Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 06 25Article 544201

Maoni of Friday, 25 June 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

UCHAMBUZI: Agizo la Rais Samia viwanja lifanyiwe kazi haraka

UCHAMBUZI: Agizo la Rais Samia viwanja lifanyiwe kazi haraka UCHAMBUZI: Agizo la Rais Samia viwanja lifanyiwe kazi haraka

JUNI 15 mwaka huu, Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Samia Suluhu Hassan alikiomba Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ni wamiliki wa viwanja vingi vya michezo nchini kuviwekea nyasi za bandia.

Kati ya viwanja vinavyomilikiwa na chama hicho ni Jamhuri Morogoro na Dodoma, Sokoine (Mbeya), Kirumba (Mwanza), Kambarage (Shinyanga), Karume (Musoma), Sheikh Amri Abeid (Arusha), Majimaji (Songea), Liti (Singida), Samora (Iringa), Sabasaba (Njombe) na Nelson Mandela (Sumbawanga)

Viwanja vingi hutumika kuchezea mechi za Ligi Kuu Bara hata zile za madaraja ya chini lakini vilivyo vingi vina hali mbaya jambo ambalo wakati mwingine husababisha kufungwa na timu kutotumia viwanja hivyo.

Kiukweli ni kama alivyosema Rais Samia kwamba viwanja haviridhishi, ni kweli havina ubora wowote na vingine ni kama vimetelekezwa tu, huku wamiliki wakikaa kimya kwa maana ya kutojihusisha navyo.

Sasa Rais ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho, ametoa ruhusa baada ya kufuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya nyasi bandia ambayo wengi ilikuwa inawaumiza.

Naamini CCM wakifanya hivyo basi hata wao wataingiza pesa nzuri hasa pale ambapo michezo inatumika kwenye viwanja hivyo kwani wahusika wa michezo ni lazima walipie na wao kuingiza kipato.

Agizo hilo lilielekezwa pia Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo ambao walitakiwa kuandaa program ya kuboresha viwanja hivyo kwani wao ndiyo wenye dhamana ya kusimamia michezo nchini.

Tunakoelekea ni wazi kuna maendeleo makubwa michezoni, kwani mwaka huu Kampuni ya Azam ilitangaza kuweka taa kwenye baadhi ya viwanja ili kuwapa fursa wananchi kuangalia mechi za Ligi Kuu Bara hata nyakati za usiku.

Sasa hili jambo linoge zaidi basi uwepo wa taa hizo za kisasa ni lazima uendane na ubora wa viwanja husika, sio leo hii Azam watumie pesa zao nyingi kuwekeza kwenye viwanja hivyo lakini vishindwe kutumika kutokana na ubovu.

Kama mnakumbuka msimu huu, Bodi ya Ligi haikuwa tayari mechi zichezwe kwenye viwanja vibovu ndiyo maana walifungia viwanja zaidi ya vitano ambavyo kwa asilimia kuwa vinamilikiwa na chama hicho.

Sidhani kama Azam na Bodi watakuwa tayari kuona jambo hilo linajitokeza tena msimu ujao, waweke taa halafu kwenye ‘pitch’ kuwe kubovu, hayo yatakuwa matumizi mabaya ya fedha.

CCM itambue na kuthamini mchango wa wengine waliojitolea kuweka taa kwenye viwanja vyao nao waonyeshe juhudi za haraka za kutengeneza ama kuboresha viwanja hivyo ili mambo yanapokamilika basi yaende yote kwa wakati mmoja.

Lengo ni kujenga na kuleta maendeleo kwa pamoja ambayo yatasaidia kukuza uchumi wa nchi lakini lisipozingatiwa hili bado tutakuwa nyuma kwenye maendeleo ya mchezo hususani mchezo pendwa wa soka.

Chama tawala, kwa mara nyingine mnaombwa kuunga mkono na juhudi za Rais Samia kwa haraka sana kwenye maboresho hayo hata kama hamtaanza viwanja vyote basi angalau vile vinavyotumika mara kwa mara na vinaongoza kwa kufungiwa.

Hebu fikiria Uwanja kama Jamhuri jijini Dodoma ambao upo makao makuu ya nchi, hauna hadhi kabisa ingawa kuna uwanja wa kisasa utajengwa hapo baadaye na huo utaojengwa utakuwa chini ya serikali na sio chama.

Hivyo kuna haja ya viwanja kama hivyo kuvifanyia haraka maana timu nyingi ama michezo mingi hutumia uwanja huo, yasisababishwe matatizo ya kiafya kwa wanamichezo ambayo yanaweza kukingwa mapema.

Ndio, wachezaji hupata matatizo hata kwenye viwanja vizuri lakini ni tofauti na majeraha wanayoyapata kwenye aina hiyo ya viwanja chakavu, na hata soka lao halipendezi kwani wanakwenda kwa kubutua tu.

Kubutua huko kunatokana na vipara vilivyomo ndani ya eneo la kuchezea, na msiombe mvua inyeshe, shughuli ndiyo inakuwa ngumu zaidi.

Agizo lifanyiwe kazi haraka,.