Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 05 24Article 539404

xxxxxxxxxxx of Monday, 24 May 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

UCHAMBUZI: Tushirikiane kukomesha uhuni huu katika ligi zetu!

VURUGU katika Ligi Kuu Bara na hata Ligi Daraja la Kwanza (FDL) hasa hatua ya lala salama hazijawahi kuisha. Haziishi na wala hazitakuja kuisha kama hatutaamua.

Karibu misimu yote ya nyuma, ligi hizi zinapokuwa ukingoni huwa na vurugu nyingi na kelele ama malalamiko mengi. Malalamiko dhidi ya waamuzi. Mechi zimekuwa zikivurundwa. Wanaolalamika iwe ni wachezaji au makocha wamekuwa wahanga. Wamekuwa wakiadhibiwa kwa kauli zao za malalamiko. Wanasema ukweli kwa kukerwa na madudu yanayofanywa uwanjani katika mechi zao, lakini wanaishia kuadhibiwa. Cha ajabu waamuzi waliovurunda na kuwatia watu hasara wanaishia kusimamishwa kuchezesha mechi mbili tatu, kisha baada ya muda watarejeshwa na maisha kuendelea.

Timu zilizobaniwa kinyonge, zinakuwa zimeshapata hasara kubwa. Zimepoteza ushindi halali uwanjani. Zimepoteza pointi muhimu za michezo yao na mbaya hakuna anayejali. Viongozi na wachezaji wanaopaniki na maamuzi mabovu ya marefa wanafungiwa miezi kadhaa na kutozwa faini kubwa kubwa. Kisingizio ni kwamba wametoa kauli za kejeli na kufedhehesha, kinyume na kanuni za ligi, hata kama walichokisema ni kweli.

Fedha za faini zinaenda Bodi ya Ligi (TPLB) au Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kutunisha mifuko ya taasisi hizo, lakini hakuna badiliko lolote linalotokea la kupunguza malalamiko hayo. Malalamiko kwa wale wanaovurunda mechi kwa makusudi. Waamuzi wamekuwa wakiziumiza klabu. Tusifiche ukweli. Wapo wanaovurunda kwa bahati mbaya kwa makosa ya kibinadamu, lakini kuna wengine kwa namna wanavyofanya uamuzi, hujenga hisia wanatumika kwa manufaa ya klabu au waliowatuma nyuma yao.

Klabu zilizoumizwa na maamuzi ya ovyo wala haziambulii kitu. Huu ni uhuni uliopo kwenye soka la Tanzania. Upo katika Ligi Kuu Bara. Upo kwenye Ligi Daraja la Kwanza (FDL). Kule kwenye vita ya kupanda daraja. Timu zimekuwa zikilazimisha kupanda hata kama hazina uwezo. Zimekuwa zikiziumiza timu nyingine zenye uwezo kwa kutumia waamuzi wasio waadilifu. Hili linafichwa, lakini ukweli ndivyo ulivyo.

Amewahi kulalamika, Ammy Ninje na Mbao yake. Amewahi kupiga kelele King Kibadeni enzi akiwa Kagera Sugar. Amepiga kelele hivi karibuni, Mkurugenzi na Mwenyekiti wa Gwambina, Alexander Mnyeti. Makocha wamelalamika. Mbwana Makatta juzi kashindwa kujizuia. Amelalamika juu ya kile alichokumbana nacho katika mchezo wao dhidi ya Ihefu. Yanga wanaugulia maumivu chinichini baada ya bao lao safi la Yacouba Songne dhidi ya Namungo, kukataliwa na kuwanyima ushindi ambao pengine ungeiweka timu yao kileleni mwa msimamo wa Ligi. Mwamuzi aliyewanyima bao hilo kafungiwa mechi tatu tu. Halafu basi. Siku chache zijazo atarudi kuendelea na kazi yake na atavurunda tena. Rekodi zinaonyesha sio mara ya kwanza kufanya kosa kama lile. Sio yeye tu, waamuzi kadhaa wamekuwa wakiadhibiwa kwa kusimamishwa mechi chache, kisha baada ya muda wanarudi na kuvurunda tena kama kawaida. Maswali mengi juu yao, je wanapokuwa nje wanapigwa msasa ili warejee wakiwa makini? Kama ndio mbona wakirudi huvurunda tena? Hapa ni lazima paangaliwe. Kwani haionekani kama wahusika wanajutia makosa yao. Haionyeshi kama wasimamizi wa soka letu wanaumizwa na madudu haya. Wataumizwa au kukerwa vipi na hali hiyo, mifuko ya taasisi zao inatuna kwa fedha za faini!

Sio Yanga au Dodoma Jiji tu, wanaolia na maamuzi tata ya marefa. Klabu ni nyingi zimekuwa zikiumizwa na kulia na vurugu hizo, zinazokithiri kila ligi zinapokuwa ukingoni. Sitaki kuzungumzia sana FDL au Ligi Daraja la Pili (SDL), licha ya kwamba nazo zilikuwa na kelele nyingi za ujanja uliofanywa na baadhi ya timu dhidi ya wenzao kupitia waamuzi wasio waaminifu na waadilifu.

Mara nyingi malalamiko na kelele hizi za kihuni zimekuwa zikiachwa kwa kukosekana kwa ushahidi wa moja kwa moja, lakini wadau wa soka wanafahamu kinachofanyika. Hakijaanza leo wala jana. Kipo kwa muda mrefu. Kimekuwa kikipigiwa kelele, lakini hakuna hatua za dhati kuzikomesha. Siku za nyuma wakati nikisaka habari mtaani, kuna baadhi ya waliokuwa viongozi wa soka mkoa wa Dar es Salaam walikuwa wakijadiliana na kupanga wapandishe timu ipo katika Ligi Kuu. Yaani timu inapandishwa nje ya uwanja kabla haijashuka uwanjani. Kwanini soka letu lisidumae!

Ukisikia viongozi wanaosimamia soka letu, wakiwamo wale wa kamati ya waamuzi, na hata Bodi ya Ligi, wanapohojiwa juu ya tatizo hili la waamuzi na wanavyotoa majibu mepesi katika maswali magumu, utaelewa kwanini uhuni huu hauishi! Wanajibu simpo tu; “Tunasubiri ripoti kisha kamati itaamua...siwezi kulisemea hili kwa sasa...” Hivyo tu, halafu basi! Hapa ndipo tunapoona ugumu wa soka letu kusonga mbele.

Kwa kuwa janga hili linahusu timu shiriki za ligi husika. Linawahusu pia wadau wote. Kushirikiana kwa pamoja kulikomesha ili kulifanya soka letu lisonge mbele kwa mafanikio.

Ujanja ujanja huu katika ligi zimekuwa zikikwamisha maendeleo ya soka la Tanzania.

Ukitaka kujua hili, angalia tu timu zinazofanya juhudi kubwa kupanda daraja, zinapotaabika zikiwa kwenye ligi ilizopanda na kujikuta zikirudi zilipotoka. Sio zote, ila asilimia kubwa ya timu zinazopanda daraja, hutumia hila na mbinu chafu. Huenda wasimamizi wa soka baadhi yao wanahusika kwa sababu ya kisiasa na masilahi yao binafsi hasa kwa turufu za chaguzi za vyama na taasisi zao wanajua ila wanakausha.

Hata hivy, bado naamini, wadau wa soka watalipigia kelele hili kwa nguvu na kushirikiana wanaweza kukomesha uhuni huu. Kama ni kweli waamuzi wanashindwa kutafsiri sheria za soka, basi wapigwe msasa zaidi kabla ya kupewa tena mechi za ligi.

Imeandikwa na BADRU KIMWAGA

Join our Newsletter