Uko hapa: NyumbaniWallMaoniArticles2020 05 20Article 501991

Maoni of Wednesday, 20 May 2020

Columnist: TanzaniaWeb

Uhuru, Ruto wajiangalie wasiirejeshe Kenya ya 2007

NI wanasiasa wawili waliokulia ndani ya kilichokuwa chama tawala nchini Kenya almaarufu Kenya African National Union (Kanu), wakiwa washirika wa karibu wa aliyekuwa rais wa pili, hayati Daniel arap Moi.

Rais Uhuru Kenyatta na Makamu William Ruto, wamekuwa na historia hiyo, ingawa wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2007, wawili hao walitengana kisiasa, wakajikuta kwenye kashfa na hatimaye tuhuma za kuchochea machafuko na mauaji ya wakati wa vurugu za baada ya uchaguzi huo.

Uhuru alikuwa upande wa Rais wa zamani Mwai Kibaki wakati Ruto alikuwa mshirika muhimu n wa karibu wa kinara wa upinzani nchini humo, Raila Odinga.

Hata hivyo, matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2007 yaliyompa ushindi wenye utata Kibaki wa PNU (kambi ya Uhuru) dhidi ya Odinga wa ODM (kambi ya Ruto) uliibua machafuko yaliyosababisha Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) iliyopo Hague nchini Uholanzi, kuwaona wawili hao kuwa na mashitaka ya kujibu dhidi ya mauaji, uharibifu wa mali na kuwasababishia maelfu ya Wakenya kuyakimbia makazi yao na kuwa wakimbizi wa ndani.

Uhuru na Ruto walikuwa miongoni mwa washukiwa sita wa awali waliotajwa na Mwendesha Mashitaka wa ICC kw wakati huo, Louis Moreno Ocampo na hivyo kuwafanya wakijulikana zaidi kama ‘Ocampo Six’.

Hatua kwa hatua, washitakiwa hao walianza kupunguzwa hadi kubakia watatu wakiwamo Uhuru, Ruto na mwanahabari, Joshua arap Sang.

Uhuru alikuwa anakabiliwa na mashitaka matano, yakiwamo mauaji, ubakaji na kuwafukuza watu kwenye makazi yao kwa madai ya kupanga ghasia za baada ya uchaguzi wa Kenya mnamo mwaka 2007 hadi 2008, ambapo zaidi ya watu 1,200 waliuawa na wengine 600,000 kukosa makazi.

Kundi lililodaiwa kulengwa zaidi ni waliokuwa wakipinga ushindi wa Kibaki, hasa wa kutoka jamii ya Wakalenjing anapotokea Ruto na Wajaluo maeneo anapotokea Odinga.

Pia Ruto alikabiliwa na tuhuma za uhalifu dhidi ya ubinadamu, lakini akielekezwa zaidi dhidi ya watu jamii ya Wakikuyu anapotokea Uhuru.

Katikati ya kadhia hiyo, iliundwa tume ya usuluhishi iliyoongozwa na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Koffi Annan (marehemu) ambayo hata hivyo, Ruto aliyekuwa katika ujumbe wa ODM ya Odinga na Martha Karua wa PNU ya Kibaki waliondolewa kutokana na misimamo yao mikali.

Hata ilipoundwa serikali ya umoja wa kitaifa yakiwa ni matokeo ya usuluhishi, Odinga alitakiwa kuwa Waziri Mkuu na pande zote mbili zilipaswa kumtoa Naibu Waziri Mkuu.

Ruto alitarajiwa kuchukua nafasi hiyo kutokea ODM, hasa kutokana na ushiriki wake mpana katika uchaguzi Mkuu huo, kama ilivyokuwa kwa Uhuru wa PNU ya Kibaki.

Kibaki alimpeleka Uhuru katika wadhifa huo, lakini katika jambo ambalo halikutarajiwa, ODM ya Odinga walimteuwa aliyekuwa Mbunge wa Sabatia, Musalia Mudavadi.

Hatua hiyo inatajwa kumkera Ruto na wafuasi wake kwa madai kuwa mwanasiasa huyo ‘anayejua kuzichanga karata za siasa za Kenya’ alifanikisha kuwaingiza wabunge wengi na kura nyingi za urais kwa Odinga ikilinganishwa na Mudavadi.

Hata Uhuru na Ruto walipofikishwa ICC dhidi ya machafuko ya kisiasa, Odinga akiwa Waziri Mkuu aliweka wazi msimamo wake wa kupinga waliokuwa wanakosoa hatua ya mahakama hiyo, huku wakitaka Kenya ijitoe kwenye uanachama wake.

Upande wa Kibaki akiwa Rais na kwa kumtumia zaidi aliyekuwa Makamu wake, Kalonzo Musyoka, walitafuta kuungwa mkono ili wawili hao wasishitakiwe na Kenya ijitoe ICC. Haikuwezekana.

Kuanzia mwishoni mwa 2011, wanasiasa hao wakaongeza kasi ya ushirikiano wao na karibu kila mwisho wa wiki, walifanya mikutano tofauti wakisisitiza kuwa hawana hatia.

Miongoni mwa mikutano iliyowaleta pamoja ni ule uliofanyika mwaka 2012 katika jimbo la Ikolomani, magharibi mwa Kenya , Ruto alisisitiza nia yao kuwania urais katika uchaguzi wa 2013, na kwamba mgombea mmoja kati yake na Uhuru ndiye angeungwa mkono dhidi ya Odinga, akimwita ‘Bwana Vitendawili’.

Akiwa Ikolomani, Ruto alisema ana uhakika kati yake na Uhuru, mmoja wao angeshinda urais, na kusisitiza kuwa kwa namna yoyote, mrithi wa Kibaki asingekuwa Odinga anayejulikana pia kwa majina ya Agwambo, Tinga ama Baba.Ndivyo ilivyokuwa Uhuru alishinda dhidi ya Odinga.

Sasa wakati taifa hilo likielekea kwenye uchaguzi mkuu, linashuhudia wanasiasa hao waliounganishwa kwa ‘chuki za kisiasa’ wamefarakana, huku Uhuru akionyesha kufungamana na Odinga.

Tangu waliposhikana mkono kwa tukio lililo maarufu kama ‘hand shake’ na kushindwa kwa kambi ya Ruto katika kura ya mabadiliko ya katiba yaliyolenga kupunguza ukubwa wa serikali, Uhuru na Odinga wamekuwa ‘wakitembea njia moja’ katika hoja na shughuli nyingi za kisiasa na maendeleo nchini humo, Ruto akiachwa.

Lakini kama ilivyo kawaida kwa siasa za Kenya, taarifa za hivi karibuni zimevuja zikimhusisha Uhuru ‘kubadili gia angani’, akitaka kutoka kwa Odinga kuelekea kwa Gideon Moi, mtoto wa hayati Daniel arap Moi ili awe mrithi wake.

Kwa siasa za Kenya, suala hilo linawezekana kutokana na sababu kadhaa; mosi, Gideon anatoka kwenye chama cha Kanu kilichoasisiwa na baba mzazi wa Uhuru, hayati Jomo Kenyatta aliyekuwa Rais wa kwanza wa Kenya. Hivyo, utawala wa Kenya ukirejea kwenye chama hicho, inatafsiriwa kuwa sehemu ya kumuenzi baba yake.

Pili, Gideon anatoka kwenye jamii ya Wakalenjing walio wengi miongoni mwa wapiga kura wa Kenya. Kwa mujibu wa Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi ya Kenua (IEBC), ukanda wa bonde la Ufa wanapopatikana watu wengi wa jamii ya Wakalenjing ni maeneo yenye wapiga kura wengi nchini humo, kama ilivyo kwa ukanda wa kati na maeneo ya Mlima Kenya wenye Wakikuyu wengi.

Ukanda wa Nyanza anapotokea Odinga una wapiga kura wasiofikia wingi wa wale wa bonde la Ufa ama ukanda wa Kati na mlima Kenya.

Ingawa hali iko hivyo, ni wazi kwamba jitihada za kuwatoa Wakenya katika maslahi ya kisiasa na kiutawala yanayojikita kwenye ukabila na ukanda zikifanikiwa, takwimu hizo zitakosa maana katika kubashiri matokeo ya uchaguzi mkuu ujao.

Sababu nyingine ni baba mzazi wa Gideon Moi, alisimama kidete kuhakikisha kwamba aliyestahili kuiongoza Kenya baada ya kustaafu kwake ni Uhuru na akawania urais, ingawa alishindwa na Kibaki.

Vyovyote iwavyo, uhusiano wa Uhuru na Ruto kwa sasa hautoi hisia za wawili hao kuwa pamoja, ingawa katika siasa za Kenya, lolote linaweza kutokea kwa wakati wowote.

Lakini iwapo Uhuru na Ruto hawatakuwa pamoja katika uchaguzi huo, nini itakuwa hatima ya wafuasi na watu wa jamii zao hasa kambi ya Ruto na Wakalenjing, walioamini kwamba baada ya Ruto kumuunga mkono Uhuru mara mbili, angestahili kuwania urais, lakini inaonekana sasa hawaivi?

Vitendo kadhaa vya Uhuru vimeonyesha kuzidi kujitenga zaidi na Ruto, likiwemo tukio la hivi karibuni la kubadili viongozi wa chama tawala cha Jubilee, huku wanaoaminika kuwa kwenye kambi ya Ruto ‘wakipigwa chini.’

Je, mfumo huo wa ‘kuwashughulikia’ walio karibu na Ruto unaweza kuwa wa manufaa kwa Uhuru dhidi ya Ruto, mwanasiasa mwenye uzoefu na aliyepitia mikikimikiki mingi ya kisiasa, akiishinda?

Pamoja na hisia nyingi zinazoelezwa kwa hali ya kisiasa ilivyo nchini Kenya, wawili hawa wanapaswa kutambua walipotoka hasa uchaguzi mkuu wa 2007, wasiingize Kenya kwenye kadhia nyingine ya kisiasa kama ile ya baada ya uchaguzi huo.

Wanasiasa hao wanaweza kutofautiana kwa namna yoyote katika kutafuta mamlaka ya utawala nchini humo, lakini hawapaswi kuwa sababu ya kuwagawa Wakenya waliorejea katika umoja.

Join our Newsletter