Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 11 01Article 567211

Maoni of Monday, 1 November 2021

Columnist: www.habarileo.co.tz

Utendaji wa Samia unavyoakisi maneno ya Nyerere

Rais Samia Hassan Suluhu Rais Samia Hassan Suluhu

UTENDAJI wa Rais wa Serikali ya Awamu ya Sita Samia Suluhu Hassan, umeonekana kuakisi maono aliyoyatoa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere katika hotuba yake ya kwanza, alipochaguliwa kuwa Waziri Mkuu, mwaka 1961.

Katika hotuba hiyo, Mwalimu Nyerere alitoa maagizo matatu kwa Watanganyika ambayo ni kuchapa kazi, kudumisha umoja na undugu.

“Kwanza, kazi. Kwani ni kazi peke yake itakayotuondolea umasikini wetu.

“Pili, umoja. Kwani bila umoja, hatuna nguvu ya kuendelea na jambo lolote. Tatu, undugu. Ili uhuru usilete utengano baina yetu na Waafrika wenzetu au binadamu wenzetu,” alisema Mwalimu Nyerere.

Alieleza namna taifa hilo la Tanganyika lilivyopata uhuru na kuanza upya huku likiwa halina fedha, idadi kubwa ya wananchi wake hawana elimu ya kutosha na pia likiwa na idadi ndogo ya wananchi tofauti na mataifa mengine yaliyopata uhuru kipindi hicho kama vile Ghana na Nigeria.

“Kwa hiyo, tunaanza bila ya kuwa na wananchi wa kutosha wenye elimu ya juu tunayohitaji katika jitihada zetu za kujenga utajiri wa nchi hii. Lakini matatizo haya, hayanitishi mimi, hayawatishi wenzangu, na wala hatuombi kwamba yawatisheni ninyi,” alisisitiza.

Aliongeza, “Tukiweza kumshinda adui huyu, tutakuwa tumeweza kupata silaha itakayotuwezesha kuushinda ujinga na maradhi. Lakini ni ninyi tu, tunaoweza kupigana vita vya umasikini. Namuomba kila raia wa Tanganyika, aape kiapo cha kuwa adui wa umasikini.”

Alisema mtu yeyote mwenye shamba lenye rutuba au aliyelima pamba lakini kwa uvivu tu akaacha kuzivuna, huyu si adui wa ujinga, umasikini na maradhi bali ni rafiki wa maadui hao.

Kuhusu umoja, alisema umoja ndio msingi wa mafanikio kwa nchi yeyote na kubainisha kuwa uhuru wa Tanganyika hakuna asiyejua kuwa umetokana na umoja wa chama cha TANU.

“Ndugu zangu, huu si wakati wa kuchezea umoja wetu, tunauhitaji sasa kama tulivyohitaji zamani kwa ajili ya kuinua hali zetu na ndugu zetu,”

Alisisitiza pia juu ya Tanganyika, kudumisha undugu na nchi jirani ikiwa ni pamoja na kuwa mstari wa mbele kusaidia nchi hizo pindi zinapokuwa kwenye matatizo huku akionya kamwe Tanganyika isijitenge.

“Ikiwa ndugu zetu katika nchi za jirani wana taabu, na tunajua wanazo taabu nyingi, wajibu wetu ni kutumia umoja wetu kuwasaidia, na kuwaonyesha kwa mfano, jinsi umoja unavyoweza kuwasaidia wao pia. Kila nilikokwenda, nilipokuwa Ghana na Nigeria, nilikumbushwa faida ya umoja,” alisema.

Hotuba hiyo ya Mwalimu Nyerere, inaakisi kwa asilimia kubwa utendaji na mambo mengi anayoyasisitiza Rais Samia ambayo ni watanzania kuchapa kazi kupambana na adui masikini, kudumisha umoja na mshikamano pamoja na kudumisha ushirikiano wa kimataifa.

Tangu aingie madarakani Machi, mwaka huu, kutokana na kifo cha Rais wa Awamu ya Tano Dk John Magufuli, Rais Samia ameonesha kwa vitendo na kutembea kwenye maneno na wosia wa baba wa taifa, kupitia kauli mbiu yake kazi iendelee akihamasisha watanzania kuchapakazi kazi na kuondakana na umasikini.

Lakini pia Rais Samia katika takribani kila hotuba yake aliyoitoa jambo la umoja na mshikamano limekuwa ni kipaumbele chake huku akiwataka viongozi wa dini kuhamasisha waumini wao kuitunza amani, umoja na mshikamano uliopo nchini.

Suala la kuendeleza undugu na nchi za jirani, amekuwa akilitekeleza pia kwa vitendo ambapo amefanya ziara katika nchi za Kenya, Burundi, Uganda na Rwanda lakini pia amehudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, na mkutano wa wakuu wa nchi Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Africa (SADC).