Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 05 14Article 537679

xxxxxxxxxxx of Friday, 14 May 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Ugomvi wa TFF, Yanga umetuvunjia Derby

NIMESOMA taarifa zote za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), nimesoma taaifa zote za Bodi ya Ligi, nimesoma taarifa zote za Yanga, nimesoma taarifa zote za Simba.

Nilichokiona ni marangi rangi tu. Hakuna hata mmoja aliyeeleza sababu za msingi za mechi kutochezeka, nimewasikiliza wasemaji wote, nimewasikiliza wachangiaji wote.

Nilichoona ni mauza uza tu. Nimetoka patupu, hakuna hata mmoja aliyetoa sababu za wazi kwa nini mechi ilipelekwa saa 1 usiku, hakuna hata mmoja aliyeeleza sababu za mechi kubadilishwa muda wa awali.

Hili jambo halikuwa kubwa, halikupaswa kuwanyima watu burudani, lilihitaji mahusiano mazuri tu baina ya Yanga na TFF.

Ni kweli Yanga walikuwa sawa kwa mujibu wa Kanuni lakini busara ingeweza kuona jambo, kuna tofauti kubwa sana kati ya kuahirisha mechi na kuchelewa kuanza.

Mechi awali haikuwa imeahirishwa, ingechelewa tu kuanza, ugomvi wa Baba na Mama, siku zote anayeathirika huwa ni mtoto.

Kwa mazingira haya, tofauti yoyote kati ya Yanga na TFF watakaoumia ni mashabiki tu.

Mabadiliko ni kweli yalitangazwa muda mfupi lakini busara ingeweza kutumika, maisha yangekwenda.

Tanzania ndiyo nchi pekee ambayo mchezaji wa Yanga akipaisha penati pale Uwanja wa Mkapa, utasikia kuna mtu kapoteza uhai kule Mwanza.

Tanzania ndiyo nchi pekee ambayo mchezaji wa Simba akifunga bao, utasikia kuna mtu kazimia kule Lindi.

Mashabiki wanazipenda mno hizi timu, wamenyimwa burudani bila sababu yoyote ya msingi.

Kama mwenzangu ulipenyezewa sababu yoyote ya kutochezwa kwa mechi ya Simba na Yanga Kwa Mkapa siku ya Jumamosi, tafadhali niandikie kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Kumekuwa na mivutano mingi sana kati ya TFF na Yanga ambao, wanaona kama wanaonewa, kuanzia suala la aliyekuwa Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera kupewa adhabu na TFF kwa sababu ya mavazi.

Yanga walijihisi wanyonge mbele ya TFF hii ya Rais Wallace Karia, likaja suala la aliyekuwa mchezaji wa Yanga, Bernard Morrison kuidhinishwa kuichezea Simba, hapa napo Yanga walijiona wanyonge tena mbele ya TFF.

Likaja tena suala la kufungiwa miaka mitano kwa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, hapa napo Yanga wamezidi kuwa wanyonge, bila kujali walikuwa na haki ama laa lakini unyonge wao kwa TFF hii uko pale pale.

Hisia hizi na mahusiano duni baina ya Yanga na TFF, yamechangia kwa kiasi kikubwa kutunyima mchezo wa Derby ya Kariakoo, nimewasikiliza TFF, nimewasikiliza Bodi ya Ligi, nimewasikiliza Yanga, nimewasikiliza Simba lakini, sijaona sababu yoyote ya Msingi. Kama mwenzangu ulibahatika kupenyezewa sababu yoyote ya maana ya mechi hiyo kutofanyika, nijuze na mimi kupitia namba ya simu hapo juu.

Kulikuwa na shabiki wa Yanga ambaye ametoka Kigoma kwa mguu kuja kutazama Derby ya Kariakoo, kulikuwa na watu wamekata tiketi zao za ndege ili baada ya mechi warudi makwao, kulikuwa na watu wako kwenye funga ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, kulikuwa na watu ambao walikuwa wanakwenda uwanjani kwa mara ya kwanza. Tumewafikiria kweli watu hawa?

Kuna dhambi kubwa sana imefanyika wikiendi iliyopita, kuna kazi kubwa sana ya kuwaponya waliovunjika moyo, nataka niamini mahusiano mabaya kati ya Yanga na TFF na Kanuni zetu zenye mwanya ndiyo yametufikisha hapa.

Kuna haja ya kuongeza kipengele kwenye Kanuni zetu kinachohusu kuchelewa kuanza kwa mechi, Yanga wamepita hapo hapo, ni mwanya ambao lazima uzibwe, nimesoma taarifa zote lakini sijaona mtu hata mmoja akieleza sababu zenye mashiko, labda taarifa zilikuwa za kiusalama zaidi.

Labda taarifa zilikuwa za siri mno lakini, mashabiki wa soka nchini wamekosewa sana. Ukubwa wa klabu hizi sio pesa na majengo yao tu, ni mamilioni ya watu ambao wamekuwa wakiwaunga mkono.

Kutochezwa kwa mechi hiyo ni kutowaheshimu mashabiki, hadi sasa sijaelewa Taasisi yoyote iliyolizungumzia jambo hili, TFF sijawaelewa, Bodi ya Ligi sijawaelewa, kama umepata taarifa yoyote ya uhakika, tafadhali nijulishe kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Kuna haja ya TFF na Yanga kutengeneza upya mahusiano yao, Kanuni zinaweza kuwepo lakini busara na mahusano mazuri ni msingi wa jambo lolote. Simba hawakuwa na tatizo la mabadiliko ya muda. Waliheshimu Mamlaka na wana mahusiano mazuri pia na TFF.

Hata wao wangeweza kususa lakini waliheshimu pia uwepo wa mashabiki wao, kuchukuwa pesa za mashabiki, wengine wamefukuzwa uwanjani kwa vurugu inasikitisha sana, mtu ametoa pesa yake ili apate burudani, kakosa alichofuata, hakurudishiwa pesa yake halafu, anatolewa kwa kusukumwa. Inaumiza sana, wakati mwingine kuomba msamaha peke yake haitoshi, kuna wakubwa wengi wanatakiwa kuwajibika ili kurudisha imanai ya mashabiki.

Nimesoma taarifa zote za TFF, nimesoma taarifa zote za Bodi ya Ligi. Nimesoma zote za Yanga, nimesoma taarifa zote za Simba lakini sijaona hata elewa aliyeeleza sababu zenye mashiko za kwa nini mechi haikuchezwa siku ya Jumamosi.

Kama mwenzangu uliwaelewa, nijuze na mimi kupitia namba yangu ya simu hapo juu, nimeona mauza uza, mwenzio nimeona mapicha picha tu.

Imeandikwa na OSCAR OSCAR

Join our Newsletter