Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 09 02Article 555097

Maoni of Thursday, 2 September 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Umemuona Haji Manara?

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Umemuona Haji Manara? UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Umemuona Haji Manara?

KUNA wasemaji wengi sana wa timu lakini, kuna Haji Manara mmoja. Amejaa mbwembwe, amejaa tambo, anaujua mpira vizuri. Ni kati ya watu wachache wanaotaka kuubadilisha upepo. Moja kati ya mambo ya kupongeza ni kuona Manara anatoka Simba na kwenda Yanga, kumbe umefika wakati wa mpira wetu kuwa biashara, kumbe umefika wakati wa mpira wetu kuwa ajira rasmi.

Kwenye ajira hakuna mtu ambaye huwa anaulizwa timu anayoshabikia, huwa unaulizwa kuwasilisha CV yako tu, kwenye biashara hakuna mtu ambaye huwa anaulizwa timu anayoshabikia, unahitaji kuwa na pesa tu.

Ndiyo maana unaweza kwenda kununua jezi ya Simba popote hata kama wewe ni shabiki wa Yanga, ndiyo maana unaweza kununua tiketi ya mechi ya Yanga na ukaruhusiwa kuingia uwanjani hata kama wewe ni Simba.

Hiki ndicho Manara alichofanya, ameamua kutumia taalamu yake ya habari kufanya kazi, ameamua kutumia taaluma yake ya Habari kufanya biashara, wapo wengi wamepongeza maamuzi ya Manara.

Wapo pia waliokwazika na maamuzi hayo, umemuona Manara? Nipe maoni yako kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Tayari Manara hakuwa na nafasi tena ndani ya Simba, tayari uamuzi wake wa kuondoka Simba umeshakubaliwa na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi.

Manara hakuwa na chake tena ndani ya Msimbazi, anapotoa Yanga na kukupa nafasi, unachowaza zaidi ni taaluma yako. Familia yako na utu wako, Manara anaweza kuwa na mapungufu mengi sana lakini, anaushawishi mkubwa sana kwa mashabiki wa soka wa nchi hii.

Manara anaweza kuwa na maneno ya kukera kuliko mtu mwingine yoyote lakini, anajua namna ya kuwahamasisha mashabiki wa soka wa nchi hii, kwa mtu mwenye familia, kwa mtu mwenye kutaka kuendeleza taaluma yake, hakuna namna angeikataa ofa ya Yanga.

Unaweza ukawa shabiki wa Simba lakini unaishi Mwembe Yanga, unaweza kuwa shabiki wa Yanga lakini makazi yake ni pale Msimbazi. Ofisa Habari ni kazi kama zilivyo kazi nyingine. Kuna Maofisa Habari wengi sana nchi hii lakini kuna Manara mmoja tu, Manara anajua na kufuatilia sana mpira, una uwezo wa kuizungumzia timu yoyote ya Ligi Kuu Bara na kwa usahihi. Anafuatilia soka, ni mtu wa soka hasa, ni Mwanahabari na Mtoto wa Mjini, Manara ana watu.

Umepokeaje Taarifa za Manara kujiunga na Yanga? Nipe maoni yako kwa kutuma ujumbe mfupi kwenye namba yangu ya simu hapo juu.

Upepo na tamaduni za Simba na Yanga ni lazima nazo ziende kwenye mabadiliko, lazima tufike mahali Yanga wakimtaka Barbara Gonzalez wampate na uwe tayari kuwatumikia. Simba wakimtaka Injinia Hersi Said wampate na awe tayari kuwatumikia.

Ndiyo mpira wa Dunia nzima, ushabiki upo, kazi pia ipo, ikitokeza Yanga wanauza hisa, mtu yoyote aruhusiwe kununua. Ushabiki na nafasi yake, kazi pia ipewe nafasi yake, ukitazama namna Tamasha la Wiki ya Mwananchi lilivyonogeshwa na Manara, unapata hamu ya kujua nini kitatokea siku ya ‘Simba Day’.

Hapa sasa ndiyo patamu hapa sasa ndiyo pakusubiri na kuona, nategemea kuwaona Simba wakija kitofauti, nategemea kuwaona Simba wakija kibingwa zaidi. Sidhani kama watataka kumleta Manara mwingine, nawaona wakija kitofauti, Manara ameiamsha Yanga, mmoja kati ya vitu vitakavyompa urahisi kazini kwake msimu ujao, ni endapo Yanga watakuwa na timu bora.

Ametoka kuisemea timu iliyoko juu, ametoka kuwasemea Mabingwa wa nchi, anahitaji kubaki juu hapo hapo, kwa namna ukitazama kikosi cha Yanga na maandalizi yake, unaiona Yanga ikiwa juu? Nitumie maoni yake kwa ujumbe mfupi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Yanga wamefanya usajili mzuri lakini, wanahitaji ubora wa Kocha kuitengeneza timu, kuwa na wachezaji wazuri ni jambo moja, kuwa na timu nzuri ni jambo lingine.

Nimewatazama Yanga dhidi ya Zanaco FC licha ya kufungwa lakini wananipa wasiwasi mkubwa sana, ni kama sehemu kubwa ya wachezaji wao bado hawana utimamu wa mwingi kwa ajili ya mashindano.

Ukitazama kambi yao ya nchini Morocco, nayo pia inatia mashaka kama kweli timu imeandaliwa kikamilifu, hili ndiyo eneo ambalo Manara linaweza kuifanya kazi yake kuwa ngumu kidogo.

Muda bado upo kwa Yanga kuimarika, muda bado kwa Kocha kuitengeneza timu, umepokeaje maamuzi ya Manara kujiunga na Yanga? Nipe maoni yake Kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Kocha wa Yanga Nasreddine Nabi ana kazi kubwa sana msimu ujao kaliko msimu uliopita alipopokea timu. Baada ya Yanga kufanya usajili mzuri, watu wanataka kuona timu yao imevuna pointi za kutosha na kucheza mpira mzuri .

Hapa ndiyo pazito kwa Nabi, baada ya kwenda msimu minne bila kutwaa Kombe lolote kubwa, Yanga wanataka makombe na Nabi anapaswa kulijua hilo.

Stori za kusema tunajenga timu, sidhani kama mashabiki wa Yanga wanataka kuzisikia, wanataka kuona soka safi na matokeo ya ushindi. Tunategemea msimu wa aina yake. Kila la kheri Nabi , kila la kheri Manara .