Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 08 19Article 552388

Maoni of Thursday, 19 August 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Umeiona karata ya bahati ya Ibrahim Ajib?

Ibrahim Ajib Ibrahim Ajib

PHIL Ivey wa Las Vegas - Marekani anatajwa kuwa mcheza kamari mwenye bahati zaidi duniani. Moja kati ya michezo migumu zaidi ya kamari ni ile ya kubashiri namba zitakazotokea katika droo inayochezeshwa na mashine.

Unabashiri namba zako kumi na mbili ambazo unaamini zitatokea muda droo inafanyika. Zikitokea kuanza namba sita ulizobashiri unakuwa mshindi, unapata pesa kulingana na idadi ya namba ulizobashiri kwa usahihi.

Huyu Phil Ivey aliwahi kucheza na kupata namba zote kumi na mbili. Akashinda mamilioni ya dola. Kesho yake aliitwa katika kituo kimoja cha televisheni kwa ajili ya mahojiano.

Wakati anaenda akaamua kununua tiketi nyingine na kuicheza kama mfano wakati anafanya mahojiano. Huwezi kuamini hiyo tiketi ya mfano pia alipata kwa usahihi namba zote kumi na mbili. Akachukua mamilioni ya dola kwa mara ya pili. Bahati iliyoje kuwa milionea wa dola ndani ya siku moja?

Leo nimemkumbuka sana mkamaria Phil Ivey baada ya kusikia Ibrahim Ajib anaongeza mkataba wa kukipiga Simba kwa miaka mingine miwili.

Hakuna kingine cha kusema kwa Ajib zaidi ya bahati. Hadi kufikia mwisho wa msimu uliotamatika jina la Ibrahim Ajib tayari lilishawekwa kwenye kilengeo kwamba lazima aondoke.

Viongozi wa Simba waliona hakuna sababu ya kuendelea kuwa na Ajib kikosini kwa sababu ‘hakuwa na maajabu yoyote.’ Ajib waliyemsajili kwa mkwara kutoka Yanga miaka miwili iliyopita siyo Ajib aliyevaa jezi ya Simba.

Sababu kubwa iliyochangia anguko la Ibrahim Ajib ni kutojituma. Mwingine anaweza kusema upana wa kikosi cha Simba, lakini hii hoja naiona hafifu. Kwa kipaji alichonacho Ibrahim Ajib sio mtu wa kuwekwa nje ya uwanja mwaka mzima na Larry Bwalya.

Sababu pekee inayonunulika ni kutojituma.

Haina mantiki sana kuitafuta sababu ya anguko la Ajib. Tunachokifahamu wote ni kuwa Ibrahim Ajib alikuwa anatemwa na Simba kwa sababu hakuwa na manufaa yoyote kwao.

Hata katika kikosi kilichokwenda Morocco kwa ajili ya maandalizi ya msimu hakujumuishwa. Simba walijua kwa jinsi yoyote ile watafanikiwa kuachana na Ibrahim Ajib.

Lakini Wakati Simba wanafikiria kuachana na Ajib, malaika wa bahati bado alikuwa anaangaza upande wake. Simba walijikuta wanampoteza Luis Miquissone na Clatous Chama kwa pamoja. Bahati mbaya sana kwa Simba wamempoteza Chama na Miquissone wakiwa hawajawaandaa wabadala wao. Wakapata kazi ya pili kuanza upya kutafuta warithi.

Ni katika harakati za kutafuta mrithi ndipo wazo la kumbakiza Ibrahim Ajib liliporejea. Licha ya kwamba Simba imewasajili wachezaji wapya watakaoziba nafasi ya Chama na Miquissone bado hawana uhakika kama wataweza kuziba mapengo ya kina Chama kwa haraka. Vipi kama hawa wageni watafeli?

Inabidi wawepo watu watakaokuwa mbadala (back up). Hapo kwenye mbadala ndipo jina la Ajib limejikuta likirejea tena Simba.

Hapa ndipo bahati ilipoangukia katika mikono ya Ajib. Vipi kama Chama na Miquissone wasingeondoka? Labda msimu ujao tungemuona Ibrahim Ajib ndani ya uzi wa machungwa wa KMC, huwezi kujua!

Lakini stori zingine za mtaani zinadai Ajib anapendwa sana na mabosi wa Simba, ndiyo maana hawezi kuondoka kirahisi.

Kwa lugha rahisi ni mtoto wa nyumbani, yeye na swahiba wake Said Hamis Ndemla. Kila majina yao yanapochorewa mstari mwekundu wanajitokeza viongozi kadhaa wanawapigia vifua waendelee kubaki kikosini.

Mtu mwingine aliyekutana na bahati ambaye jina lake lilishapitishiwa mstari mwekundu ni la Mzimbwabwe Perfect Chikwende. Kesi ya Chikwende ni tofauti kidogo na ile ya Ajib.

Kilichokuwa kinasababisha Chikwende aliwe kichwa pale Msimbazi ni uraia wake. Tayari Simba ilishakuwa na wachezaji kumi wa kigeni.

Ilihitaji kupunguza wachezaji wapya ili wapate nafasi ya kusajili wageni wengine. Wakati wakifikiria kumkata Chikwende na Meddie Kagere, ghafla idadi ya wachezaji wa kigeni ikaongezwa hadi kumi na mbili.

Hapo ndipo Chikwende alipopona na kupewa nafasi ya pili ya kujitetea. Kama sio idadi ya wageni kuongezwa, Chikwende angeshakutana na salamu za ‘goodbye’ siku nyingi.

Mwisho kabisa bahati imewapa Ibrahim Ajib na Perfect Chikwende nafasi nyingine ya kujitetea. Kama watashindwa tena wanaweza kukutana na mlango wa kutokea Simba.

Binafsi ninaweza kumuwekea dhamana Chikwende, lakini siyo Ibrahim Ajib. Labda Chikwende hakuonyesha makali yake kwa sababu ya changamoto ya ugeni. Tukumbuke hata Miquissone alianza kwa kuchechemea.

Labda Chikwende gari litawaka na tutamuona yule wa Platinum dhidi ya Simba kwenye micuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kipindi kile. Kuhusu Ajib sijui kama lipo jipya la kutarajia kutoka kwake, nadhani atasaini kandarasi yake ya miaka miwili kisha aendelee kufurahia safari na mshahara wake akiwa benchi.