Uko hapa: NyumbaniInfosAfya2020 09 25Article 510421

Health News of Friday, 25 September 2020

Chanzo: HabariLeo

JKCI yachunguza 150 shinikizo la damu Temeke

JKCI yachunguza 150 shinikizo la damu Temeke

WATAALAMU wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamewafanyia uchunguzi watu 150 na kati ya hao, 37 wamekutwa na shinikizo la damu huku 19 kati ya waathirika walikuwa hawajijui hali zao.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa JKCI, Dk Samweli Rweyemamu alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari na kutoa tathmini kuhusu huduma ya uchunguzi na tiba waliyoitoa kwa wakazi wa Temeke, Septemba 18 na 23, mwaka huu katika Viwanja vya Mwembeyanga na Zakheem, kwenye Jukwaa la ‘One Stop Jawabu.’

“Mwamko na mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa, tumepima kisukari, uzito, shinikizo la damu na moyo kwa kutumia mashine ya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO), umeme wa moyo (Electrocardiography – ECG) na kutoa dawa kwa watu tuliowakuta na matatizo ya moyo,” alibainisha na kuongeza kuwa, watu hao ni wanawake, wanaume, vijana na watoto.

“Wawili tumewakuta tayari moyo umetanuka, mmoja ni binti mwenye umri wa miaka 18, tunahisi alipata maambukizi ya bakteria ambayo baadae huleta athari ya moyo kutanuka, tumempa rufaa kuja JKCI kwa uchunguzi zaidi,” alisema, na kwamba, watatu kati ya hao waliochunguzwa walikutwa wana kisukari hali inayoweza kuwaletea shida ya shinikizo la damu na kuathiri afya ya moyo kwa jumla.”

“Tumewaelekeza jinsi ya kuishi ili kuepukana na magonjwa haya, wazingatie mtindo bora wa maisha, ulaji bora, waepuke mafuta yasiyokidhi vigezo na tunahimiza mafuta ya mbegu ikiwamo alizeti… Tukiweza kuyatumia hayo na kuepuka zaidi yale yatokanayo na wanyama yanayosababisha mishipa ya damu kwenye moyo kuziba, tutaepuka magonjwa haya,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk Rweyemamu, miongoni mwa watu waliowaona wapo pia waliwakuta na shinikizo la juu la damu na wanatumia pombe kupita kiasi.

“Mmoja ametueleza anatumia chupa saba za bia kwa siku; tumemshauri ametuahidi anakwenda kupunguza kiasi hicho ili kulinda afya yake. Tumewashauri pia kupunguza matumizi ya chumvi nyingi kwenye chakula, kuepuka ulaji wa lambalamba, soda na kunenepa mwili,” alisema.

Dk Rweyemamu alisema kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani yanayofanyika Septemba 29, kila mwaka, wanahimiza Watanzania kuepuka matumizi ya chumvi kupita kiasi.

Aliwakaribisha Watanzania katika Viwanja vya Tanganyika Parkers Septemba 29, mwaka huu yatakapofanyika maadhimisho yanayoratibiwa na taasisi hiyo.

Wananchi waliopimwa katika banda hilo waliishukuru serikali wilayani Temeke kwa kuandaa jukwaa hilo lililowapa nafasi ya kupata huduma mbalimbali za muhimu kwa wakati mmoja.

Mkazi wa Temeke Mikoroshini, Tausi Yusuph alisema watu wengi katika jamii wana matatizo mbalimbali ya afya, lakini kutokana na uwezo mdogo wa kifedha walionao wanashindwa kwenda hospitali kwa matibabu.

Naye mkazi wa Buza, Isaya Ngunwa, alisema: “Nilikuwa na tatizo la msongo wa mawazo kwa muda mrefu na nilifikiria hali ile inaweza ikanisababishia magonjwa ya moyo. Leo nilipofika katika viwanja hivi kutafuta huduma ya cheti cha kuzaliwa nikasikia Taasisi ya Moyo wako hapa kwa ajili ya matibabu. Nashukuru baada ya kufanyiwa vipimo nimekutwa moyo wangu uko safi hauna tatizo.”

Join our Newsletter