Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 11 11Article 570100

Maoni of Thursday, 11 November 2021

Columnist: mwananchidigital

Uhai wa Maalim Seif baada ya kifo chake

Uhai wa Maalim Seif baada ya kifo chake Uhai wa Maalim Seif baada ya kifo chake

Nini hatima ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) na mustakabali wa siasa za Zanzibar baada ya kifo cha Maalim Seif Sharif Hamad?

Hili ndilo swali linalogonga vichwani mwa viongozi, wafuasi na wafuatiliaji wa masuala ya siasa visiwani Zanzibar, wanajiuliza tangu Maalim Seif aliyefariki dunia Februari 17, mwaka huu, kiongozi huyu anatajwa kuwa mhimili muhimu wa kutuliza hali ya kisiasa na kufanikisha kuundwa kwa SUK baada ya kufikia maridhiano na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Aman Abeid Karume.

Novemba 5, 2021 Rais Samia Suluhu Hassan alizindua taasisi ya Maalim Seif ambayo inalenga kuenzi mchango wa mwanasiasa huyo kwa kuandaa shughuli mbalimbali, ikiwemo makongamano ya wadau mbalimbali.

Maalim Seif aliwania urais mara sita (1995-2020) na wakati huo wote alidai alishinda lakini hakutangazwa mshindi, hali iliyosababisha kukua kwa uhasama na chuki za kisiasa baina ya wafuasi wake na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mivutano hiyo ilifikia wakati watu hawakuwa wakishirikiana katika misiba, harusi, elimu na shughuli mbalimbali za kijamii, lakini baada ya maridhiano hali imetulia na watu wanashirikiana.

Hata hivyo, pamoja na misukosuko ya kisiasa aliyoipata Maalim Seif, ikiwamo kufukuzwa ndani ya CCM na kufunguliwa kesi ya uhaini, bado anatajwa kuwa jabali la siasa za maridhiano, umoja, mshikamano ambaye kwake masilahi ya taifa yalikuwa kipaumbele namba moja kuliko kitu kingine chochote.

Licha ya kifo cha Maalim Seif, bado anaishi kwa kuwa harakati na matendo aliyoyafanya yamekuwa dira katika siasa za Zanzibar ambazo zimekuwa na mivutano ya kiitikadi kati ya Wapemba na Waunguja.

Rais Samia Suluhu Hassan siku chache zilizopita wakati akizindua Taasisi ya Maalim Seif na kongamano lililobeba kaulimbiu ya ‘Maalim Seif, Umoja na maridhiano katika ujenzi wa Zanzibar na Tanzania Mpya’ aliwataka Watanzania waige na wamuenzi Maalim Seif kwa kudumisha umoja, maridhiano na mshikamano ambavyo alivisimamia katika uhai wake.

Anasema Maalim Seif aliangalia masilahi mapana kwa taifa, pale ambapo tofauti za wafuasi na wanasiasa zilivuka mpaka lakini mwanasiasa huyo alionyesha utayari wa kuzungumza na upande mwingine ili kutafuta maridhiano.

“Katika uhai wake, Maalim Seif alikuwa makutano ya watu, alikuwa mwalimu wa watu siyo wanafunzi tu darasani...watu wa aina ya Maalim Seif ni nadra kutokea katika maisha, vizazi na jamii inatutaka tuhifadhi kumbukumbu zao ili ziendelee kufaa vizazi vya sasa na vijavyo.

Jambo linalompambanua Maalim Seif ni uthabiti wa misimamo yake na utayari wake wa kutafuta maridhiano pale inapotokea kusigana na kutofautiana katika jambo analoliamini, aliifanya kazi hiyo kati ya chama chake na chama kingine na hata ndani ya chama chake, hii si sifa ya kawaida kwa wanasiasa na viongozi wengi duniani ambao mara nyingi walitofautiana na kinachofuata ni vurugu ambazo haziishi, taswira hii hujitokeza hapa kwetu, lakini akiwepo mtu kama Maalim Seif, vurugu hukatika na maridhiano yakaendelea.

“Tulimheshimu kwa sababu alituheshimu, alitupinga kwa hoja si kwa matusi kama wafanyavyo wafuasi ambao wanasababisha mvurugano wa umoja wetu.

“Hata pale alipotupinga hakuacha kutafuta fursa ya kuzungumzia tofauti zetu, hata pale ambapo mazungumzo hayakuzaa matunda hakukata tamaa, alitafuta fursa nyingine lakini pia hakukubali kinyongo kimtawale, aliangalia masilahi mapana ya taifa,” anasema.

Viongozi mbalimbali waliohudhuria uzinduzi na kongamano hilo walielezea namna Maalim Seif alivyokuwa kinara wa kuweka mbele masilahi ya Zanzibar na hata pale alipotofautiana zaidi na wenzake alisaka mwafaka bila kujali maumivu anayoyapata.

Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume anasema Maalim Seif alikuwa mtu mwenye msimamo thabiti tangu akiwa ndani ya CCM, pia alikuwa muungwana, asiyekata tamaa, mvumilivu mwenye kuipenda Zanzibar, ndiyo maana alikubali kushiriki kwenye mazungumzo ya kusaka maridhiano.

Anasema licha ya baadhi ya watu kumtusi, kumdhihaki na kumtuhumu kwa kutaka kuvunja muungano, lakini mchango wa Maalim Seif ni mkubwa na unapaswa kuenziwa kwa vitendo.

“Mimi najua kuna watu hawakuwa wanampenda Maalim Seif kwa sababu ya misimamo yake na tofauti za itikadi, tujifunze kuvumiliana na kusikiliza mawazo kinzani kwa kuwa tunapata mafunzo mbalimbali, tuache ukiritimba na rafu za kisiasa

“Kuna hofu kuwa wakishinda wapinzani eti muungano utavunjika, wengine hawataki upinzani uwepo. Hawa wapinzani ni raia wa wapi? Hawapendi usawa na haki kama unavyopenda wewe? Mimi napenda uwepo wao kwa kuwa tutashindana kwa hoja na kama za mwenzako ni imara zaidi unapata kujifunza na kama zako ni imara zaidi naye anapata cha kujifunza na mwishowe nchi inasonga mbele zaidi,” anasema.

Rais huyo mstaafu anasema maridhiano baina yake na Maalim Seif waliyofikia tangu mwaka 2009 na kushuhudia uchaguzi murua uliofanyika mwaka 2010 hakutegemea kama Zanzibar ingepata misukosuko ya kuitikisa SUK kama ilivyotokea mwaka 2015 na 2020. “Niliamini matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2015 hayakupaswa kufutwa hivi hivi na uchaguzi ukarudiwa bila ya pande mbili kufikia mwafaka, lakini kwa kuwa limeshatokea na Maalim Seif alichangia kutuliza upepo, ni vema tukamuenzi kwa kuheshimu maridhiano, Katiba na taratibu tulizojiwekea,” anasema.

“Maalim Seif nakumbuka kuna wakati aliniomba msamaha kwa kunitukana na kunisingizia mambo mengi na alidiriki kuniambia mengine walikuwa wakiambiwa na wana CCM wenzangu alionitajia, ukweli Maalim alikuwa muungwana sana, tumuenzi vizuri,” anasema.

Karume anasema jambo kubwa alilojifunza ambalo pia anataka viongozi wa Afrika waliige na kulienzi kutoka kwa Maalim Seif ni kujenga tabia ya kuheshimiana na kuthaminiana na kutafuta maridhiano wanapokwazana badala ya kujenga uhasama kila baada ya uchaguzi. Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amesema Maalim Seif alikuwa kiongozi asiyependa kuona mambo yakienda tofauti na hakukata tamaa, licha ya kupitia vipindi vigumu.

“Mtu anaweza kuwa kiongozi wa kisiasa lakini akawa haaminiki kwa wanachama na wafuasi wake. Ila kinachompa heshima ni wadhifa wake alionao ukiondolewa anakuwa hana maana tena, Maalim Seif alikuwa tofauti. Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia anasema funzo kubwa alilopata kutoka kwa Maalim Seif ni nidhamu ya uongozi na kuweka mbele masilahi ya taifa.

Jaji mstaafu Joseph Warioba anasema urithi mkubwa aliouacha Maalim Seif ni viongozi kujenga utaratibu wa kuzungumza kila yanapotokea matatizo. “Maalim alikuwa mvumilivu, ameacha pengo kubwa sana, lazima tupate viongozi watakaotatua matatizo ya uongozi kwa njia ya mazungumzo, chaguzi zinapofanyika ni lazima kuwepo na watu wa kuliunganisha taifa. Mhadhiri na mwanasheria nguli hapa nchini, Profesa Issa Shivji amesema Maalim Seif ni kioo kwa wanasiasa wasio na msimamo ambao kila kukicha hutoa kauli tofauti kwa lengo la kutetea msimamo wa chama au kundi fulani la watu. Anasema Maalim Seif hakuwa kiongozi aliyekubali maagizo asiyoyaamini na yaliyo kinyume na masilahi ya taifa, ndiyo maana hivi sasa anapata heshima kubwa ndani na nje ya nchi, pia alikuwa bingwa wa kusamehe na kujali masilahi ya taifa. Hata hivyo, amesema kosa Maalim Seif alilolifanya ni kutoandaa mapema mrithi wake, hivyo kila wakati yeye ndiye aliyeonekana anafaa zaidi kuliko wanachama na wafuasi wake.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar) Salum Mwalimu amemfananisha Maalim Seif na hayati Nelson Mandela ambaye licha ya kusukumwa jela kwa miaka 27, alipoingia Ikulu aliwasamehe waliomfunga na kufanya nao maridhiano.

“Wanasiasa tunapaswa kujifunza kutoka kwa Maalim Seif, ana mchango mkubwa sana katika utulivu tulionao hivi sasa visiwani Zanzibar, niwe mkweli yeye ndiye mwanasiasa niliyemhusudu na kunivutia kuingia katika siasa,” anasema.

Naye aliyekuwa Waziri wa SMZ, Mansour Himid Mansour amesema Zanzibar itaendelea kuwa salama kwa kuwa Maalim Seif amewarithisha uvumilivu, busara, hekima na kujali masilahi ya Zanzibar na Taifa.

Katibu wa Taasisi ya Maalim, Seif Jussa Ismail Ladhu, amesema wataendelea kuenzi na kutunza kumbukumbu nzuri alizowaachia ili zitumike kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

“Maalim Seif alitupika vizuri katika kutambua thamani ya utu, usawa na haki, nasi tumedhamiria kuweka vizuri urithi wa maarifa aliyoyaacha Maalim Seif ili taifa letu liendelee kuwa imara, tutasimamia umoja, maridhiano, hivyo hakuna sababu ya watu kuhofia kuwa Maalim Seif kaondoka na alivyovisimamia navyo vitaondoka,” anasema.

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema wataendelea kulinda, kudumisha mambo aliyoyafanya Maalim Seif Hamad kwa kuwa mchango wake katika siasa za Tanzania ni mkubwa na hautafutika, hivyo kila Mtanzania ana wajibu wa kuweka mbele masilahi ya taifa na pale yanapotokea matatizo ni vema wakakaa chini na kuzungumza.

“Maalim alikuwa kinara wa siasa za utaifa, alikuwa tayari kugombana na yeyote anayejali masilahi ya chama au kundi fulani la watu, utajiri wake wa mawazo na busara tutaendelea kuukumbuka na kuuenzi, ACT-Wazalendo tunawahakikishia Watanzania kudumisha umoja, mshikamano na utulivu,” anasema.

Mwenyekiti wa ADC, Hamad Rashid Mohamed amesema miongoni mwa mambo ya kijasiri aliyofanya Maalim Seif ni kwenda kufanya mazungumzo na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Aman Abeid Karume mwaka 2009 na baadaye kutangaza kuutambua uongozi wake ambao mwaka 2005 CUF walitangaza kutoutambua baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huo.

“Uamuzi wake aliufanya bila ya kushirikisha chama, ulileta mtikisiko mkubwa ndani na nje ya chama, alionekana amenunuliwa na alikubali shutuma zote lakini alibaki na msimamo wake kuwa hilo lilikuwa jambo sahihi la kutafuta maridhiano yatakayoituliza Zanzibar na watu wanashirikiana,” anasema.