Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 09 05Article 555376

Maoni of Sunday, 5 September 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

UCHAMBUZI: Hesabu ziwe asubuhi kufuzu kombe la Dunia

UCHAMBUZI: Hesabu ziwe asubuhi kufuzu kombe la Dunia UCHAMBUZI: Hesabu ziwe asubuhi kufuzu kombe la Dunia

FAINALI za Kombe la Dunia la FIFA ndio mashindano makubwa na yanayofuatiliwa na watu wengi zaidi duniani kuliko mashindano yote ya mchezo wa soka.

Ndio maana kila nchi huwa na utashi mkubwa wa kutaka kushiriki katika mashindano hayo kwa kuwa ndio kipimo kikuu cha mafaniko ya soka kwa nchi lakini hata kwa wachezaji na benchi la ufundi pia.

Wiki iliyopita tumeshuhudia hatua ya pili ya mechi za awali za kuwania kufuzu ushiriki wa Kombe la Dunia la Fifa 2022 zinazotarajiwa kufanyika Qatar zikiendelea kuchezwa katika mabara yote.

Kwa upande wetu, Afrika tumeona mechi mbalimbali zikitawaliwa na matokeo ya sare kwa mechi za kwanza kama vile Afrika ya Kati waliotoka sare ya 1-1 dhidi ya Cape Verde, Guinea Bissau 1-1 Guinea, Kenya 0-0 Uganda huku timu chache zikipata ya ushindi mdogo kama vile kama vile Misri 1-0 Angola, Libya 2-1 Gabon. Achana na mabingwa wa Afrika, Algeria ambao waliwachakaza 8-0 vibonde Djibouti.

Kwa upande wa timu yetu ya taifa, Taifa Stars, tumeshuhudia vijana wetu wakipata matokeo ya sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika mechi iliyochezwa katika mji wa Lubumbashi.

Ikumbukwe kuwa hatua hii ya makundi katika mashindano haya ni ya pili kabla ya kuingia hatua ya tatu na ya mwisho ambapyo itazijumuisha timu kumi (10) tu ambazo ndio zitapangiwa kila mmoja mpinzani wake katika play-off ya kupata timu tano za kuwakilisha Bara la Afrika katika fainali hizo.

Hatua ya awali ilikuwa ni ya mchujo ambapo Shirikisho la Soka Afrika (Caf) lilizikutanisha timu zilizo chini kabisa katika msimamo wa ubora wa viwango vya Fifa.

Hatua hiyo hata sisi Tanzania tulicheza dhidi ya timu ya Taifa ya Burundi na katika mechi zote mbili tulipata matokeo ya sare ya 1-1 na kutulazimisha kwenda kwenye hatua ya kupigiana penalti, ambayo tulifanikiwa kuvuka.

Igawa mechi hizi za awali huwa hazitiliwi umakini sana kama mechi za hatua ya mwisho zikiwemo mechi za fainali zenyewe, lakini mechi hizi ndio msingi wa kila kitu.

Mataifa ambayo leo hii tunayaoana yameendelea katika mchezo wa soka yalianza kuwa na mikakati ya mechi za awali kwanza na kuwekeza nguvu katika mechi hizi kwani bila ya hatua ya awali hakuwezi kuwa na hatua ya mwisho.

Watanzania tunapaswa kuweka mikakati ya kushinda mechi hizi za mapema za hatua ya makundi, hata kama bado hatujawa tayari kushiriki fainali za Kombe la Dunia.

Nasema hatujawa tayari kushindana kwa levo hizo za dunia kwa sababu bado kiwango cha soka letu kiko chini ukilinganisha na viwango vya timu nyingine za taifa kama Senegal, Tunisia, Algeria, Morocco na Nigeria ambazo ndio zinaongoza katika nafasi tano za juu za ubora wa soka kwa Bara la Afrika.

Katika mechi za awali kama hizi timu hutakiwa kuwa na mikakati stahiki na mipango ya kutumia vema uwanja wa nyumbani.

Tanzania baada ya kupata sare katika mechi ya kwanza ugenini kule DR Congo, tunaweza kuyatumia matokeo haya kama ngazi ya kutufikisha mbali katika kampeni hizi za kufuzu.

Sare hii ina manufaa makubwa kwetu.

Kama kikosi cha Stars kilichojaza vijana wengi kiliweza kupata sare dhidi ya timu ya DR Congo tena ugenini, maana yake ni kwamba tunaweza kujiwekea malengo ya muda mfupi ya kuhakikisha tunapata alama tisa katika mechi zote za nyumbani tukianzia na mechi ijayo dhidi ya Madagascar.

Sare ile hakika itasaidia kuwajenga wachezaji kisaikolojia lakini pia kuhamasisha mashabiki kuiunga mkono timu ya Taifa kama wanavyoziunga mkono klabu za Simba na Yanga kwenye matamasha yao ya Siku ya Mwananchi na Simba Day.

Leo hii sisi katika viwango vya ubora vya Fifa tupo katika nafasi ya 135, Congo DR iko nafasi ya 65, wakati wapinzani wengine wa kundi letu, Benin wako katika nafasi ya 86 na Madagascar wako nafasi ya 97.

Kwa mujibu wa viwango hivyo vya ubora wa soka, sisi ndio ‘underdogs’ wa kundi na kwamba kila timu itakuwa na ndoto ya kutufunga ili kujiweka katika nafasi nzuri.

Lakini sare ya ugenini dhidi ya DR Congo katika mechi ya juzi ambayo kiuhakika tulitengeneza nafasi nyingi nzuri zaidi ya zile walizotengeneza wenyeji ambazo zingeweza kutupa ushindi, inaweza kutumika kama hamasa ya kushinda mechi ijayo nyumbani dhidi ya Madagascar.

Tukomae katika michuano ya mwaka huu ili tupate hamasa ya kufika mbali zaidi katika kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2026 ambazo timu shiriki zinatarajiwa kuongezeka kutoka 32 na kuwa nyingi zaidi.