Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 06 25Article 544204

Maoni of Friday, 25 June 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

UCHAMBUZI: Naifikiria Yanga ya hapa GSM, kule Manji, chini Mashauri

UCHAMBUZI: Naifikiria Yanga ya hapa GSM, kule Manji, chini Mashauri UCHAMBUZI: Naifikiria Yanga ya hapa GSM, kule Manji, chini Mashauri

YANGA wanakutana katika Mkutano Mkuu wa kwanza tangu uongozi wa Dk Mshindo Msolla uingie madarakani ambao utakuwa na akili kubwa ya kwenda kuanza safari halisi ya kubadilisha mfumo wa uendeshaji.

Wakati wanachama wakieleweshwa juu ya mabadiliko hayo yatakavyokwenda, kukaibuka habari mpya ya kurejea kwa aliyekuwa Mwenyekiti wao Mfanyabiashara Yusuf Manji na habari zikaenda mbali zaidi baada ya jamaa mwenyewe kulipia kadi yake ya uanachama.

Ikumbukwe Manji hakuwepo nchini kwa muda mrefu lakini pia hapo kabla ya kuondoka kwake alijiondoa Yanga na alipotaka kurejea mamlaka zikamzuia na kutaka viongozi wapya wachanguliwe na kuanza maisha mapya.

Manji alikuwa anafanya makubwa ndani ya Yanga wakati akiwa kiongozi wao. Yanga waliishi kama wako sehemu fulani wasiyojua shida. Hakukuwa na njaa kama ambayo walipitia hapa kati baada ya kuondoka kwake. Uwanjani nako walikuwa wanachukua mataji wanavyotaka lakini ghafla tangu aondoke maisha hayo yaliondoka.

Baada ya kuondoka Manji mkombozi akaja kuwa Ghalib Said Mohamed ‘GSM’ ambaye naye akaamua kuivalisha nguo Yanga kwa kuihudumia kwa kiasi kikuba kiasi cha kurejea na taswira ya ushindani wa kuanza hata kuwa Yanga iliyozoeleka miaka ya nyuma kabla ya kuyumba.

Kama Wanayanga hawataishukuru GSM hawataweza kupata baraka ya kupata kingi zaidi kwani kwa muda wa miaka miwili tu hata tabasamu na hata mashabiki kutamani kingi ilirejea baada ya nguvu ya fedha za Ghalib.

Umuhimu wa Yanga kumshukuru Ghalib lazima uwe katika hatua yake ya kusimamia mchakato wa mabadiliko ambao watakwenda kuujadili Jumapili kwa jinsi alivyojitolea kuweka fedha zake hadi hali ilipofikia sasa.

Nimeona jinsi mchakato huu unavyoendeshwa, sina shaka kwamba Wanayanga wameshirikishwa vyema kuanzia hatua ya mwanzo hadi sasa kwa kila kundi lakini kilichonivutia zaidi ni jinsi mgawanyo wa hisa utakavyokuwa na hasa klabu kuzidi kubaki katika miliki ya wanachama.

Watu waliosimamia mchakato huu kuanzia uongozi wa Yanga, sekretarieti yao na hata mshauri wao Senzo Mazingisa wanapaswa kupongezwa kwa jinsi walivyosimamia sio tu kuona klabu inabaki katika miliki ya wenye klabu lakini pia kuendana na matakwa ya serikali ambayo imekuwa ikitaka kuona asili ya hizi klabu kongwe haibadiliki sana katika umiliki.

Sasa Wanayanga wanajadili jina la Manji kurejea. Haiwezi kuwa hatua mbaya kutokana na mchakato wao unaruhusu wawekezaji zaidi ya wawili na wasizidi wanne katika muundo wao na hapa ndipo naona kuna uwezekano mkubwa wa Yanga kurejea na nguvu.

Itakumbukwa kabla ya kuingia kwa uongozi wa Dk Msolla, Yanga ilipitia katika kuwa chini ya kamati maalum ya kusimamia klabu chini ya mwenyekiti Lucas Mashauri ambaye ni mtu mwenye nguvu ndani ya Yanga.

Mashauri hakuwa na kiu ya madaraka zaidi ya kutaka kuona Yanga inasimama imara na hatimaye ikapita katika wakati ule mgumu na baadaye kupatikana uongozi kamili wa Dk Msola lakini sasa haitakua kazi endapo Manji, Ghalib na Mashauri na wengine wataunganisha nguvu na akili zao katika kuijenga klabu yao na hatimaye ikasimama.

Yanga inahitaji akili kubwa za watu kama hawa watatu ambao huwezi kuja kusema kuna kitu wanakitaka katika kuchukua ndani ya Yanga bali ni mapenzi yao ndio yanawafanya kukubali majukumu hayo na hata kutumia fedha zao kuisaidia klabu wanayoipenda.

Mpira wa sasa unahitaji fedha kitu ambacho Yanga kiliwayumbisha, lakini pia Yanga ilikosa aina ya viongozi wenye maono ya mbali ambao wanaweza kuyasimamia na kuyatekeleza kwa weledi wakati huo timu ikiendelea kufanya vyema uwanjani.

Viongozi hawa watatu wameisimamia Yanga kwa nyakati tofauti ngumu na kisha kuonekana kuwa na sura ambayo inaweza kuwafariji wanachama na sasa ndio wakati wa wanachama na mashabiki wa Yanga kuwa na akili ndefu katika mkutano mkuu wao ujao.

Waachane na makelele ya kufuata mkumbo wa wasioitakia mema klabu na badala yake wakatulize akili ya jinsi gani watawaunganisha viongozi wao hao ili klabu yao ipige hatua na sio kuwa na akili ya kugawanya nguvu yao.

Yanga wanapaswa kujifunza kupitia maisha magumu waliyopitia lakini bado wakapata nafasi nyingine ya kutulia na kurejea katika maisha mazuri. Nafasi hii iwape umakini katika uamuzi wao kuanzia katika mkutano mkuu wao ujao.

Acha tukaone.