Uko hapa: NyumbaniHabariHealth2021 10 27Article 566056

Habari za Afya of Wednesday, 27 October 2021

Chanzo: mwananchidigital

Jinsi dawa za hospitali zinavyochochea matumizi ya dawa za kulevya

Jinsi dawa za hospitali zinavyochochea matumizi ya dawa za kulevya Jinsi dawa za hospitali zinavyochochea matumizi ya dawa za kulevya

Matumizi mabaya ya tiba zenye asili ya kulevya zikiwamo dawa kama Tramadol, Morphine na Valium, yanatajwa kuwa moja ya visababishi vikuu kwa vijana wengi kuingia katika matumizi ya dawa za kulevya.

Hayo yamebainishwa na wataalamu wa tiba waliokuwa wakichangia hoja katika mjadala ulioandaliwa na mtandao wa Maendeleo Podcast hivi karibuni. Mjadala ulilenga kuangalia matumizi mabaya ya dawa hizo kama ilivyozoeleka kwa baahi ya watu nchini.

Imeelezwa wengi hutumia dawa hizo kuondolea maumivu na kutafutia usingizi, na wanapokuwa waraibu wa dawa hizo mwishowe hujikuta wakiingia kwenye hatua nyingine ya matumizi ya mihadarati.

Aidha, tafiti zimebaini kuwa waraibu wa dawa za kulevya wanaopokea tiba ya methadone, wameonekana kuwa na kiwango kikubwa cha dawa aina ya valium katika damu zao.

Hilo linaashiria kuwa wapo waliotumia dawa hizi za hospitali kwa wingi kabla ya kuwa waraibu wa mihadarati baadaye.

Mbunge wa viti maalum kupitia kundi la asasi za kiraia, Neema Lugangira alisema kuwa aliwahi kutembelea makazi ya kuhudumia waraibu wa mihadarati mkoani Tanga na kukutana na vijana wa kati ya miaka 19 hadi 21, ambao walimweleza kuwa waliingia kwenye mihadarati baada ya kuanza kutumia dawatiba hizo.

“Walisema tulianza kutumia dawa kama valium, tramadol tunakunywa na pombe tunazichanganya baadaye ikawa hatupati stimu, washkaji wakawa wanasema badilisha tumia hii na baadaye tukajikuta tumeingia katika matumizi ya dawa za kulevya,” alisema Lugangira, akimnukuu mmoja wa vijana hao.

Dawa tiba zinazolevya

Mkuu wa kItengo cha magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Omary Ubuguyu, alisema kuna makundi matatu ya dawa tiba zenye asili za kulevya, akitaja makundi hayo kuwa ni vipumbaza, vichangamshi na vileta njozi.

Alisema makundi hayo ya dawa huchepushwa sana ikiwemo Morphin ambazo hutumiwa zaidi na watu wenye saratani.

“Zamani dawa hizi zilipatikana Ocean Road pekee lakini kwa sasa vituo vingi vimepewa ruhusa ya kuzitoa. Kwa bahati mbaya waathirika wakubwa ni wanaotumia zile dawa za sicklecell (selimundu) yaani pethidine, lakini Tramadol zipo zinaathiri sana, ingawaje wanaoletwa wakiwa wameathirika kwa Tramadol hawazidi wale wa Pethidine,” alisema Dk Ubuguyu.

Akizungumzia dawa aina ya Valium Dk Ubuguyu ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya afya ya akili, alisema utafiti uliofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili baada ya kuwapima wagonjwa kwa kutumia ‘ methadone drug screening’ walibaini mtu mmoja kati ya wanne alikuwa na kiwango kikubwa cha valium katika damu.

“Tuliona walikuwa wanatumia na wengine hawajui kuhusu Valium tukahisi zinaongezwa kwenye heroin ili wauze zaidi,” alisema.

Hata hivyo, Dk Ubuguyu alisema bado kuna changamoto ya kupata takwimu kwa watumiaji wengine wa dawa zenye kulevya kwani hivi sasa nchini kuna matumizi mabaya ya pombe na sigara kupita kiasi na wazazi wengi wanatumia mbele ya watoto hivyo kuwafanya watoto kujiingiza huko mapema.

“Uraibu wa dawa hizi upo mkubwa sana, lakini tukiangalia namna gani watu wanapata hizo dawa, wengi wanaoanza kutumia wanapewa na ndugu na asilimia 90 wananunua kutoka kwa watoa huduma,” alisema.

Alisema dawa hizi zimekua zikiuzwa katika maduka ya dawa ya mtaani kwa kuwa wauzaji wengi hawana muda wa kumsikiliza mgonjwa, hivyo anapoelezwa kuwa mtu ana maumivu anatoa dawa yoyote anayoona inamfaa.

“Kuna sababu nyingi watu kuingia kwenye uraibu wa dawa za kulevya, lakini chanzo watu hawaoni, tunazungumza kwamba aliachwa, alifukuzwa kazi kumbe kuna mahala alipoanzia. Watu wanabakwa, wengine wana dalili za magonjwa wanapewa hizo dawa,” alisema Dk Ubuguyu.

Wanaweza kupona

Daktari bingwa wa magonjwa ya afya ya akili Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Iddi Haruna, alisema aliyeathirika na dawa tiba zenye kulevya anaweza kutibiwa na kupona kupitia dawa za methadone.

“Inawezeka kumsaidia mtu kuacha kabisa matumizi ya dawa hizi na kurudisha utu wake na kuweza kurudisha maisha yake ya kila siku. Dawa tunazozitumia ni methadone hivyo wanatumia dawa hizo na kuna nyingine za vidonge,” alisema.

Dk Haruna alisema mpaka sasa kuna wagonjwa zaidi ya 10,000 ambao wanatibiwa kote nchini na wachache wana uraibu wa dawa tiba ambao pia wanatibiwa na methadone.

Msajili wa Baraza la Famasia nchini, Elizabeth Shekalaghe alisema katika utoaji na uandikaji wa dawa hizi eneo la sheria, usimamizi unafanyika chini ya sheria ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), kwani wao wanaangalia zaidi kudhibiti uingizwaji na kwa mujibum wa sheria yao wametunga kanuni tisa zinazoratibu shughuli hiyo.

Alisema watoa huduma wa afya wanahusika sana na uchepushwaji wa hizi dawa kwa kudhamiria na wengine kutodhamiria.

“Tulifanya ukaguzi pale Ocean Road wagonjwa wanaotumia morfine, ndugu wa mgonjwa anakuja pale anapatiwa dawa za mgonjwa kwa siku 14 kabla ya siku hazijaisha anakuja tena kuchukua nyingine, lakini hakuna ufuatiliaji hili ni kosa,” alisema Shekalaghe.

Alisema kisheria TMDA haihusiki moja kwa moja iwapo imeshathibitisha ubora. Hospitali zinatakiwa kuomba kupitia Bohari ya Dawa (MSD) lakini mara zinapofika hospitali wengi huzichepusha.

“Nchi za wenzetu hizi dawa haziuzwi ovyo lakini kwetu hizi valium zinauzwa kwa watu ambao hawastahili; anapewa,” alisema Shekalaghe.