Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 10 30Article 566785

Maoni of Saturday, 30 October 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

UCHAMBUZI: Viongozi Simba wajitofautishe na mashabiki

Crescentius Magori Crescentius Magori

Kuna wakati mwingine vinafanyika vitu vya ajabu sana kwenye mpira wetu mpaka sasa mashabiki tunashangaa.

Yanafanyika maamuzi ya ajabu sana ambayo wakati mwingine unajiuliza imekuwaje au huyo aliyefanya alikuwa anafikiria nini.

Sisi mashabiki tunaamini kwamba viongozi ni watu sahihi sana wakutuongoza inafika kwenye jambo lolote kubwa au dogo. Ni utaratibu wa kawaida tu.

Kwa nini nasema hivi. Mimi kama mtu wa mashabiki na mashabiki wenzangu, tumesikitishwa sana tena sana na hiki kilichotokea kwenye klabu ya Simba baada ya kufungwa na Galaxy na kuondoshwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kusema ule ukweli kitendo cha kutolewa kwenye mashindano tena kwenye Uwanja wa Mkapa kilitukera sana mashabiki. Hatukutegemea wala hatukuwahi kufikiria tungefedheheka kiasi hiki tena mbele ya timu ya kawaida kabisa.

Wamekuja Waarabu wote wa maana tumewapasua tumeenda kuangukia kwenye kale katimu cha Botswana kweli? Inauma sana.

Lakini viongozi hawakupaswa kutuvuruga kiasi kile. Baada ya kupoteza ile mechi walipaswa kutulia na kuangalia mbele Zaidi.

Kitendo cha Cresentius Magori na Mohamed Dewji kukimbilia kuposti kwenye mitandao na kuonyesha kuna hujuma au Simba kuna watu wamehusika kuhujumu ili kupoteza mchezo ule sidhani kama kilikuwa cha kiungwana.

Walikurupuka wale jamaa. Siyo uungwana kabisa, walipaswa kutulia kwanza na kutafakari na hata kama kuna sehemu kuna tatizo walitatue kwa kumuita mhusika.

Kitendo cha kuposti video vya baadhi ya matukio na kuwazungushia duara wachezaji ni kutengeneza lawama na kuwachafulia, kulipaswa kutumika njia sahihi za kuwaadhibu kama ni kweli kulikuwa na ulazima na vithibitisho hivyo. Si uungwana. Kitendo cha wale viongozi kuwahusisha wachezaji na hujuma kinawaweka kwenye presha ya kuzidi kufanya vibaya kwenye siku za usoni.

Inawaondolea kujiamini, kama kulikuwa na tatizo viongozi walipaswa kuwaita wahusika na kuzungumza nao kwa ushahidi.

Walichokifanya ni kurudisha presha kwa wachezaji jambo ambalo litachangia kuwatoa zaidi mchezoni na kuwapotezea kujiamini.

Ifike mahali viongozi wajue athari za matamko yao wanayofanya kwa watu wengine hasa kwa klabu hizi kubwa zenye mashabiki wenye mapenzi makubwa ambayo yanafikia hata hatua ya kuhatarisha maisha ya wengine.

Lazima ifike mahali kiongozi afanye kazi yake na shabiki au mwanachama afanye kazi yake na ajue miiko yake.

Nini anachopaswa kufanya na nini hapaswi kufanya kwa wakati gani. Vinginevyo soka letu litakuwa kwenye wakati mgumu sana, tutakuwa tunapiga hatua chache mbele na nyingi nyuma. Na siyo lazima kiongozi utolee tamko kila kitu. Fanya vitendo Zaidi.

Wote tunaelewa presha mliyonayo kama viongozi. Lakini siyo lazima kila wakati umsukumie mtu jumba bovu ili wewe ubaki salama.

Madhara yake ni makubwa sana kwa vile timu nzima sasa inacheza kwa presha kubwa mchezaji akikosea kidogo uwezekano wa kutoka mchezoni au kuendelea kufanya vibaya ni mkubwa.

Ni wakati wa viongozi wa Simba hata klabu zingine kujifunza kwa kosa hili. Kiongozi ni lazima ujitofautishe na mashabiki. Usifanye mambo kwa mihemko.

Utaathiri watu wengine walioko chini yako, usiangalie masilahi yako tu angalia na kesho ya klabu na mambo mengine ikiwemo maisha yajayo ya hao wachezaji haswa enzi hizi za digitali ambazo kila kitu kinabaki kwenye mitandao.