Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 12 30Article 582178

Maoni of Thursday, 30 December 2021

Columnist: Mwanaspoti

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Sure Boy, maandishi yalisomeka ukutani

Usajili mpya Yanga, Salum Abubakar Usajili mpya Yanga, Salum Abubakar "Sure boy"

Linapotokea jambo ambalo lilionekana litatokea kwa muda mrefu wazungu wanasema “The writing was on the wall”. Tafsiri isiyo rasmi ni kuwa ‘maandishi yalikuwa ukutani’.

Ndivyo unavyoweza kusema kuhusu usajili wa kiungo mpya wa Yanga, Salum Abubakar Salum ‘Sure Boy’.

Maandishi yalikuwa ukutani kwamba Sure Boy angejiunga na Yanga kama siyo dirisha lililopita basi ilikuwa iwe dirisha hili. Kama siyo hili basi dirisha lijalo. Lakini kwa vyovyote vile Sure Boy hakupaswa kumaliza kucheza soka bila kupita Yanga.

Kwa miaka mingi watu wengi nchini wameishi wakiamini Sure Boy ni shabiki mkubwa wa Yanga.

Inadaiwa hadi mechi za Azam FC dhidi ya Yanga hakuwa anacheza vizuri sana. Hii ni imani tu ambayo sitaki kuiamini sana.

Hakuna shida yoyote mchezaji kuwa shabiki wa timu nyingine kisha akachezea timu nyingine. Soka ni kazi na hupaswi kuweka mahaba mbele.

Hata kule Ulaya, Jamie Caragher alicheza Liverpool kwa mafanikio makubwa sana licha ya yeye na familia yake kuwa mashabiki wa kutupwa wa Everton.

Sifahamu sana kama ni kweli Sure Boy alikuwa shabiki mkubwa wa Yanga, japo pia haishtui yeye kushabikia Yanga. Baba yake, mzee Abubakar Salum alikuwa winga hatari wa Yanga. Kipi ajabu mtoto kumfuata baba? Hata jina la Sure Boy mtoto alirithi kutoka kwa baba.

Huenda baba alichangia Sure Boy kuwa shabiki wa Yanga kama inavyodaiwa.

Hata mashabiki wa Yanga wameishi kwa miaka mingi wakiamini Sure Boy ni mwenzao.

Wameishi wakiamini Sure Boy ni mchezaji wao aliyekuwa anavaa jezi ya Azam FC. Sasa watafurahi kumuona akiwa ndani ya uzi wao wa kijani na njano. Usajili wa kwanza waliofanya dirisha dogo na kutambulishwa kama zawadi ya Krismasi kwao. Usajili ninaopenda kuuita ‘usajili wa kishkaji’. Nitakueleza kwanini.

Kwa miaka mingi Simba, Yanga na Azam wamekuwa na tabia ya kuvizia mikataba ya wachezaji kati yao iishe ili waweze kuwasajili. Hawajawahi kuwa na ujasiri wa kuweka pesa mezani na kuvunja mikataba ili kumpata mchezaji ambaye walikuwa wanamhitaji.

Haishangazi kuona wachezaji wengi wazuri nchini wamecheza timu mbili kati ya hizi tatu kwa kipindi kinachofuatana. Sijui huu woga wa kufanya biashara unatoka wapi.

Mara nyingine utakuta mchezaji hana nafasi katika klabu yake, lakini bado klabu ya pili watakuwa na hofu ya kutuma ofa kumpata.

Sijui kama ni kweli kwamba soka ni biashara huku kwetu. Mchezaji pekee ambaye mpaka leo bado siamini kama hakuvaa jezi ya Simba na Yanga ni mu-Ivory Coast Kipre Tchetche tu.

Alikuwa mchezaji mwenye kipaji kikubwa ambaye viongozi wa Simba na Yanga walikuwa wakimtamani, ila hawakufanikiwa kumpata.

Zaidi sana nafikiri ni ‘Sure Boy’ - ni usajili mzuri kwa Yanga. Anaweza asiende kuingia katika kikosi cha kwanza cha Yanga moja kwa moja, lakini atakwenda kuongeza machaguo (options) katika eneo la kiungo hasa kiungo mshambuliaji.

Sasa Yanga wanaweza kuanza na Feisal Salum ‘Fei Toto’ kisha baadaye akampumzika na kuingia Sure Boy.

Mabadiliko kama haya yanataiongezea timu nguvu. Ni tofauti kidogo na hali ilivyokuwa mwanzo ambapo hawakuwa na mbadala wa moja kwa moja wa Fei Toto.

Sasa Yanga wanaweza kucheza mechi ya Shirikisho (FA) wakamuweka Sure Boy uwanjani kisha Fei Toto akakaa jukwaani na wasiwe na hofu.

Hiki ndicho watakachokikosa Azam FC. Azam wanaweza kwenda nje ya nchi kumsajili kiungo mshambuliaji na wakafanikiwa kumpata zaidi ya Sure Boy, lakini hapo watakuwa wamepunguza idadi ya wachezaji wa kigeni.

Wangeweza kuwa na Sureboy kisha wakatumia wachezaji wa kigeni kuziba maeneo mengine.

Unapokuwa na mchezaji bora wa Kitanzania katika eneo fulani uwanjani unapaswa kumtunza ili utumie nafasi za wachezaji wa kigeni katika maeneo mengine.

Simba wamefanikiwa hili kwa mabeki wao wa pembeni, Yanga wamefanikiwa kwa mabeki wao wa kati.

Mwisho kabisa nafikiri Sure Boy amejiunga na Yanga katika kipindi sahihi cha maisha yake. Ameshaivuna Azam kwa miaka 15 sasa ataivuna Yanga kwa miaka kadhaa kisha atatokomea zake. Kama angejiunga na Yanga miaka 15 iliyopota sidhani kama angedumu kama alivyodumu Azam.