Uko hapa: NyumbaniHabariAfya2021 06 11Article 542176

xxxxxxxxxxx of Friday, 11 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

TBS yafunda mawakala,wafanyabiashara sumukuvu

MAWAKALA wa Forodha na wafanyabiashara wa mahindi na nafaka nyingine wamepatiwa mafunzo kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu sumukuvu, visababishi, madhara yake na namna ya kuhifadhi mazao.

Maeneo hayo ni kuhusu taratibu za kupata ushauri wa kitaalamu wakati wa kusafirisha shehena nje ya nchi, taarifa za fursa za masoko na upatikanaji wa taarifa zake pamoja na taratibu za kupata vibali vya kusafirisha mazao kwenda nje ya nchi.

Mafunzo hayo yaliyotolea kwa siku tatu zilizopita yametolewa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika mipaka iliyopo kanda ya Kaskazini ambayo ni Horohoro- Tanga, Holili Kilimanjaro na Namanga-Arusha ili kuwawezesha mawakala wa forodha na wafanyabiashara kuondokana na changamoto za shehena zao kukataliwa na nchi walizokuwa wakipeleka biashara zao.

Ofisa Masoko wa TBS, Rhoda Mayugu alisema "Mawakala wa forodha na wafanyabiashara wa mahindi na nafaka nyingine walikuwa wakikabiliana na changamoto ya shehena zao kukataliwa kuingia kwenye nchi wanakopeleka shehena kwa sababu ya kuwa hafifu na kwa kuwa hawakuwa na taarifa yoyote ya maabara inayoonesha shehena zao zilipimwa na kukidhi viwango na hiyo ilifanya baadhi ya wafanyabiashara hao kupata hasara".

Alisema wafanyabiashara na mawakala wa forodha wanatakiwa kuhakikisha mahindi na nafaka wanazonunua zimeandaliwa katika hali ya usafi, lakini pia nafaka hizo zichambuliwe na zile zilizooza, zenye uvundo na zilizonyauka ambazo hata kwa macho zikiangaliwa huonekana kuwa dhaifu basi ziondolewe.

Alisema wanapoona dalili hizo waelewe kwamba uwezekano wa kuwa na sumukuvu ni mkubwa zaidi. Hata hivyo, alisisitiza kwamba lazima waelewe kwamba sumu kuvu haionekani kwa macho, bali kwa vipimo vya maabara.

Alisema kwa upande wa kiafya yapo madhara ya muda mfupi ambayo ni kuumwa tumbo, manjano, kutapika na degedege, huku madhara ya muda mrefu yakiwa ni kansa ya ini, kupungua kwa kinga mwilini, udumavu wa watoto na hata kupoteza maisha.

Kwa mujibu wa Mayugu, wafanyabiashara na mawakala wa forodha wanatakiwa kutumia msaada wa kitaalamu unaotolewa na TBS wakati wa ufarishaji wa shehena nje ya nchi.

Join our Newsletter