Uko hapa: NyumbaniHabariHealth2021 09 14Article 557338

Habari za Afya of Tuesday, 14 September 2021

Chanzo: Mwananchi

MUHAS yatekeleza tafiti 115 ikiwemo Uviko-19

Muhas Muhas

Jumla ya tafiti 115 zinaendelea kufanywa katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) zikijikita katika maradhi ya kuambukiza, yasiyoambukiza pamoja na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Uviko-19.

Miradi hiyo inayotekelezwa na Muhas pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ni sehemu ya utekelezaji wa afua mbalimbali kudhibiti magonjwa kama Virusi vya Ukimwi, Malaria, Kifua Kikuu na yale yasiyoambukiza yaliyotajwa kuongezeka kwa kasi.

Hayo yamesemwa Septemba 13, 2021 na Mkurugenzi wa tafiti na machapisho wa Muhas, Profesa Bruno Sanguya, wakati Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dk Donald Wright alipofanya ziara chuoni hapo kwa ajili ya kuangalia namna miradi ya kiutafiti 35 iliyofadhiliwa na ubalozi huo inavyotekelezwa.

Amesema jumla ya miradi mikubwa 115 inaendelea kufanyika na iliyofadhiliwa na Serikali ya Marekani ni 35 ni sawa na asilimia 30.4 ya miradi iliyopo chuoni apo inayotafiti namna ya kudhibiti magojwa mbalimbali.

Ametaja magonjwa hayo kuwa ni pamoja na ya milipuko, maambukizi kama malaria na kifua kikuu, yasiyoambukiza kama saratani, moyo na magonjwa ya ajali pamoja na mifumo ya afya na kuboresha ujuzi mbalimbali ya watendaji wa afya nchini.

Ameeleza kuwa lengo la miradi hiyo ni kutatua changamoto mbalimbali za Watanzania na kuboresha mifumo ya afya, ujuzi na weledi wa wataalamu wa afya.

‘‘Maendeleo yaliyopatikana kutokana na miradi hiyo yamesaidia kubadilisha miongozo ya baadhi ya matibabu ya VVU na kliniki ya kwanza ya kutoa dawa ya kufubaza ukimwi zilianzishwa katika chuo cha muhimbili na havard nchini Marekani,” amesema Sanguya.

Sunguya amesema kati ya tafiti zilizofadhiliwa na Serikali ya Marekani, ilianza kufanywa miongo mitatu iliyopita, “Miradi hii ina thamani ya Dola za Marekani milioni 11 sawa na Sh25 bilioni na inaanzia Dola 15,000 mpaka 300,000 kwa utafiti mmoja.”

Akizungumza mara baada ya ziara hiyo Balozi Wright amesema, “Taasisi ya utafiti leo imefanya mrejesho wa miradi ya utafiti iliyofadhiliwa na Ubalozi wa Marekani kwa ajili ya kuboresha afya, katika kazi za tafiti tumefanya upande wa VVU, seli mundu, kifua kikuu na magonjwa mengine, tunaagiza tafiti hizi zifanyike kwa weledi na ziwe na manufaa kwa Watanzania.”