Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2022 01 01Article 582472

Maoni of Saturday, 1 January 2022

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

UCHAMBUZI: Simba ilijitega yenyewe bila kujua, ila viporo lazima viliwe

Wekundu wa Msimbazi, Simba SC Wekundu wa Msimbazi, Simba SC

Inachekesha sana sana. Simba ilisafiri umbali wa Kilomita 1,008 kuifuata Kagera Sugar mjini Bukoba. Ilienda huko kwa ajili ya mechi ya Ligi Kuu Bara. Mechi haikuchezwa kwa vile nyota 16 wa Simba waliugua ghafla mafua makali, kifua pamoja na homa. Mabosi wa Simba waliomba udhuru mechi yao iahirishwe. Kagera Sugar nayo ilikuwa na baadhi ya nyota wake wenye maradhi kama hayo akiwamo Kocha wake, Francis Baraza. Lakini wao hawakutaka mechi iahirishwe kwa kutamba jogoo hafi kwa utitiri. Walitaka mechi ipigwe hivyo hivyo. Simba ikagoma na kuiomba TPLB isikilize kilio chao. Bodi ya Ligi (TPLB) ingefanya nini mbele ya Simba. Ikatangaza mechi kuahirishwa. Itachezwa lini? Hakuna anayejua!

Hadi sasa bado haijapangiwa siku ya kuchezwa tena. Simba ikageuza zake ikarudi Dar ikiwa na nyota wake wote. Wakaa kidogo Dar kisha ikasafiri na wachezaji wale wale iliyodai walikuwa hoi kwenda Tabora kuvaana na KMC. Yaani wachezaji 16 waliugua pamoja na kupona pamoja. Inafikirisha kidogo! Ilipotua Tabora, ilishuka uwanjani na kuwavaa kwa hasira wenyeji wao KMC na kuwapasua kwa mabao 4-1. Hatukusikia tena habari za wachezaji kuugua.

Hata Yanga, siku moja baada ya udhuru wa Simba nayo ilitangaza wachezaji wake kama watano walikuwa wagonjwa, lakini hawakutaka waahirishiwe mechi yao na Tanzania Prisons. Walicheza hivyo hivyo na kushinda mabao 2-1. Mtibwa Sugar nayo iliomba udhuru kwa TPLB, saa chache baada ya Simba kusikilizwa. Nayo ilidai nyota wake wengi walikuwa wagonjwa. TPLB ikawagomea na kutoa muongozo uliokuwa kama muarobaini ya mafua makali na kifua.

Bodi ilisema kama timu inauguliwa na wachezaji wake wa kikosi cha kwanza, watalazimika kucheza mechi zao kwa kutumia kikosi cha vijana na wale watakaokuwa salama. Lengo ikiwa ni kuepuka viporo visivyo vya lazima. Mtibwa ikaona isiwe tabu ikacheza mechi yao na Polisi Tanzania na kutoka sare 1-1. Hata hivyo kukaibuka malalamiko, kuwa TPLB iliipendeleza Simba kwa kusikiliza kilio chao kwa jambo lile lile ambao Mtibwa iliomba.

Cha kuchekesha zaidi ni kwamba tangu baada ya mkwara wa TPLB kuwa timu inayouguliwa lazima icheze mechi zao kwa kutumia timu ya vijana, hakuna klabu iliyoibuka tena kudai inauguliwa na wachezaji wake.

Timu zote zinaupiga kama kawaida kulingana na ratiba ya ligi ilivyo. Yaani ugonjwa wa mafua makali, kifua sambamba na homa zimeisha ghafla! Inachekesha sana.

Ni ngumu kuamini maradhi hayo yameyeyushwa na tamko wa TPLB la kutaka timu zenye wachezaji wagonjwa kutumia U20 katika mechi zao za Ligi Kuu.

Inawezekana ni kweli upepo wa kuugua mafua makali, kifua na homa ulipita, lakini kuna timu zilitaka kutumia kama kichaka cha kulazimisha mechi za viporo vya ligi hiyo. Bahati nzuri TPLB ikashtukia.

Mtu wa mashabiki nawaza tu, namna gani, Simba ilivyojibebesgha mzigo wa gharama usio na sababu ya kutaka iwe na kiporo na Kagera Sugar tena ugenini?

Ndio. Ilienda hadi Bukoba kwa ajili ya kucheza mechi yao. Lakini ikaondoka mjini humo bila ya kuicheza. Hii ina maana itagharamika tena kuifuata Kagera kumaliza kiporo hicho.

Kuna baadhi ya wafukunyuku wanadai, eti Mnyama alichungulia na kuona anapasuka, hivyo ikajiongeza kwa kupitia mafua makali..teh..teh...teh..! Watu buana!

Sitaki kuamini tetesi hizo, lakini nafikiria tu, namna mabosi wa timu hiyo walivyojitia gharama nyingine isiyo na sababu. Ndio, timu itatakiwa kusafiri tena kwenda Bukoba kula kiporo chake.

Mbaya zaidi ni kwamba, kiporo hicho kimekuja huku timu ikikabiliwa na ratiba ngumu ya mechi za ligi ya nyumbani na zile za hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Simba ndio wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya CAF kwa sasa. Ikiwa imetinga hatua ya makundi na kupangwa Kundi D sambamba na RS Berkane ya Morocco, Asec Mimosas ya Ivory Coast na US Gendarmarie ya Niger.

Ratiba ya mechi hizo zinazoanza Februari mwakani, zipo karibu karibu mno. hivyo kuifanya Simba icheze bila kupumua. Yaani itatakiwa kucheza mechi za Ligi, Kombe la ASFC na zile za CAF kwa ufanisi ule ule ili kutimiza malengo waliyojiwekea. Kumbuka wao ndio watetezi wa Ligi Kuu na Kombe la ASFC.

Kama Simba itasonga mbele kwenye michuano hiyo ya CAF ni wazi itakuwa na ratiba ngumu zaidi. Nilichokiona kwa ile mechi ya Kagera ni kama Simba ilijibebesha mzigo wa gharama bila kujua. Kwani sasa itawachosha wachezaji wake kucheza mfululizo na kuwachosha. Kama ingeamua kukomaa kama watani wao kushuka uwanjani na kumalizana na wenyeji wao, kidogo wangekuwa wamejitua mzigo.

Watoto wa mjini wanasema mwana kulitafuta, mwana kulipata. Simba imekipata ilichokitafuta kwa Kagera. Kwani ni lazima kiporo kiliwe Bukoba.