Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 06 09Article 541690

xxxxxxxxxxx of Wednesday, 9 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Udhibiti uvuvi haramu na ongezeko mavuno ya samaki 

CHIMBUKO la Siku ya Uvuvi Haramu Duniani ni wazo lililoibuliwa katika Kikao cha 39 cha Kamisheni ya Nchi za Mediterranean mwaka 2015.

Kikao hicho kilipendekeza kuwepo kwa siku ya kimataifa ya kudhibiti uvuvi haramu, uvuvi usiotolewa taarifa na uvuvi usioratibiwa.

Kamisheni hii ilipendekeza kutangazwa kwa siku hiyo ili kutoa uelewa wa umuhimu wa vita dhidi ya uvuvi haramu, uvuvi usiotolewa taarifa na uvuvi usioratibiwa.

Pendekezo hili iliwasilishwa na kuridhiwa katika Kikao cha 32 cha Kamati ya Masuala ya Uvuvi ya Shirika la Chakula Duniani (FAO).

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayehusika na Uvuvi, Dk Rashid Tamatamah, anasema Desemba 2017, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika maazimio yake ya mwaka kuhusu uvuvi endelevu, ilitangaza rasmi Juni 5 ya kila Mwaka kuwa Siku ya Kimataifa ya Vita dhidi ya Uvuvi Haramu, Uvuvi Usiotolewa Taarifa na Usioratibiwa.

Tamatamah anasema, Juni 5 ilichaguliwa kwa sababu wakati azimio hilo linapitishwa, kulikuwa na Itifaki ya Kuzuia Uvuvi Haramu kwa kupitia bandari.

Anasema Tanzania iliridhia itifaki hiyo iliyolenga kudhibiti uvuvi haramu na kuongeza kuwa, siku ambayo itifaki hiyo ilipitishwa ilikuwa Juni 5, hivyo UN iliona vyema tarehe hiyo iendelee kwa kuwa inahusu uvuvi haramu.

Anasema kwa kuwa Tanzana imeridhia itifaki hiyo na kuunga mkono Azimio la Umoja wa Mataifa dhidi ya Uvuvi Haramu, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imedhibiti uvuvi haramu kwa asilimia 80 katika maji baridi yakiwemo maziwa, mito na mabwawa.

Kadhalika, imedhibiti uvuvi haramu kwa asilimia 100 katika maji chumvi hususan Bahari ya Hindi ambako aina kubwa ya uvuvi haramu iliyokuwa ikitumika ni wa kutumia milipuko ya baruti.

“Uvuvi haramu ni dhana pana ambayo pamoja na kuhusisha matumizi ya nyavu zisizoruhusiwa, pia inahusisha kitendo cha mtu kuvua bila kuwa na leseni, kutumia chombo cha uvuvi ambacho hakijasajiliwa na utoroshaji wa samaki kwenda nje ya nchi,” anasema Dk Tamatamah.

Pamoja na serikali kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti uvuvi haramu, anasema changamoto za matumizi ya makokoro, watu kuvua bila leseni na utoroshaji wa samaki kwenda nje ya nchi bado zipo japo kwa kiasi kidogo.

“Kabla ya mwaka 2017, hali ilikuwa mbaya sana, lakini mwaka 2018 idara kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, waliendesha operesheni mwaka mzima ikiwemo Operesheni Sangara katika Ziwa Victoria na Operesheni Jodari katika Bahari ya Hindi zilizofanikiwa kuondoa nyavu haramu,” anasema na kuongeza: “Katika bahari tulikamata meli moja ya uvuvi Mtwara ya kutoka Vietnam na wahusika walifungwa.”

Anasema tangu mwaka jana, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilianzisha Mkakati Shirikishi wa Usimamizi na Udhibiti wa Rasilimali za Uvuvi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuimarisha ulinzi shirikishi.

“Baada ya kukamilika kwa zile operesheni, idadi ya samaki kwenye maziwa, bahari na mito imeongezeka kwa kiasi kikubwa.”

“Miaka ya nyuma kabla ya operesheni ile, mavuno ya samaki Tanzania kutoka vyanzo vyote vya maji yalikuwa tani 350,000 hadi 360,000, lakini kwa mara ya kwanza mwaka 2019 zilifika tani 382,000 na mwaka jana tulifikia tani 497,000,” anasema Dk Tamatamah.

Kuhusu idadi ya wavuvi waliopo nchini, anasema Tanzania ina wavuvi wanaotambulika 253,000 na wafugaji samaki 30,000.

Anabainisha kuwa, kesi zilizopo mahakamani kuhusu uvuvi haramu hazizidi 10 kwa kuwa wengi hulipa faini.

MBUNGE WA CHONGA

Mbunge wa Chonga Salum Mohammed Shaafi (ACT-Wazalendo), anasema kuchoma nyavu za wavuvi si suluhisho kwa uvuvi haramu, bali serikali inapaswa kuwapatia mikopo wavuvi ili wanunue zana za kisasa za uvuvi zikiwemo boti za uvuvi, na pia iendelee kutoa elimu kuhusu athari za uvuvi haramu.

“Uvuvi umetoa ajira kwa Watanzania, hivyo ni jukumu la serikali hasa ni kutoa elimu ili wananchi waondokane na uvuvi haramu unaoharibu mazalia ya samaki, unaoharibu utalii kwa kuwa bahari na maziwa ni sehemu ya vivutio vya utalii,”anasema Shaafi.

KUHUSU MIKOPO

Anasema mwaka 2018 lilianzishwa dawati la sekta binafsi ili wavuvi waweze kukopesheka na kabla ya 2018 kulikuwa hakuna mtu yeyote au kikundi chochote kilichopata mkopo benki, lakini mpaka Aprili mwaka huu, kuna vikundi ambavyo vimepata mkopo kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB).

“Kwa mfano, Ukerewe kuna akina mama wanaofanya kazi ya kuanika dagaa ambao ni tatizo kuanikwa wakati wa masika, tukawaunganisha na kusaidia kuwaandikia pendekezo na kulipeleka Benki ya TADB na walipata mkopo wa Sh milioni 200 walizotumia kununua mashine kwa ajili ya kukaushia samaki, kikundi kingine kinaitwa Iragula kilichopo Sengerema ambao walinunua boti za kuvulia na nyavu,”anasema Dk Tamatamah.

WAZIRI MIFUGO NA UVUVI

Wakati anawasilisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya fedha kwa Wizara yake kwa mwaka 2021/2022 bungeni hivi karibuni, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, alisema katika mwaka 2020/2021, Sekta ya Uvuvi nchini ilikua kwa asilimia 6.7.

Pia mchango wa sekta hii kwa pato la taifa ulikuwa asilimia 1.71 na kutoa ajira za moja kwa moja kwa wavuvi 195,435, wakuzaji viumbe maji 30,064 na Watanzania milioni 4.5 wameendelea kupata mahitaji yao ya kila siku kutokana na shughuli mbalimbali zinazohusiana na sekta ya uvuvi.

Ndaki anasema shughuli za wavuvi wadogo huchangia asilimia 95 ya samaki wote wanaovuliwa nchini na asilimia tano iliyobaki huchangiwa na wavuvi wakubwa.

Anasema hadi Aprili mwaka huu, wavuvi wadogo 195,435 walishiriki moja kwa moja shughuli za uvuvi kwa kutumia vyombo vya uvuvi 58,231 na kuvuna tani 422,859.8 za samaki zenye thamani ya Sh trilioni 2.62.

“Kulingana na taarifa za utafiti katika Ziwa Victoria mwaka 2020, kiasi cha samaki katika ziwa hilo kimeongezeka kutoka tani milioni 2.7 mwaka 2019 hadi tani milioni 3.5 kwa ziwa zima ongezeko ambalo ni sawa na asilimia 29.3. Ongezeko hili limechangia kiasi cha samaki kilichopo katika maji yote kufikia tani milioni 4.1,” anasema Ndaki.

Join our Newsletter