Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 11 20Article 572974

Maoni of Saturday, 20 November 2021

Columnist: www.habarileo.co.tz

Ukatili jinsia unavyoua soka la wanawake Tanzania

Ukatili jinsia unavyoua soka la wanawake Tanzania Ukatili jinsia unavyoua soka la wanawake Tanzania

IMEELEZWA asilimia 44 ya wachezaji wanawake wamekumbana na ukatili wa kijinsia michezoni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Global Peace Fund.

Akizungumza wakati akiwasilisha matokeo ya utafiti huo uliofanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Lucius Mugisha alisema walihoji watu 100 na kati ya hao asilimia 44 walikiri kushuhudia au kufanyiwa ukatili wa kijinsia michezoni.

“Asilimia tisa wanajua aina za ukatili, theluthi wamesikia habari za kudharauliwa na kubezwa, asilimia 44 wameshuhudia au walifanyiwa ukatili ama na makocha, viongozi wa mpira au mashabiki na asilimia 65 hawajui utaratibu wa kufuata, endapo watakuwa wamefanyiwa ukatili,” alisema Dk Mugisha.

Alisema ili kuondoa ukatili, taasisi zinazosimamia soka ziweke mwongozo bora kwa jamii ili kuwavutia wanawake/ wasichana katika michezo na kuongeza pia wanawake wenyewe wameonekana kusababisha ukatili wao wenyewe kwa kupenda kuiga tabia za kiume kuanzia kuongea, mavazi na kutembea.

“Jamii inatakiwa kujua soka la wanawake siyo uhuni, bali ni fursa na kuhakikisha wachezaji wa kike wanaondokana na uhalisia wa kiume na katika muonekano wa wanawake,” alisema Dk Mugisha.

Akitoa maoni ya serikali Mkurugenzi msaidizi wa maendeleo ya michezo, Alex Mkenyenge alisema ili kukuza soka la wanawake inatakiwa kuondoa fikra potofu kwa jamii ili watoto wa kike washiriki kwa wingi na kwenye nafasi za uongozi michezoni.

Mkenyenge alimwakilisha Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul, alisema siku zote wanawake wakipewa fursa wanafanya vizuri na kutuletea makombe, hivyo inatakiwa kupinga ukatili wa kijinsia dhidi yao ili kuondoa fikra potofu kwa wazazi.

“Wanawake wakipewa fursa wanazitendea haki, medali ya kwanza ya kimataifa ililetwa na mwanamke, hivyo inabidi tubadilike na kuwapa fursa wanawake kushiriki kwenye mpira wa miguu, kwani ni fursa na inajenga umoja pia ni ajira,” alisema Mkenyenge.

Naye Mkurugenzi wa Global Peace Fund, Martha Nghambi, alisema amefurahi kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Shirikisho la Zanzibar (ZFF) Chama cha Soka la Wanawake (TWFA) na wadau wengine wa soka kuhakikisha wanapinga unyayasaji wa kijinsia na watahakikisha wanatokomeza kabisa ukatili huo.

“Kazi yetu ni kuhamasisha amani na sasa tumeingia kwenye michezo kuhakikisha michezo inachezwa kwa amani ndio maana tumefanya utafiti huu ambao dhima yake ni ‘Ukatili wa kijinsia michezoni haukubaliki,”.

Alisema utafiti wao uliwahoji wadau mbalimbali wa soka, timu za soka za wanawake ambazo ni Simba Queens, Yanga Princess, Ilala Queens, Amani Queens, Baobab Queens, Fountain Gate Princess, New Generation kutoka Zanzibar.

Mkurugenzi wa Habari na Masoko wa TFF, Boniface Wambura, alisema soka la wanawake limekuwa kwa kasi na katika makombe 10, ambayo TFF imepata katika kipindi cha miaka mitano, manne yameletwa na timu za wanawake.

“Kauli yetu ni mchezo wa kiungwana ndani na nje ya uwanja, tumefurahia kupata utafiti huu na sisi tutapenda TWFA ituletee mapendekezo ya utafiti huu ili tuufanyie kazi na tutakuwa bega kwa bega na wachezaji ili kutokomeza unyanyasaji wa kijinsia,” alisema Wambura.