Uko hapa: NyumbaniWallMaoniArticles2020 07 30Article 506098

Maoni of Thursday, 30 July 2020

Columnist: HabariLeo

Wadau wana nafasi kusaidia uboreshaji elimu

Wadau wana nafasi kusaidia uboreshaji elimu

NI takribani mwezi sasa tangu kufunguliwa tena kwa shule baada ya kufungwa katika juhuzi za kupambana na ugonjwa wa corona uliozikumba nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.

Tangu Juni 29 shule zilipofunguliwa, tahadhari kadhaa zinaendelea kuchukuliwa kwa umakini pale wanafunzi wanapoingia shuleni asubuh mpaka kuondoka.

Licha ya shule kufunguliwa wadau mbalimbali wamekuwa wakiangaliwa kwa jicho la ukaribu namna wanavyoweza kujitoa kusaidia shule za msingi na sekondari ili kuhakikisha muda wote watoto wanaendelea kubaki katika afya njema kwa kunawa mikono kwa maji safi na sabuni za kunawia mikono.

Kagera ni miongoni mwa mikoa inayoendelea kusimamia kwa ukaribu utaratibu mzima wa kujikinga ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza katika kipindi hiki cha ugonjwa wa corona. Mbali na corona, hatua zinazochukuliwa pia zinasaidia watoto mashuleni kujikinga na magonjwa kama ya kuhara na hata kuambukizana mafua.

Kwa mujibu wa kaimu ofisa elimu mkoa wa Kagera, Maya Mubaraka, ofisi yake inaendelea kupokea wadau mbalimbali ambao wako tayari kutoa msaada wa vifaa vya kunawia mikono kama vile ndoo na sabuni ili kuwakinga watoto walioko mashuleni na tishio la magonjwa.

“Hii ni nafasi muhimu kwa wadau ambao tunaangalia sisi kama ofisi ya elimu tunaweza kushirikiana vipi kuwakinga watoto wetu wasipate ugonjwa na kusimamia sheria zote na miongozo ya wizara ya afya kwa kushirikiana na wadau wa elimu,” anasema Mubaraka.

Mkoa wa Kagera una shule takribani 900 za msingi na 193 za sekondari. Shule zote hizo zinatakiwa kuchukua tahadhari ya kunawa mikono huanzia asubuhi hadi jioni na hufanyika watoto wanapofika asubuhi shuleni, wakati wa mapumziko, wakati wa kumaliza michezo na wakati wa kurejea majumbani.

Kwa kufuata miongozo ya wizara ya afya, walimu wakuu wa shule za msingi walitakiwa kutenga ndoo moja kwa wanafunzi 25 wa shule za msingi na ndoo moja kwa wanafunzi 50 wa shule za sekondari.

Siku chache hizi tangu shule kufunguliwa kumekuwepo na changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya wanafunzi kupasua vifaa vya kunawia mikono, kuharibu sabuni na baadhi kujirundika katika ndoo moja.

Uchunguzi unaonesha kwamba shule za serikali zinatumia asilimia 10 inayotokana na mfuko wa elimu bila malipo katika kipengele cha matumizi ya ofisi kwa shule za msingi na asilimia 10 kutoka katika kipengele cha kununua dawa ili kununua vifaa vya kunawia na sabuni katika shule za sekondari.

Ingawa kiasi hicho hakikidhi haja kwa asilimia 100 kuhusu vifaa vya kujikinga na corona, endapo wadau mbalimbali watajitokeza kusaidiana na idara ya elimu kununua vifaa hivyo, itasaidia sana kupeleka fedha zinazotumika sasa kununua vifaa kwa ajili ya corona kwenda kwenye matumizi yaliyokusudiwa.

Neema Rugangila ni mkurugenzi wa Shirika la Agrithamani Foundation lililoanzishwa mwaka 2018 likiwa na lengo la kutoa elimu ya lishe kwa ujumla ili kupambana na udumavu na kuhamasisha kilimo cha mbogamboga mashuleni.

Baada kuangalia uhitaji mkubwa wa sabuni za kunawa mikono shuleni alifika ofisi ya elimu na kuomba angalau ‘kuikomboa’ halamshauri moja kati ya nane za mkoa wa Kagera kwa kutoa mafunzo ya kutengeneza sabuni wenyewe ili kuokoa gharama kwa kununua sabuni za viwandani ili fedha hizo zitumike kwa masuala mengine.

Wakusudiwa wa mafunzo hayo walikuwa ni pamoja na maofisa afya wa vituo mbalimbali.

"Katika kutafakari wazo langu ambalo nilitakiwa niwasiliane na ofisi ya elimu mkoa niliona ongezeko la gharama kubwa kwa shule zetu maana sikudhani kama bajeti ya sabuni za kunawa mikono kwa kiwango ambacho kinatakiwa ilikuwepo shuleni, na nikawaza je shule hizi zitafanyaje ili waweze kununua hizi sabuni ambazo ni muhimu kwa ajili ya usalama wa watoto wetu?” Anasema Rugangila

Anaongeza: “Ndipo nikaona badala ya kununua sabuni na kuwapa mashule kama msaada ni vyema zaidi nitoe elimu ya kutengeneza sabuni za maji kwa walimu wa afya shuleni na maofisa afya wa kata ili walimu waweze kutumia ujuzi huu kutengeneza sabuni shuleni wenyewe. Hii itapunguza gharama kwa shule kwa kiasi kikubwa sana maana badala ya kununua sabuni sasa watanunua vifaa vya kutengenezea sabuni hata kwa mwaka mzima bila kuathiri bajeti yao kwa upana,” anasema.

Anasema shule zote za msingi na sekondari 45 ilizoko katika Manispaa ya Bukoba baada ya mafunzo hayo sasa zinaweza kutengeneza sabuni zao zenyewe baada ya mafunzo hayo.

Matarajio ya Neema ni kuwa maofisa afya wa kata waliopata elimu hii ni kuendelea kusimamia utengenezaji wa sabuni shuleni huku wao pia wakijitengenezea kwa ajili ya jamii mfano vituo vya afya na kaya zao na kupunguza matumizi.

“Kupitia Agri Thamani Foundation tutahakikisha kuwa kwa kushirikiana na idara za elimu na afya mkoa wa Kagera tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na maofisa afya wa kata ili tuhakikishe kuwa elimu hii inaleta manufaa yaliyotarajiwa na inakuwa endelevu.

“Wito wangu ni watumie elimu hii kwanza kwa ajili ya kulinda na kuwakinga watoto wetu shuleni ambapo zaidi ya watoto 56,000 kutoka shule 45 za Manispaa ya Bukoba watanufaika moja kwa moja na mafunzo tuliyoyatoa,” anasema.

Hata hivyo, anasema wadau wanayo fursa ya kuhakikisha watoto wanaendelea vizuri kwa kusaidia bajeti za shule zinafanya vitu vingi, na zinakuwa na fursa ya kuhakikisha wanaunganisha mawazo pamoja ili kuhakiksha elimu inasonga mbele.

Mwenyekiti wa Agrithamani Foundation, Mizengo Pinda, anasema pamoja na kutoa elimu katika mkoa wa Kagera shirika hilo linaendelea kutoa huduma zake katika mikoa ya Geita, Mwanza, Kigoma, Tabora na Dodoma.

Anasema mikoa hiyo itanufaika pia na kwamba ni fursa kwa watakaobahatika kujifunza kutengeneza sabuni na kuuza sabuni kwa jamii kwa gharama nafuu ili kila mwananchi aweze kuwa na sabuni ya maji ya kunawa mikono nyumbani kwake.

Pinda anasema matarajio yake baada ya Agri Thamani kutoa mafunzo haya kwa walimu ni wao pia waende kuwa walimu kwa wengine maana uhitaji wa sabuni ya maji ya kunawa mikono ni mkubwa nchini na kwamba ni vyema wanafunzi wafundidhwe pia katika vipindi vya stadi za kazi.

Mafunzo ya kutengeza sabuni yalijumuisha watu 120, walimu wa afya mashuleni wakiwa 45, maofisa afya wa kata 14, wanawake ambao waliwahi kuhitimu kidato cha nne walikuwa 61 na wote walijitoa kutengeneza lita 600 za sabuni kama kianzio cha watoto kunawa mikono katika shule 45 za msingi na sekondari katika manispaa ya Bukoba.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kagera, Dk Boniphace Kayegeji anasema kutokana na kunawa mikono, kasi ya magonjwa ya kuhara na matumbo imepungua.

“Unaweza kumaliza wiki nzima kwa sasa bila kupata kesi hata moja ya watoto wanaohara au kuumwa tumbo kwa sababu kunawa mikono hakuondoi tu ugonjwa wa corona bali hata afya zinaimarika na kupunguza magonjwa mbalimbali kwa watoto,” anase Kayegeji.

Afisa elimu wa shule za msingi Manspaa ya Bukoba, Elpidius Baganda anasema lita 600 zilizotengenezwa zinaendelea kutumika vizuri na wanafunzi wanaendelea kunawa mikono.

Anahamiza wadau wengine kuchangia walicho nacho katika kuboresha elimu popote walipo.

Join our Newsletter