Uko hapa: NyumbaniInfosAfya2019 11 15Article 488080

Health News of Friday, 15 November 2019

Chanzo: mwananchi.co.tz

Dawa za Kichina, kupunguza uzito tishio jipya magonjwa sugu ya figo

Dawa za Kichina, kupunguza uzito tishio jipya magonjwa sugu ya figo

Dar es Salaam. Chama cha Madaktari wa Figo Tanzania (Nesot) kimeonya matumizi ya dawa yasiyo sahihi zikiwemo za Kichina kuwa yanasababisha ongezeko la wagonjwa wa figo nchini pamoja na kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo shinikizo la damu ‘presha’ na kisukari.

Utafiti uliofanyika katika mikoa ya kaskazini umeonyesha asilimia saba ya Watanzania wanaugua ugonjwa huo huku wengine wakiishia kusafishwa damu mara tatu kwa wiki ‘diarysis’ na wachache wakipandikizwa figo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kongamano la madaktari wa figo leo Ijumaa, Novemba 15, 2019 Rais wa chama hicho, Dk Onesmo Kisanga amesema mbali na magonjwa hayo unywaji wa dawa kiholela hasa mitishamba imekuwa sababu kuu ya kuharibika kwa figo kwa walio wengi.

“Madawa haya ya kutibu magonjwa mbalimbali ya Kichina, kienyeji, yanayopunguza uzito yanaharibu figo, kwa maana hayana vipimo na mengi hayajathibitishwa, matumizi ya dawa za kutuliza maumivu pia ni sababu nyingine,” amesema.

Dk Kisanga amesema uzito uliopitiliza peke yake huwa sababu ya figo kuharibika, “uzito ni kitu muhimu, peke yake unaweza kuharibu figo licha ya kwamba unakaribiana na shinikizo la damu na kisukari. Nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara ni asilimia 10, Kenya ni asilimia saba, Uganda asilimia nane kwa hiyo Afrika Mashariki tupo kwenye asilimia saba na nane.”

Mmoja wa wanachama wa chama cha madaktari waliopo katika nchi za Diaspora, Dk Mubarak Mohammed amesema katika kitengo cha figo chochote duniani zaidi ya asilimia 50 ya wagonjwa waliopo kwenye matibabu ya diarysis (kusafishwa damu) ni wale wenye ugonjwa wa kisukari kwa hivyo yanaendana na magonjwa yasiyoambukiza.

Mwaka 2017 Tanzania ilianza rasmi kutoa matibabu ya upandikizaji figo na kwa kipindi cha miaka miwili sasa Tanzania imefanikiwa kuwapandikiza kiungo hicho jumla ya wagonjwa 51.

Tatizo hilo linakua wakati nchi ikiwa na madaktari bingwa wa figo 18, hata hivyo Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile alisema Serikali ipo kwenye mikakati ya kuhakikisha inasomesha wataalamu 100 kila mwaka kwa ufadhili.

Join our Newsletter