndani ya Simba, alianza taratibu sana. Mashabiki wa Yanga wakaanza kuwasema Simba wamelamba garasa, hata Simba nao wakaanza kuingia wasiwasi kwamba huenda kweli wamelamba galasa.

Lakini Kanoute aliimarika taratibu, siku baada ya siku akapandisha uwezo wake hadi sasa anaonekana ameimarika zaidi, kumbe si kweli Simba walilamba galasa, ni muda tu ulihitajika kwa Kanoute kuingia kwenye mfumo.

Nakumbuka hata Taddeo Lwanga alipoonekana kwa mara ya kwanza kule Zanzibar kwenye mashindano ya Kombe la mapinduzi alianza kwa kuchechemea na watu walisema Simba wamelamba galasa, ‘Taddeo alikuja kuchochea’ na kila mtu alimkubali.

Ni muhimu kujifunza kuwaelewa wachezaji wapo wanaochukua muda kuzoea mazingira, wapo wachezaji waliowahi kuachwa kwa sababu tu walichelewa ‘kuingia kwenye mfumo’. Pengine walikuwa wachezaji wazuri. Vipi kuhusu Perfect Chikwende wa Simba?

Mchezaji mwingine aliyesisimua zaidi ni beki wa kulia wa Yanga Shomari Kibwana, nafikiri yeye ndiye aliyekuwa shujaa wa mchezo kwa upande wa Yanga.

Kibwana alipambana sana na Denis Kibu kisha baadae akamdhibiti Bernard Morrison aliyehamishiwa upande wake baada ya mabadiliko ya Rally Bwalya, Kibwana ana jambo moja analolifanya kwa ufasaha sana, kulinda lango lake.

Watu wa Yanga hawakuridhishwa na namna alivyokuwa akihusika katika kushambulia ndiyo maana waliamua kwenda DR Congo kumleta Djuma Shaban, kisha upande wa kushoto wakamsajili Bryson David ambaye anaweza kushambulia zaidi kuliko mabeki waliokuwa wanacheza nafasi hiyo, Mustapha Yassin na Saleh Adeyum.

Kocha Nabi bado alikuwa na mapenzi makubwa kwa Kibwana, akaamua kumuhamishia upande wa kushoto ambao amecheza vema hadi sasa. Kibwana ana kitu kimoja anachokifanya kwa umaridadi mkubwa, kulihami lango lake ambayo ndiyo kazi ya msingi ya beki.

Mabadiliko ya soka la kisasa yanataka beki ahusike zaidi katika kushambulia, hili bado Kibwana halifanyi vizuri sana, lakini katika umri wake mdogo bado ana muda wa kujifunza. Cha muhimu zaidi ni kwamba kwa sasa anafanya vema kazi ya msingi ya beki, analihami lango lake vema.

Nakumbuka wakati Juma Abdul anajiunga na Yanga miaka ile alikuwa kama Kibwana, alijua kulihami lango lake vema, baadae alijitambisha kama beki bora zaidi wa pembeni nchini kwa kushambulia, kikubwa Kibwana aendelee kufanya kazi yake ya msingi vema, hizo kazi za ziada atazifanya kadri muda unavokwenda.