Uko hapa: NyumbaniUkurasaMaoniArticles2021 08 24Article 553360

Maoni of Tuesday, 24 August 2021

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz

Wako wapi kina Florent Ibenge wetu?

Kiungo wa Simba, Said Hamisi Ndemla Kiungo wa Simba, Said Hamisi Ndemla

Achana na lawama dhidi ya wachezaji zinazokuzwa na uamuzi wa kuongeza wageni Ligi Kuu Bara, eti kuwapa changamoto wajifunze, wako wapi makocha wa mfano wa Florent Ibenge, ambaye sasa anaifundisha RS Berkane?

Tumekuwa tukiwatupia lawama wachezaji wetu kwamba wamezubaa, hawajitambui, hawachangamkii fursa za kwenda nje na hawajifunzi chochote kutoka kwa wanasoka wageni wanaokuja kusakata soka Tanzania.

Kiungo kama Said Ndemla yuko pale Simba kwa muda sasa, akishuhudia nyota wa nje wakija na kuondoka wakimuacha anaendelea kuishi kwa matumaini. Hajifunzi kitu au viongozi wanamjazia nzi kiasi cha kutoonekana?

Yuko Ramadhani Kabwili anaendelea kusaini mikataba ili aendelee kuwa kipa wa akiba, akishuhudia nyota kadhaa wakija na kuondoka na kumuachia benchi lake.

Hata yule kijana mdogo mwenye talanta ya aina yake pale Azam, Yahya Zaydi anaendelea kuonjeshwa ladha ya kikosi cha kwanza lakini anasahauliwa benchi msimu unapoanza.

Hayo yote yanatosha kujaza mashuhuda maneno ya kuhalalisha wachezaji wageni kujazwa kwenye klabu za Tanzania. Ni rahisi kusema; “Kama anataka, Ndemla anaweza kushika kiungo cha juu pale Simba, lakini hajifunzi kwa wageni.”

Maneno hayo yaweza kusemwa dhidi ya Kabwili, Zayd na nyota wengine kadhaa walio klabu hizo tajiri na hivyo kutokuwa na tatizo la kanuni mpya ya kuruhusu wachezaji wageni 12 ili hawa wazawa wapate fundisho.

Lakini hakuna anayehoji; “Yuko wapi kocha anayetoka nje?”

Ibenge ni kocha raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) ambaye hivi sasa anaifundisha RS Berkane ya Morocco. Alianzia kibarua cha ukocha nchini Ufaransa ambako alikuwa anaifundisha ES Wasquehal mwaka 2008 kabla ya kwenda SC Douai alikofanya kazi kati ya 2010 na 2011.

Baadaye alivuka bahari na kwenda Asia ambako alikwenda kuifundisha klabu maarufu ya Ligi Kuu, Shanghai Shenhua mwaka 2012 lakini akadumu kwa mwezi mmoja kabla ya kuonyeshwa mlango wa kutokea.

Lakini baadaye akajiunga na AS Vita Club na baadaye kutangazwa kocha wa timu ya taifa ya Congo, aliyoifundisha kwa miaka mitano hadi aliposhindwa kuivusha hatua ya 16 bora wakati wa fainali za Mataifa ya Afrika za mwaka 2019.

Hivi sasa ameaminiwa na RS Berkane. Na ameanza kwa kuchukua nyota anaowafahamu kama Clatous Chama na Tuisila Kisinda, huku jaribio lake la kumnasa Mukoko Tonombe likigonga mwamba.

Yuko wapi kocha kama huyu ambaye bila shaka angesaidia si tu kuinua viwango vya wachezaji wetu waweze kushindana na hao wageni, bali hata ajira zake nje zingeweza kusaidia kuvuta wanasoka wetu wazawa kama anavyofanya huko Morocco kwa sasa.

Kama katika kiwango cha Ligi Kuu hakuna kocha mithili ya Ibenge, sitaki kumtaja Pitso Mosimane au Waarabu wengine kama kina, Nasreddine Nabi waliosambaa Afrika- watoto wetu na vijana wetu watafundishwa na nani wa kuweza kuwapika kiasi cha kushindana na wageni wanaokuja au kwenda nje wakiwa wameiva au wamekamilika.

Angalau zamani kina Sunday Kayuni, Mansour Magram na Talib Hilal walithubutu kwenda nje ya nchi na wakaaminiwa. Leo hii huoni hata jaribio la kocha mmoja kuomba kazi klabu za nje.

Wachezaji wetu wanachelea kwenda nje, makocha ndio kabisa!

Eneo hili halina budi kuangaliwa kwa makini zaidi.