Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2022 01 01Article 582466

Maoni of Saturday, 1 January 2022

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

UCHAMBUZI: Utulivu, umakini utawabeba Simba makundi Shirikisho

Simba SC Simba SC

Droo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ile ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu ilichezeshwa huko Cairo, Misri Jumanne.

Wawakilishi pekee wa Tanzania katika mashindano ya klabu Afrika waliosalia msimu huu, Simba ambao wapo katika Kombe la Shirikisho Afrika wamepangwa kundi D ambalo lina timu za RS Berkane ya Morocco, Asec Mimosas (Ivory Coast) na US Gendarmerie Nationale ya Niger.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa baada ya droo ya Jumanne, Simba itaanzia nyumbani kwa kuivaa Asec Mimosas, Februari 13 mwakani na baada ya hapo siku chache baadaye itakabiliana na Gendarmerie ugenini, mchezo uliopangwa kuchezwa siku mojawapo kati ya Februari 18 au 19.

Februari 25 au 26 Simba itacheza ugenini na RS Berkane ambayo watarudiana nayo kati ya Machi 11 au 12 kisha watasafiri kwenda Abidjan kuvaana na Asec Mimosas kati ya Machi 18 au 19.

Hatua ya makundi ya mashindano hayo itakamilishwa rasmi kati ya Aprili Mosi au 2 ambapo Simba itakuwa nyumbani kucheza na US Gendarmerie.

Baada ya ndoto zao za kutinga hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kukwama baada ya kutolewa na Jwaneng Galaxy ya Botswana katika raundi ya kwanza kwa kanuni ya bao la ugenini kufuatia sare ya mabao 3-3 ambayo timu zilitoka katika mechi mbili baina yao za hatua hiyo, bila shaka malengo ya Simba kwa sasa ni kufanya vyema Kombe la Shirikisho.

Hilo ni jambo lililo wazi ukizingatia hadhi ya Simba na mafanikio waliyoyapata msimu uliopita ambao waliishia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika licha ya wengi kuwa na imani kuwa wangefika mbali zaidi ya hapo.

Matumaini ya Wanasimba wengi na baadhi ya wadau wa soka nchini ni kwamba timu hiyo itafanya vyema kwenye michuano hiyo kwa kufika hatua ya nusu fainali na hata kwenda mbele zaidi ya hapo wakiamini wana uzoefu wa kutosha wa kuwawezesha kutimiza hilo.

Hata hivyo. kwa namna kundi D lilivyo, Simba wanapaswa kuchukua tahadhari kubwa na wanatakiwa kuhakikisha kazi ya ziada inafanyika ili waweze kupenya na kusonga mbele.

Tathmini na utafiti wa kina kwa wapinzani na mazingira ambayo Simba itakutana nayo hatua hiyo inapaswa kufanyika na baada ya hapo uongozi, benchi la ufundi na wachezaji wanapaswa kufanyia kazi kwa ufasaha yale yote watakayoyabaini ili waweze kusonga mbele.

Kazi hiyo inapaswa kufanyika kitaalam na ihusishe watu sahihi ili kuepuka kutengeneza mazingira na vikwazo ambavyo vitakwamisha malengo ya wawakilishi hao wa Tanzania.

Hawapaswi kufanya mambo kwa kukurupuka au kwa kufuata mihemko na ni vyema kutoruhusu mianya ambayo inaweza kutumiwa na wapinzani wao kuwadhuru.

Simba wanapaswa kutambua wapo kundi gumu na hawatakiwi kuidharau timu yoyote kati ya tatu walizopangwa nazo kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanajichimbia kaburi.

RS Berkane sio timu nyepesi na ina uzoefu wa kutosha wa mashindano hayo kwa sababu imeshawahi kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2019/20 na kumaliza nafasi ya pili ya taji la Caf Super Cup mwaka 2021 huku ikiishia nafasi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2018/19.

Kwa upande wa Asec Mimosas, imewahi kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1998 pia katika nyakati tofauti imewahi kufika hatua ya fainali, nusu fainali, robo fainali na makundi ya mashindano ya klabu Afrika.

US Gendarmerie ni wageni katika hatua hiyo lakini wanaonekana ni timu yenye kiu ya kufanya vyema kwenye mashindano hayo ikibebwa na historia nzuri ya kutumia vyema uwanja wa nyumbani.

Mbali na hayo, timu hizo bila shaka zinaitazama Simba kama moja ya timu tishio hivyo ni wazi zitajiandaa vilivyo kukabiliana nayo zikiamini kama zisipofanya hivyo nafasi yao ya kusonga mbele itakuwa ngumu.