Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 05 17Article 537991

Maoni of Monday, 17 May 2021

Columnist: www.habarileo.co.tz

Unatunza mazingara yako, au unadhani hauhusiki?

Unatunza mazingara yako,  au unadhani hauhusiki? Unatunza mazingara yako, au unadhani hauhusiki?

SUALA la ulinzi na utunzaji wa mazingira na maliasili ni wajibu wa kila mtu. Hii ina maana kuwa watu wote tuna wajibu kuhakikisha kuwa mazingira yanayotuzunguka ni safi na salama kwa maisha ya mwanadamu na viumbe hai.

Dunia ndio sayari yenye mandhari nzuri inayowezesha binadamu na mamilioni ya viumbe hai wengine kuishi.

Binadamu na viumbe hai wengine tunategemea mazingira ili kupata chakula, malazi na mahitaji mengine. Mazingira yanatupa kila kitu bure lakini inasikitisha kuona inatuwia ngumu wakati in mwingine kulinda mazingira yetu.

Mahatma Gandhi, mpigania uhuru na baba wa taifa la India, aliwahi kusema: “Dunia ina uwezo wa kumpa kila mtu mahitaji yake, lakini dunia haiwezi kumtosheleza binadamu mroho."

Kila siku tunashuhudia watu wanatupa taka ovyo tena bila kujali. Aidha, tunaendelea kushuhudia moshi na gesi mbalimbali kutoka majumbani, viwandani na vyombo vya usafiri; watu wanakata miti hovyo; watu wanatiririsha maji taka kwenye mitaro na maji yenye kemikali yanaendelea kutiririka na kuingia kwenye vyanzo vya maji.

Haya yote yanatokea angali tunajua watu, wanyama na mimea katika dunia hii tunategemea maji katika kuishi kwetu.

Mwanasheria kutoka timu ya wanasheria watetezi wa mazingira kwa vitendo (LEAT), Mary Kessy, anasema Kanuni ya 10 ya Tamko la Rio la Mazingira na Maendeleo la mwaka 1992 linaeleza kuwa matatizo ya kimazingira yanatatuliwa kwa kiwango cha hali ya juu pale tu panapokuwa na ushiriki wa watu katika nyanja mbalimbali kuanzia ngazi ya chini yaani mtu mmoja mmoja na mpaka ngazi ya juu kabisa. Hii ni kwamba kila mtu ana wajibu na nafasi yake katika kulinda na kuyatunza mazingira.

Katika kutimiza wajibu wetu wa utunzaji wa mazingira, wananchi wanaweza kushiriki vyema kwa kufanya maamuzi yanayolinda mazingira, kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuhusiana na shughuli yeyote ambayo inaweza kuathiri mazingira kwa namna moja ama nyingine.

Hali kadhalika, mamlaka zenye dhamana zina wajibu wa kutoa taarifa juu ya hali ya mazingira kwa wananchi ambao kiasili ndio wamiliki wa mazingira na maliasili.

Kizazi kilichopo kina wajibu wa kusimamia, kutumia na kutunza mazingira kwa manufaa yao wenyewe bila kuathiri uwezo wa kizazi kijacho kunufaika maliasili zilizopo.

Kessy anafafanua kuwa msingi wa wajibu wa wananchi katika kutunza mazingira na maliasili umeelezwa wazi chini ya ibara ya 27 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1997 kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kwa mara.

Inaelezwa kwamba, kila mtu ana wajibu wa kutunza maliasili za Jamhuri ya Muungano, mali za serikali, mali zote zinazomilikiwa na watu kwa pamoja na pia kuheshimu mali za mtu mwingine. Pia, kila mtu ana wajibu wa kuzuia aina yoyote ya uchafuzi, uharibifu na kulinda uchumi wa nchi kwa kuzingatia fikra yakinifu ya kwamba watu ndio nguzo ya mafanikio ya nchi yao.

Ijapokuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haijaeleza wazi juu ya suala la haki za kimazingira ikiwemo haki ya kuishi katika mazingira safi na salama na suala zima la utunzaji wa mazingira, ibara ya 27 inayoelezea wajibu wa kutunza maliasili inaweza ikafafanuliwa kwa kina zaidi na kujumuisha utunzaji wa mazingira.

Hii ni kwa sababu maliasili kama vyanzo vya maji, misitu, wanyamapori na ardhi ni sehemu ya mazingira.

Wajibu wa kutunza mazingira kwa kila mtu umeelezwa wazi pia kwenye sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 (Sheria Na. 20 ya mwaka 2004) chini ya kifungu cha 6 kwamba kila mtu anayeishi Tanzania ana wajibu wa kutunza mazingira na kutoa taarifa kwa mamlaka husika, juu ya shughuli au mradi wowote au kitu chochote ambacho kinaweza kikaathiri mazingira.

Utunzaji wa mazingira na maliasili ikiwa kama wajibu wa kila mtu, serikali nayo inawajibu wa kuyatunza mazingira na kuhakikisha kuwa mazingira yanatunzwa na kusimamiwa ipasavyo katika shughuli za uzalishaji kwa kizazi kilichopo bila ya kuathiri mazingira kwa ajili ya uzalishaji na manufaa ya kizazi kijacho.

Serikali ina wajibu wa kutunga sera bora, sheria, kuunda mikakati na miongozo bora pamoja na kutekeleza mipango iliyowekwa kwa ajili ya kutunza mazingira na maliasili.

Wajibu wa kutunza mazingira uko sambamba na haki ya kuishi kwenye mazingira safi na salama. Kama una haki ya kuishi katika mazingira safi na salama basi kama mtanzania unawajibu pia wa kuyatunza mazingira ili kuilinda haki yako ya kuishi mazingira safi.

Haki ya kuishi katika mazingira safi na salama ni haki ambayo watu kwenye jamii wanaweza kuilinda kwa kuonyesha ushirikiano katika kutunza mazingira yao.

Wajibu ulioelezwa kifungu cha 6 cha sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 kama utatekelezwa vyema basi itachangia kwa kiasi kikubwa kulinda haki ya kuishi katika mazingira safi na salama.

Licha ya watu kupewa jukumu la kutunza mazingira kama sehemu inayoathiri maisha yao, wamekuwa pia wachangiaji wakubwa wa uharibifu wa mazingira.

Utupaji wa taka hovyo, ukataji wa miti holela, uharibifu au uchafuzi wa vyanzo vya maji na shughuli nyingine nyingi za wananchi ni vitu ambavyo vinakwamisha sana suala la utunzaji wa mazingira kwa manufaa yetu na kizazi kijacho.

Vyote hivyo vinaweza vikawa vimechangiwa na sababu moja ama nyingine zikiwemo, uelewa mdogo juu ya suala zima la wajibu wa kutunza mazingira na miundombinu mibovu.

Kuna baadhi ya watakaosema kuwa suala la kutunza mazingira ni wajibu wa serikali kumbe ni wajibu wa kila mtu. Hivyo basi kuna uhitaji mkubwa wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu wajibu wao katika utunzaji wa mazingira.

Pia, baadhi ya wananchi hupuuzia sheria na pia kuna mwitikio hafifu wa wananchi kwenye masuala yanayohusu mazingira. Hi ni moja ya changamoto inayokumba suala la utunzaji wa mazingira.

Inapokuja suala mzima la usafi wa mazingira ni wajibu wa kila mtu kuhakikisha mazingira yanayomzunguka yanakuwa safi na salama, watu wanaokaidi na kupuuzia wanayoelekezwa inabidi wachukuliwe hatua za kisheria.

Kila mtu atimize wajibu wake kuyatunza mazingira, kwa pamoja tuyalinde mazingira yetu na mazingira yatutunze.

Habari

Michezo

Biashara

Burudani

Afrika