Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 05 29Article 540481

xxxxxxxxxxx ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Waamuzi sawa vipi kuhusu ratiba ya ligi

MJADALA mkubwa hivi sasa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ni kuhusu mkataba mpya uliosainiwa baina ya Azam Media na Shirikisho la Soka wa miguu nchini TFF.

Mkataba huo wa miaka 10 wenye thamani ya Sh bilioni 225.6 unatarajia kutatua matatizo mengi katika soka la Tanzania ambalo linakua kwa kasi siku za karibuni na kuongeza mvuto wa ligi.

Awali timu ndogo za Ligi Kuu ya Tanzania Bara zilikutana na wakati mgumu kushiriki kutokana na kukosa fedha za kutosha za kuandaa kambi lakini pia fedha za kusafiri kutoka kituo kimoja hadi kingine kwaajili ya kucheza michezo ya ligi na kombe la Shirikisho la Azam.

Lakini pia TFF itaenda kuboresha baadhi ya maeneo yake hasa upande wa waamuzi ambao walikuwa wakitupiwa lawama kila uchwao na klabu pamoja na wadau wa soka kwa kula rushwa na kuzipa upendeleo timu kubwa.

Hii ilichangiwa kwa kiasi kikubwa na kucheleweshwa kwa posho zao pindi wanapomaliza majukumu yao jambo lililopunguza ufanisi wao na kusababisha kutupiwa lawama kwa kushindwa kuzitafsiri vema sheria 17 za soka.

Lakini kupitia kwa madhaifu hayo baadhi ya klabu zimekumbana na adhabu baada ya mashabiki wao kusababisha vurugu kwa kushindwa kukubaliana na maamuzi ya waamuzi ambao wengine walikumbana na adhabu pia.

Kitendo cha rais wa TFF, Wallace Karia, kusema kuwa sasa kilio cha waamuzi itakuwa historia ni ishara nzuri katika ustawi wa soka letu ambalo sasa limekuwa likitolewa macho kutokana na ushiriki wa Simba katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo ndani ya miaka mitatu imefika mara mbili hatua ya robo fainali.

Nimefarijika na suala la waamuzi kupatiwa ufumbuzi lakini vipi kuhusu panga pangua ya ratiba ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara nayo lini itapatiwa muarobaini na kupunguza malalamiko kwa klabu.

Kilio cha ratiba katika ligi imekuwa wimbo unaochosha zaidi katika masikio ya wapenda soka na kuwa kero ambayo inachafua taswira ya soka.

Baada ya kupata dawa ya waamuzi naamini ni wakati muafaka kwa bodi ya ligi chini ya Ofisa mtendaji mkuu Almas Kasongo, pia kupatia ufumbuzi wa jambo hili ambalo limekuwa likizisababishia hasara klabu pamoja na mashabiki wake.

Rejea kile kilichotokea katika mchezo wa Ligi Kuu baina ya Simba na Yanga mabadiliko ya ratiba muda mchache kabla ya mchezo yalisababisha kuibua mtafaruku mkubwa kwa mashabiki pamoja na klabu hizo kubwa naamini msimu ujao tatizo la ratiba litakuwa historia pia.

Join our Newsletter