Uko hapa: NyumbaniWallMaoniArticles2021 02 22Article 525742

Maoni of Monday, 22 February 2021

Columnist: HabariLeo

Wakati umefika Posta kwenda kidijitali

Wakati umefika Posta kwenda kidijitali Wakati umefika Posta kwenda kidijitali

SIKU za karibuni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile aliagiza Shirika la Posta Tanzania (TPC), kwenda na mabadiliko ya teknolojia ili kuwa kisasa zaidi katika kutafuta fursa mpya za biashara na ustawi wake.

Agizo hilo lilitolewa wakati Waziri Ndugulile alipokuwa akifungua kikao kazi cha menejimenti na mameneja wa TPC kilichofanyika jijini Dodoma kwa ajili ya kujadili utekelezaji wa majukumu yake.

Ndugulile alieleza kuwa shirika hilo haliwezi kuendeshwa kama zamani bali liende na mabadiliko ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) pamoja na mahitaji ya sasa ya dunia.

Katika kuweka msisitizo wa hilo alisema kila mkoa una aina tofauti ya fursa na kuwataka mameneja wa mikoa wa shirika hilo waziangalie ili kuleta mabadiliko chanya pamoja na kulifanya liwe miongoni mwa taasisi zenye mapato makubwa na mchango mkubwa kwa taifa.

Anachosema Ndugulile ni ukweli kwa ni shirika hilo lina mtandao mpana ndani ya nchi na kuunganishwa na matawi mbalimbali ya Posta yaliyopo nchi nyingine hivyo likijiingiza vizuri katika biashara ya mtandao litaleta tija.

Lakini pia linapaswa kutafuta fursa mbalimbali za kufanya biashara na taasisi za serikali kwa ajili ya kupeleka nyaraka mbalimbali za siri na vifurushi mbalimbali. Hivyo kuna haja kwa TPC kuangalia upya muundo wake na kurugenzi kama upo sawa unaokidhi mahitaji lengo likiwa ni kuongeza tija, ufanisi na utendaji bora.

Lakini pia shirika hilo linapaswa kujitangaza zaidi ili kukuza biashara zake kwa kutumia mbinu mbalimbali za kutangaza masoko pamoja na kutengeneza vifaa vyenye nembo ya posta kwa mfano kutengeneza na kutumia shajara zenye nembo ya Shirika hilo.

Posta inatoa huduma ya kupokea barua, nyaraka, taarifa na bidhaa mbalimbali kutoka ndani nan je ya nchi na kuzifikisha nyumbani au ofisini kwa mtumiwa.

Na sasa shirika hilo linaanzisha huduma ya Posta Kiganjani ambapo simu ya mtu ndiyo itakayokuwa anuani yake.

Hatua hii ni kubwa sana kwa shirika hilo kwani namba ya simu ya mtu husika ndiyo itakayosajiliwa kama sanduku lake badala ya mtindo ule wa awali wa kufuata barua kwenye masanduku ya Posta yaliyopo maeneo mbalimbali nchini.

Hivyo ili kufikia azma hiyo ya Posta kwenda kidijitali mhusika atapata anwani yake kwa kujisajili katika mfumo wa Posta Kiganjani ili simu ya mhusika iwe na anuani yake rasmi.

Kwa kufanya hivyo mhusika atapata taarifa za ujumbe mfupi kupitia simu yake kuhusu barua au mzigo wake kwa ajili ya kumfahamisha mahali ulipo na namna ya utakavyosafiri.

Pia teknolojia hiyo itamwezesha mhusika kupata taarifa ya kutumwa au kupokelewa kwa mzigo wake kwa kupitia simu yake ya mkononi.

Ni ukweli usiopingika kuwa hivi sasa huduma za posta zitakuwa zimerahisishwa kupitia simu ya mkononi hivyo wadau wa shirika hilo wakiwemo wizara, taasisi za serikali, mashirika ya umma, mashirika binafsi, wafanyabiashara, wafanyakazi, wanafunzi na wananchi wote wanahamasishwa kujiunga na huduma hiyo ambayo itazinduliwa hivi karibuni. Hakuna shaka kuwa Posta sasa ipo kidijitali zaidi kutokana na mabadiliko ya kidunia ya sayansi na teknolojia yaliyopo.

Join our Newsletter