Uko hapa: NyumbaniWallMaoniArticles2019 11 14Article 487579

Maoni of Thursday, 14 November 2019

Columnist: mwananchi.co.tz

Viboko vinawasaidia watoto kiwango gani?

Viboko vinawasaidia watoto kiwango gani?

Ni kwa kiasi gani fimbo au viboko vinawasaidia watoto katika muktadha mbalimbali wa maisha? Jambo hili linahitaji mjadala na mabishano ya muda mrefu na bado wahusika wanaweza wasifikie muafaka kirahisi.

Mijadala ya fimbo ni migumu kutokana na falsafa, maono na fikra kinzani zinazoendana na utashi wa watu wanaolitizama jambo lenyewe, utata uliomo katika jambo lenyewe na utamaduni wa jamii husika.

Mtizamo wa kifamilia

Kila familia ina malezi yake ambayo huamua aina ya adhabu ambayo watoto hukutana nayo pindi wanapotenda makosa. Adhabu hizo hutofautiana kutokana na ukubwa wa makosa ambayo mtoto anakuwa ametenda. Mathalani, familia yangu kwa maana ya watoto wangu, kwa kawaida hawachapwi fimbo kwa makosa yote madogomadogo au ya bahati mbaya, ya kila aina, lakini huchapwa pale wanapofanya makosa makubwa mara ya kwanza au makosa ya kati yanayojirudiarudia.

Ukubwa au udogo wa kosa au kipimo cha kosa pia ni mjadala unaootegemea falsafa nyingi zisizo na majibu. Kwa kifupi kila familia ina namna ya malezi ambayo yanapima uzito na ukubwa wa kosa alilotenda mtoto na aina ya adhabu itakayofuatia.

Ziko familia ambazo mtoto akifanya kosa dogo sana anachapwa, akifanya kosa la kati anachapwa pia, akifanya kosa la juu anachapwa vilevile.

Ziko familia ambazo hata mtoto akifanya makosa makubwa haguswi, makosa makubwa kwa mtizamo wa kifamilia ambao nimeutumia kulea watoto wangu ni ile hali ya makosa ambayo yana madhara makubwa katika tabia za mtoto atakapokua mkubwa. Mathalani, ikiwa mtoto anagoma kutenda jambo aliloelekezwa kutenda, nyumbani kwangu hilo ni kosa kubwa na linastahili fimbo kwa mtoto mpaka siku atakapoacha.

Kwamba mtoto anaweza kuropoka neno fulani baya kwa mara ya kwanza akaonywa na kufahamishwa, lakini mtoto yuleyule akitumwa dukani akakataa kwenda, hilo si kosa la mazungumzo peke yake, kwa hakika ni mazungumzo na viboko.

Lakini ziko familia ambazo, hata mtoto akigoma kutenda maelekezo aliyopewa, hawezi kuguswa na huendelea kulindwa na kutetewa. Hizi ni aina ya familia ambazo wazazi wamewaacha watoto wajiamulie masuala wenyewe, wazazi wakiamini kuwa namna bora ya kulea watoto ni kuwapa uhuru wa kuamua hata wanapotumwa majukumu na wakubwa.

Tunaweza kuwalea bila viboko?

Ndiyo, inawezekana kabisa. Ziko familia ambazo watoto wao hawaguswi na fimbo na hawajawahi kuguswa na fimbo, ukitembelea familia za namna hiyo unastaajabishwa na kiwango cha juu cha nidhamu za watoto, adabu, kujituma na utulivu.

Ukifuatilia watoto wa namna hiyo, bado utakuta ni watoto wenye upeo mkubwa wa kielimu na utakutana na sifa zao shuleni na nyumbani.

Familia za namna hii ni zile zilizowekeza kwa watoto tokea wakiwa wadogo, zikawajengea misingi ya kufanya maamuzi sahihi na kuwasikiliza maelekezo bila kusukumwa, hizi ni familia ambazo mtoto akiwa na mwaka mmoja au miwili tayari anaanza kufundishwa kutumwa hapa na pale ndani ya nyumba, ufundishaji ambao una lengo la kumfanya mtoto aanze kuyaishi maisha halisi ya kuchangamka na kutekeleza masuala anayoambiwa.

Pamoja na kuwepo kwa mbinu nyingi za malezi, mbinu hizi haziwezi kufanya kazi ikiwa udhihirikaji wake kwa mtoto hauwezi kuanza tangu utotoni ili azoeshwe kutenda masuala bila kusukumwa.

Walezi na wazazi wengi ambao huanza kuchapa watoto tangu wakiwa na umri mdogo, na tena uchapaji wenyewe ukihusisha nguvu, vitisho na makatazo huwafanya watoto hao kujenga usugu tangu utotoni na baadaye kuwa mzigo kwenye malezi ya utu uzima.

Njia zote zinawezekana

Malezi ya watoto wetu bila viboko yanawezekana, lakini yanapaswa kuhusisha makosa ya watoto ambayo ni ya kawaida. Makosa makubwa yanayotokana na kiburi au aina nyingine za utovu wa nidhamu ambao umekithiri, vinaweza kutatuliwa kwa kutumia njia zote muhimu; kuzungumza na mtoto, kumuonya kwa upole au ukali, kujipa muda wa kukaa naye na kumpa ushauri nasaha, kumpa adhabu za kiwajibu zinazohusisha kumnyima haki fulani kwa kipindi fulani ili ajutie makosa yake, kumpa adhabu za kazi ngumu au rahisi, au mchanganyiko wa adhabu hizo zote ikiwa ni pamoja na viboko.

Mjadala huu unaweza kuendelea kutufungua macho na kutuonyesha ni kwa kiasi gani bado nchi za Afrika zinahitaji kujizatiti katika mifumo yake muhimu ya kulea jamii kuliko kuiga kila kitu kutoka Magharibi.