Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 06 03Article 540811

Maoni of Thursday, 3 June 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Tatizo sio Carlinhos kuondoka Yanga

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Tatizo sio Carlinhos kuondoka Yanga UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Tatizo sio Carlinhos kuondoka Yanga

NAIKUMBUKA vizuri Yanga ya Mwenyekiti, Yussuph Manji. Kuna majina ya watu yananijia kichwani namkumbuka Isaac Chanji, namkumbuka Abdalah Bin Kleb, namkumbuka Seif Magari. Hawa walikuwa wanaume haswa. Hawa walikuwa watu wa mpira kwelikweli.

Walijitahidi sana kuzitumia sawasawa pesa za Manji. Walijitahidi mno kuleta wachezaji bora. Walipigana usiku na mchana kuiweka Yanga kwenye ramani, unadhani tatizo ni Carlinhos? Hapana. Siamini katika hilo nadhani tatizo kubwa lipo kwa aliyemleta mchezaji huyo kutoka Angola. Hatimaye Yanga wametangaza kuvunja mkataba na mchezaji wao kutoka Angola, Carlinhos. Nadhani huu ni mwanzo tu, nategemea kuona wachezaji wengi wakiondoka kuelekea msimu ujao. Nategemea watu wengi sana kutimka klabuni hapo. Siamini kama tatizo ni wachezaji, nadhani ni watu waliowaleta.

Yanga bado wanaendesha timu kikomandoo. Yanga bado inaendesha timu kisela. Maisha ya mpira yamebadilika, mpira unazidi kuwa sayansi zaidi. Ni kweli upo usajili mzuri umefanywa msimu huu na mdhamini wa timu hiyo, GSM.

Tonombe Mukoko ni mtu na nusu, Tuisila Kisinda ni mashine kwelikweli, lakini sajili zilizobaki ni za kawaida sana. Sio wachezaji wanaoweza kuipa ubingwa Yanga. Huyu Carlinhos ni matokeo ya kukosa watu makini wa kutengeneza timu pale Jangwani. Yanga ni kubwa sana.

Yanga ni wananchi, haiwezekani kuendeshwa kwa fikra na matakwa ya watu wachache. Yanga ni kubwa sana. Yanga ni mali ya wananchi.

Ukitazama pale kwa watani zao Simba, unaona sura za watu wa kazi. Unamuona mzee wangu, Zacharia Hans Poppe amedumu ndani ya uongozi wa Simba kwa zaidi ya miaka 10. Ukichugulia tena unakutana na Mulamu Nghambi, mtu wa kazi kwelikweli. Amekuwa na Simba kwa miaka nenda rudi. Hii ndiyo tofauti kubwa ya Simba na Yanga. Hiki ndicho kinachofanya Simba iwe imara zaidi kuliko Yanga.

Usisahau pale Simba yuko Crescentius Magori, msomi, mwanamichezo na mzoefu. Huwezi kumpata mtu kama huyu pale Yanga. Watu kama kina Salim Abdallah maarufu kama Try Again, watu kama hawa pale Yanga hawapo. Kama na wewe una amaini kama mimi kwamba Yanga inakosa watu sahihi kwenye uongozi wa timu niandikie maoni yako kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Mpira wetu una sarakasi nyingi sana ambazo Injinia Hersi peke yake hawezi. Mpira wetu una njia zake ambazo GSM peke yao hawawezi. Wanafanya kazi nzuri sana ya kuhudumia timu, lakini wanahitaji watu aina ya Abdalah Bin Kleb, Seif Magari, Isaac Chanji kurejesha heshima ya klabu.

Bila kupata watu sahihi itachukua miaka mingi sana kwa Yanga kuwa na timu bora ya ushindani. Bila kupata watu wa kazi inaweza kwenda hata miaka mitano bila Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Kwa misimu mitatu yote ya hivi karibuni, Yanga wanafanya kazi ya kuleta wachezaji na kuwafukuza. Yanga inafanya kazi ya kuajiri makocha na kuwafukuza. Siioni Yanga ikipiga hatua. Ni Yanga ambayo iko palepale.

Carlinhos hakuwa mchezaji wa daraja la juu, lakini alikuwa na msaada pale Yanga. Kwa aina ya timu ilivyo, alikuwa na msaada. Yanga haipaswi kusajili wachezaji wa kigeni ambao ubora wao ni wa kawaida. kukosekana kwa watu aina ya kina Bin Kleb ndiyo kunawafikisha Yanga hapa walipo leo.

Kabla ya kuanza kufanya usajili wa msimu ujao na kufukuzana pale klabuni, Yanga iongeze nguvu ya watu sahihi kwenye klabu yao. Carlinhos ni miongoni mwa wachezaji tu wataokimbia klabuni hapo. Yanga wasisubiri mpaka mchezaji kama Mukoko naye atake kuondoka.

Yanga wasisubiri mpaka barua ya Kisinda nayo ifike mezani akitaka kuondoka. Wachezaji wana matatizo yao lakini Klabu ya Yanga ina matatizo zaidi na Mwenyekiti wao, Dk Mshindo Msolla lazima abebe lawama zote. Kuna msemo wa mtaani unasema “kama baba utashindwa kutekeleza majukumu yako kwa mkeo, watu wengine watakusaidia.” Kazi ya kiongozi ni kutekeleza majukumu yake.

Namuona mwenyekiti wa Yanga akichemsha katika hili. Baada ya kupata mdhamini na mfadhili, naona kaamua kuwa tegemezi kupitiliza. Naona ameamua kuwaachia mzigo wadhamini wake na yeye amebaki kama mtazamaji tu.

GSM wanasaidia sana timu, mweyekiti anapaswa na yeye kuchangamka. Badala ya kuomba pesa za usajili kwa wadhamini wake alitakiwa kutengeneza kikosi kazi cha wataalamu cha kumsaidia kuimarisha timu na sio makomandoo. Zama za makomandoo zimepitwa na wakati.

Kama na wewe unaamaini kama mimi kwamba tatizo kubwa la Yanga lipo kwenye uongozi, nitumie ujumbe mfupi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Tofauti kubwa sana ya Simba na Yanga katika kipindi cha hivi karibuni iko kwenye uongozi. Yanga inataka kufanikiwa kwa kubahatisha. Bila kuweka watu sahihi kama kina Chanji, Yanga itasubiri sana kupata ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Bila kupata watu kama Seif Magari, Yanga wataendelea kuuota ubingwa. Injinia Hersi anajitahidi sana kwenda kila pembe ya dunia kuwaleta kina Carlinhos, lakini peke yake hawezi.

GSM wanajitahidi sana kuleta wachezaji na makocha lakini peke yao hawawezi. Mwisho watakata tamaa. Mwisho hawatakuwa na nguvu tena. Waswahili wanasema “ukibebwa, bebeka”. Yanga wanasaidiwa sana na GSM kuliko wanavyojisaidia wenyewe, maisha hayapo hivyo.

Mwenyekiti wa Yanga ni kama ameshindwa kutekeleza majukumu yake ya msingi matokeo yake mdhamini anaonekana kama anabeba kila kitu. Simba walishatoka huko miaka mingi. Ni kweli na wao bado wana changamoto zao, lakini sio hizi za Yanga. Walau kuna watu wanaoujua vyema mpira wetu.

Walau watu timu ya ushindi nyuma ya Barbara Gonzalez kama mtendaji mkuu, Yanga kuna Injinia Hersi tu. Yanga kuna mdhamini tu. Baada ya Carlinhos kuondoka, muda si mrefu tutaona kituko kingine. Siku si nyingi tutaona timuatimua nyingine. Yanga ni kubwa sana. Yanga ina watu wengi sana wa kuipeleka mbele. Carlinhos ni sehemu ndogo sana ya tatizo la Yanga. Dk Mshindo Msolla ni kama timu inampwaya kwa sasa. Ni kama baadhi ya majukumu ya msingi kawaachia wafadhili na wadhamini wa klabu hiyo.

Kama Yanga haitapata aina ya watu kama kina Bin Kleb, Chanji, Magari, watasubiri sana.

Huku ndiko uliko mzizi wa tatizo la Yanga na huku. Ndiko kunakoleta tofauti kubwa ya uendeshaji wa klabu baina ya Simba na Yanga.

Pale Simba katika miaka minne ya hivi karibuni, mgeni ni Barbara tu wengine wote ni wazoefu wa kazi. Kwa jitihada za GSM na Injinia Hersi kama wangepata watu kama kina Bin Kleb, timu ingerejea fasta kwenye ubora wake. Timu ingeweza kushindana lakini kwa hali ilivyo, sioni muujiza wowote kwa Yanga.

Yanga ya sasa imejaa wachezaji wageni, makocha wageni na viongozi wageni. Ngumu sana kupata mafanikio kwa staili hii.

IMEANDIKWA NA OSCAR OSCAR

Join our Newsletter