Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 11 14Article 571102

Maoni of Sunday, 14 November 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

WANAUME: Chama la kibabe la wakomaaji

WANAUME: Chama la kibabe la wakomaaji WANAUME: Chama la kibabe la wakomaaji

WACHEZAJI wa kigeni wameendelea kuwa tishio katika vikosi vya timu zetu kutokana na kuwa siriaz kazini tofauti na wachezaji wetu wengi, lakini kuna wazawa hao hawataki utani. Wanakomaa nao.

Simba na Yanga ndizo zinazoongoza kwa ushindani wa kusajili wageni, ingawa na Azam FC kwa sasa inaingia kwenye anga hizo, jambo ambalo linawavuruga wazawa wengi hasa wale ambao hawapendi kujituma.

Wazawa ambao wamehamia kwenye timu kubwa zilizojaa ushindani na nyota wa kigeni ni lazima wajipange kisawasawa ili kutoboa, vinginevyo itakula kwao.

Miongoni mwa wazawa ambao wanatakiwa kukaza msuli ni Jeremiah Kisubi, Kibu Denis, Yusuf Mhilu, Jimmyson Mwanuke na Israel Mwenda ambao wametua Simba, huku David Bryson, Dickson Ambundo, Erick Johora na Yusuf Athuman wakitua Yanga.

Mwanaspoti linakuletea kikosi cha mastaa wazawa waliotafuna mfupa uliowashinda wengi, wanaotoa somo kwa wengine wanaojiunga na timu hizo.

AISHI MANULA

Ndiye mbadala wa Juma Kaseja kwenye timu ya Taifa ‘Taifa Stars’. Hii ni kutokana na ubora anaouonyesha kwenye klabu yake ya Simba tangu alipotua akitokea Azam msimu wa 2017-22. Ubora wa kipa huyo si wa kusimuliwa anaonyesha kwa vitendo kila apatapo nafasi ya kucheza.

Kabla ya Manula, pale Simba wamepita makipa wengi, lakini wameshindwa kuonyesha kiwango bora na kujikuta wakitemwa huku wengine wakibakia kuwa watazamaji mbele ya Manula, mfano alikuwepo Deogratius Munishi ‘Dida’, Said Nduda, Emmanuel Mseja na Beno Kakolanya ambaye anadaka mara moja moja.

SHOMARI KAPOMBE

Ni panga pangua kwenye kikosi cha Simba, licha ya kusajiliwa mastaa wengine ndani ya kikosi hicho wameshindwa kufua dafu mbele yake, ukiachana na klabu yake, pia ni tegemeo Stars.

Simba ilimsajili Haruna Shamte, David Kameta ‘Duchu’, Zana Coulibaly ambaye aliletwa baada ya Kapombe kuumia, lakini ‘Show Me’ alipopona tu, Zana alishindwa kuhimili ushindani akaondolewa.

KIBWANA / TSHABALALA

Japokuwa usajili wa Kibwana Shomari, haukuwa wa mbwembwe, huku wengine wakimbeza kutokana na kimo chake, amewafunga mdomo kwa kuwaonyesha kazi makini uwanjani, mbali na kusajiliwa kama beki namba mbili ndani ya Yanga anaweza kumudu kucheza beki tatu na kuwakalisha pembeni kina Adeyum Saleh, Yassin Mustafa na David Bryson.

Kwa upande wa nahodha msaidizi wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ameishikilia namba hiyo kwa muda mrefu, akaletwa Asante Kwasi akaondoka na sasa anamsugulisha benchi Gadiel Michael.

BAKARI MWAMNYETO

Alisajiliwa kutoka Coastal Union ya Tanga,kuziba pengo la Kelvin Yondan, amelifanikisha hilo na amekuwa tegemeo kwenye kikosi cha Yanga na Taifa Stars.

Tangu amejiunga na timu wamepita mabeki mbalimbali kama Lamine Moro, bado alionyesha uimara na akastahimili kupangwa naye, wakati mwingine walikuwa wanacheza na Abdallah Shaibu ‘Ninja’.

DICKSON JOB

Ni beki aliyehimili mikiki mingi ya washambuliaji akiwa ndani ya Yanga tangu amesajiliwa msimu uliopita na kudumu kwenye nafasi hiyo hadi sasa.

Huduma yake inaifaa siyo Yanga tu, bali ni beki wa kati tegemeo Stars, alianza kucheza kuanzia timu za vijana za taifa tangu akiwa Mtibwa Sugar.

MZAMIRU YASSIN

Ni miongoni mwa wachezaji wazawa ambao wameonekana kulinda vipaji vyao na kulinda kiwango chake, kilichomfanya adumu Simba hadi sasa, wakati wapo wachezaji waliokuja katika nafasi yake, wakaondoka.

Kiungo huyu licha kuongezewa changamoto eneo lake ambao ni Thadeo Lwanga na Sadio Kanoute, bado ameendelea kubaki akiingia na kutoka katika kikosi cha kwanza.

FARID MUSSA

Ni msimu wake wa pili tangu ajiunge Yanga akitokea Hispania aliko-kuwa akicheza klabu ya Tenerife, ha-kua-nza vizuri kutokana na kukaa nje miezi sita bila kucheza, hivyo akawa anarejea taratibu.

Kwa sasa Farid amerejea kwenye kiwango kizuri na amekuwa akitoa pasi za maana na hadi sasa ametoa asisti mbili. Anaingia na kutoka kwenye kikosi cha kwanza msimu huu.

JONAS MKUDE

Aliingia Simba akitokea timu B. Tangu alipoaminiwa amekuwa hatingishwi na ujio wa wageni. Hata hivyo, kusajiliwa kwa Tadeo Lwanga na migogoro yake ya hapa na pale na uongozi wake ndivyo vilivyomtoa kikosini. Lakini kuumia kwa Lwanga kumemrejesha kikosi cha kwanza. Mkude alipandishwa pamoja na Ibrahim Ajibu, Abdallah Seseme, Christopher Edward na William Lucian walioondoka.

Simba ilisajili wachezaji wa kumpa changamoto Mkude kama James Kotei, Nicholas Gyan ambao waliondoka baadaye,

JOHN BOCCO

Kwasasa ndiye msambuliaji mzawa ambaye anafanya vizuri bila ya kiwango chake kushuka, amedumu kikosi cha kwanza tangu yupo Azam FC, pamoja na ushindani uliopo kwenye namba yake bado anastahimili kikosini.

Ndani ya kikosi hicho anacheza mastraika mbalimbali akiwemo Meddie Kagere na Chris Mugalu ambao ni wageni lakini bado anaonekana muhimu.

FEISAL SALUM

Ukitaja viungo bora wa ushambuliaji kwa sasa, moja ya majina ya kwanza kabisa litakuja la Fei Toto. Licha ya umri wake kuwa mdogo katika nafasi yake, anapambana na Saido Ntibanzonkiza bado anapenya.

Ndiye kinara wa upachikaji wa mabao ndani ya Yanga (3, astisti 1).

WASIKIE HAWA

Nyota wa zamani wa Simba, Godwin Aswile anasema; “Inafurahisha kuona wachezaji wazawa wanajijengea ufalme wao Simba na Yanga, inanikumbusha zamani ambapo wageni walikuwa wachache sana, kwasababu tulionyesha uwezo.”

Aliyekuwa winga wa Yanga, Edibly Lunyamila anasema: “Kufanya vizuri kwa wazawa kunasaidia kuwa na timu ya taifa imara.”