Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 06 05Article 541165

Maoni of Saturday, 5 June 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

UCHAMBUZI: Kwaheri mtumishi hewa wa Yanga, Carlinhos

UCHAMBUZI: Kwaheri mtumishi hewa wa Yanga, Carlinhos UCHAMBUZI: Kwaheri mtumishi hewa wa Yanga, Carlinhos

JUMATATU, Mei 31 mwaka huu, Yanga ilitangaza uamuzi wa kuachana na kiungo kutoka Angola, Carlos Sténio Fernandes Guimarães do Carmo ‘Carlinhos’.

Ilikuwa ni mwisho rasmi wa matumaini makubwa ambayo mashabiki, wanachama, viongozi na wadhamini wa Yanga walikuwa nayo kwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 26, mzaliwa wa Luanda pale Angola.

Mkataba baina ya pande hizo mbili ulilazimika kuvunjika baada ya Yanga na Carlinhos mwenyewe kufanya mazungumzo na kuamua kusitisha mkataba baina yao kwa manufaa ya kila upande (mutual agreement)

Kabla ya mkataba huo wa Carlinhos kuvunjwa na klabu hiyo kuridhia kuachana naye, kulikuwa na matarajio makubwa ambayo wengi walikuwa nayo kwa kiungo huyo mshambuliaji.

Kiwango bora alichokionyesha katika baadhi ya mechi alizocheza akiwa na jezi ya Yanga kilionekana kuwakosha wengi na ilionekana kama angekuwa mkombozi wa timu hiyo katika kipindi chote cha mkataba wake.

Akili ya haraka ya kuusoma mchezo kufanya maamuzi pindi awapo na mpira, ufundi wa kuchezesha timu, kutengeneza nafasi na kufunga mabao, vilimfanya Carlinhos awe kipenzi cha wengi.

Kwa namna alivyokuwa akipendwa ndani ya klabu hiyo, wengi hawakutarajia kuona Carlinhos akiachana na Yanga mara baada ya kuitumikia timu hiyo kwa msimu mmoja tu.

Wapo wanaoweza kuilaumu na kuishangaa Yanga kwa kukubali kuachana na nyota huyo kirahisi katika kipindi hiki ambacho tayari timu hiyo imeshaanza kuonyesha muelekeo wa kuwa na kikosi bora na chenye ushindani, huku Carlinhos akiwa ni miongoni mwa wachezaji ambao wanaonekana kama ndio watu wa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha hilo linatimia.

Lakini pamoja na ubora na uwezo wa Carlinhos ndani ya uwanja, itakuwa sio sawa kuibebesha Yanga mzigo wa lawama kwa uamuzi huo wa kuachana na mchezaji huyo baada ya kuwatumikia kwa muda usiozidi msimu mmoja na klabu hiyo ilikuwa na sababu za msingi za kumfungulia milango Carlinhos.

Hakuna ambaye hakuridhika na uwezo wa Carlinhos uwanjani, lakini maisha yake binafsi pamoja na tabia havikuendana na hadhi na thamani aliyokuwa akipewa ndani ya timu hiyo tangu walipomsajili.

Japo ilikuwa inafichwa na Yanga wenyewe, mara nyingi Carlinhos alizikosa mechi nyingi za timu hiyo bila sababu za msingi huku akitumia muda wake katika maeneo ya starehe

Mara kadhaa Yanga ilikuwa inamtetea Carlinhos kwa kudai ana majeraha lakini nyuma ya pazia mchezaji huyo aligubikwa na matukio mengi ya utovu wa nidhamu ambayo mengine yalijionyesha wazi.

Kuna nyakati aligoma kucheza kisa tu kile kilichodaiwa hakufurahishwa na uamuzi wa Yanga kuwataka wachezaji wote waishi kambini Kigamboni na badala yake akawa anataka yeye aishi nje ya kambi.

Hiyo imepelekea acheze idadi ndogo ya mechi katika Ligi Kuu Bara msimu huu ambayo haiendani na gharama ambazo Yanga imezitumia katika kumsajili na kumhudumia nyota huyo kutoka Angola.

Wakati wenzake wa kigeni wengi wakijitahidi kuwa mihimili ya timu, Carlinhos yeye amecheza jumla ya michezo tisa (9) tu katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, akifunga mabao matatu na kupiga pasi tatu za mabao.

Hizi zinaweza kuonekana ni takwimu bora kwa mchezaji huyo kwa vile ameicheza mechi chache lakini kiuhalisia hazitoshi kumfanya aonekane amefanya kitu kikubwa ndani ya timu hiyo kwa sababu amekosa idadi kubwa ya mechi ambazo uwepo wake pengine ungekuwa na msaada kwa Yanga katika harakati za ubingwa.

Changamoto kubwa kwa Yanga msimu huu imekuwa ni uchache wa nafasi za mabao ambazo imekuwa ikitengeneza lakini pia ubutu katika safu yake ya ushambuliaji kwenye kufumania nyavu.

Kutokana na uwezo wa Carlinhos kulikuwa na uwezekano mkubwa kwa Yanga kufanya vyema kwenye mechi nyingi ambazo alizikosa kama nyota huyo angecheza kwani ingekuwa na uhakika wa kutengeneza nafasi nyingi za mabao au kufunga jambo ambalo walikuwa wanalikosa.

Mechi tisa alizoichezea Yanga hadi sasa ukizigawa kwa miezi tisa ambayo Ligi Kuu imechezwa tangu Septemba mwaka jana, kwa wastani inamaanisha kuwa Carlinhos amekuwa akiichezea Yanga, mechi moja tu kwa kila mwezi.

Hii maana yake ni kwamba Yanga ilikuwa inatumia zaidi ya Sh 5 milioni kila mwezi kumgharamia Carlinhos ili acheze mechi moja tu jambo ambalo linaipa hasara kubwa timu. Unapokuwa na mchezaji anayekupa hasara kubwa kiasi hicho kama Carlinhos, suluhisho kubwa na la kwanza ni kuachana naye na sio kuacha aendelee kuvuna fedha asiyoitolea jasho.

Join our Newsletter