Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 09 12Article 556996

Maoni of Sunday, 12 September 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

UCHAMBUZI: Wachezaji wa kigeni wana deni kubwa Kimataifa

Mmoja ya wachezaji wa kigeni waliosajiliwa Simba, Pape Ousmane Sakho Mmoja ya wachezaji wa kigeni waliosajiliwa Simba, Pape Ousmane Sakho

Agosti 31 ilikuwa siku ya mwisho ya dirisha kubwa la usajili kwa timu za Ligi Kuu na nyinginezo hapa Tanzania Bara.

Tumeshuhudia wachezaji mbalimbali wakihama kutoka timu moja kwenda nyingine, baadhi wakipandishwa kutoka vikosi vya vijana kwenda vile vya wakubwa huku wengine wakiongezwa mikataba ya kuziendelea timu zao baada ya kuonyesha viwango bora na mchango mkubwa katika msimu uliomalizika ingawa wapo walioachwa kutokana na viwango vyao kutokuwa vya kuvutia.

Yote hiyo ni mikakati ya timu kuhakikisha zinakuwa na vikosi imara ambavyo vitaleta ushindani mkubwa katika kuwania mataji ya mashindano mbalimbali msimu ujao.

Idadi kubwa ya wachezaji ambao wamesajiliwa katika dirisha lililomalizika la usajili ni wale wazawa huku namba ndogo ikiwa ni wachezaji wa kigeni kutoka mataifa tofauti duniani ambao wamekuja kusaka malisho ya kijani katika klabu za hapa nchini.

Na kama ilivyozoeleka, ni timu zilezile tatu kubwa hapa nchini, Simba, Yanga na Azam ambazo zimeonyesha misuli ya kifedha kwa kila moja kusajili zaidi ya wachezaji 10 wa kigeni katika vikosi vyao tofauti na timu nyingine ambazo zenyewe vikosi vyao vinaundwa na idadi kubwa ya wachezaji wazawa.

Simba katika msimu ujao itakuway na wachezaji 12 wa kigeni ambao ni Enock Ibanga, Sadio Kanoute, Pape Sakho, Pascal Wawa, Duncan Nyoni, Peter Banda, Lwanga Taddeo, Bernard Morriso, Chris Mugalu, Rally Bwalya, Joash Onyango na Medie Kagere.

Kwa upande wa Yanga wao watakuwa na nyota wa kigeni 10 ingawa idadi hiyo inaweza kuongezeka siku za usoni kwani wamebakia na nafasi mbili za kusajili wachezaji wa kigeni katika dirisha dogo la usajili.

Wachezaji wa kigeni kutoka mataifa mbalimbali tofauti ambao wataitumikia Yanga msimu ujao ni Djigui Diarra, Shaban Djuma, Yannick Bangala, Mukoko Tonombe, Khalid Aucho, Ducapel Moloko,Yacouba Songne, Heriter Makambo, Saido Ntibazonkiza na Fiston Mayele.

Katika kikosi cha Azam FC, wachezaji wa kigeni watakuwa na Daniel Amoah, Mathias Kigonya, Bruce Kangwa, Nico Wadada, Never Tigere, Prince Dube, Idrissa Mbombo, Rodgers Kola, Yvan Mballa, Charles Zulu, Paul Katema na Kenneth Muguna.

Ipo sababu kubwa kwa timu hizo kuamua kusajili idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni katika vikosi vyao nayo ni ushiriki wao katika mashindano ya klabu Afrika Timu hizo tatu safari hii zimejiwekea malengo ya kumaliza katika hatua za juu za mashindano hayo ambayo yana thamani kubwa kwa ngazi ya klabu barani humu.

Simba na Yanga kila moja inatamani kufanya vizuri na kutinga hatua ya makundi au zaidi katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambako zitashiriki wakati Azam FC yenyewe inataka ifanye vyema kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Zinaamini kwamba uwepo wa idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni katika vikosi vyao utasaidia ziweze kuleta ushindani na kutamba katika mashindano hayo kutokana na uzoefu, ubora na nidhamu ambayo imekuwa ikiwawezesha kulinda na kuwa na muendelezo mzuri wa viwango vyao.

Hivyo kuelekea msimu mpya wa mashindano ya kimataifa ambao unaanza mwishoni mwa wiki hii, ni wajibu kwa wachezaji hao wa kigeni kulipa imani ambayo imejengeka kwao kwa kuhakikisha timu hizo zinafanya vizuri badala ya wao kugeuka watumishi hewa.

Wanatakiwa kutoa mchango mkubwa ndani ya uwanja ili kuonyesha na kuthibitisha kwamba timu hizo hazikufanya makosa kuwasajili jambo ambalo pia litaonyesha utofauti baina yao na wale wazawa.

Gharama kubwa ya fedha ambayo timu hizo zinatumia kuwasajili na kuwahudumia wachezaji hao wa kigeni inapaswa kurudishwa kwa mchango mkubwa na mafanikio ya uwanjani katika mashindano hayo ya kimataifa.

Wafahamu kwamba kutwaa mataji ya ndani hakupaswi kuwa utetezi kwao ikiwa watashindwa kufanya vyema kimataifa kwani hata wale wazawa wanaweza na wanamudu jukumu hilo.

Wakae wakifahamu fika kwamba heshima na ustaa wao katika timu hizo vitakuja na kuchochewa zaidi na mafanikio ambayo wao watachangia kupatikana katika mashindano ya klabu Afrika.

Vinginevyo, sifa walizopata baada ya kusajiliwa hazitokuwa na maana yoyote na wataonekana mizigo tu ndani ya timu hizo.