Uko hapa: NyumbaniHabariHealthBima ya Afya ya Taifa

Bima ya Afya Tanzania

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umepanua wigo wake wa mafao kwa kuanzisha vifurushi ili kuwapa fursa wananchi wengi zaidi kujiunga na kunufaika na huduma za bima ya afya nchini. Vifurushi hivi vinatoa fursa kwa mtu mmoja mmoja, familia au makundi mbalimbali ya wananchi kujiunga na bima ya afya kwa kuzingatia vigezo na masharti yaliyowekwa na Mfuko.

Aidha, uanzishwaji wa mpango wa vifurushi unawawezesha wananchi wengi zaidi kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha. Hivyo, kutokana na maboresho haya, wananchi wana fursa ya kukabiliana na gharama za matibabu ambazo zimekua zikiongezeka siku hadi siku na wakati mwingine kushindwa kuzimudu na kuangukia katika janga la umaskini au kifo.

MADHUMUNI YA VIFURUSHI VYA BIMA YA AFYA

 • Kutoa fursa kwa wananchi katika sekta isiyo rasmi wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea ili kujisajili na kunufaika na huduma za matibabu.
 • Kutoa fursa kwa wananchi wengi zaidi kupata huduma za matibabu kwa uhitaji wa huduma na ukubwa wa familia;

KIFURUSHI CHA NAJALI AFYA

Kifurushi hiki ni mahsusi kwa mwananchi mwenye kujali afya yake kwa kujiunga na bima ya afya na kuwa na uhakika wa kupata huduma mwaka mzima. Mwanachama wa kifurushi cha NAJALI AFYA atapatiwa kadi ya matibabu ya Mfuko ambayo ataitumia kupata huduma katika vituo zaidi ya 7,000 vilivyosajiliwa na Mfuko ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kifurushi hiki pia kinatoa fursa ya kusajili mtu zaidi ya mmoja katika familia kulingana na mahitaji ya mchangiaji. Kupitia kifurushi hiki, Mfuko unawahakikishia wanufaika kupata huduma bora za matibabu kwa gharama nafuu zinazopatikana kupitia mtandao mpana wa vituo vya afya vilivyosajiliwa nchi nzima ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

MWANACHAMA WA NAJALI AFYA ATANUFAIKA NA NINI?

Mwanachama wa Mfuko kupitia kifurushi cha NAJALI AFYA atapata huduma katika vituo vyote vya umma, binafsi na vya mashirika ya dini vilivyosajiliwa na Mfuko nchi nzima hadi ngazi ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Mwanachama atahitajika kuwa na barua ya rufaa ili kupata huduma katika ngazi ya Hospitali za Kanda na Hospitali ya Rufaa ya Taifa. Katika ngazi zote za vituo, mwanachama wa NAJALI AFYA atanufaika na mafao yafuatayo:-

 1. Kulipiwa ada ya kujiandikisha na kumuona daktari,
 2. Kulipiwa huduma ya kulazwa hadi siku 30 kwa mwaka kwa kila mwanafamilia,
 3. Kulipiwa dawa zilizosajiliwa na kuruhusiwa hadi ngazi ya kituo cha afya,
 4. Kulipiwa gharama za huduma za kinywa na meno kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa,
 5. Kulipiwa gharama za huduma za upasuaji mdogo zaidi ya aina 27 na za upasuaji mkubwa zaidi ya aina 14,
 6. Kuanza kulipiwa huduma za uzazi baada ya kuchangia kwa miaka miwili (2) kwa kuzingatia vigezo na masharti yaliyowekwa,
 7. Kulipiwa huduma za vipimo zaidi ya aina 162 vikiwemo Ultrasound, X-Ray, ECHO na EEG.

KIFURUSHI CHA WEKEZA AFYA

Kifurushi cha WEKEZA AFYA ni mahsusi kwa mwananchi anayehitaji kuwekeza katika hali yake ya kiafya au pamoja na afya ya familia yake kwa lengo la kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu pale anapozihitaji. Mwanachama wa kifurushi cha WEKEZA AFYA atapatiwa kadi ya matibabu ya Mfuko ambayo ataitumia kupata huduma katika vituo zaidi ya 7,000 vilivyosajiliwa na Mfuko ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kifurushi hiki pia kinatoa fursa ya kusajili mtu zaidi ya mmoja katika familia kuendana na mahitaji ya mchangiaji. Kupitia kifurushi hiki, Mfuko unawahakikishia wanufaika kupata huduma bora za matibabu kwa gharama nafuu zinazopatikana kupitia mtandao mpana wa vituo vya afya vilivyosajiliwa nchi nzima.

 

MWANACHAMA WA WEKEZA AFYA ATANUFAIKA NA NINI?

Mwanachama wa Mfuko kupitia kifurushi cha WEKEZA AFYA atapata huduma katika vituo vyote vya umma, binafsi na vya mashirika ya dini vilivyosajiliwa na Mfuko nchi nzima hadi ngazi ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Mwanachama atahitaji barua ya rufaa ili kupata huduma katika ngazi ya Hospitali za Kanda na Hospitali ya Rufaa ya Taifa. Katika ngazi zote za vituo, mwanachama wa WEKEZA AFYA atanufaika na mafao yafuatayo:-

 1. Kulipiwa ada ya kujiandikisha na kumuona daktari,
 2. Kulipiwa huduma ya kulazwa hadi siku 45 kwa mwaka kwa kila mnufaika,
 3. Kulipiwa dawa zilizosajiliwa na kuruhusiwa hadi ngazi ya hospitali ya wilaya,
 4. Kulipiwa huduma za kinywa na meno kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa,
 5. Kupata zaidi ya aina 30 za huduma za upasuaji mdogo na zaidi ya aina 36 za upasuaji mkubwa,
 6. Kuanza kulipiwa huduma za uzazi baada ya mwaka mmoja (1) wa kuchangia kwa kuzingatia vigezo na masharti yaliyowekwa,
 7. Kupata zaidi ya aina 197 ya huduma za vipimo vikiwemo Ultrasound, X-Ray, ECHO na EEG.

KIFURUSHI CHA TIMIZA AFYA

Kifurushi cha TIMIZA AFYA ni mahsusi kwa mwananchi aliyefikia ndoto yake ya kupata kitita kipana cha huduma za matibabu kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa mwaka. Mwanachama wa kifurushi cha TIMIZA AFYA atapatiwa kadi ya matibabu ya Mfuko ambayo ataitumia kupata huduma katika vituo zaidi ya 7,000 vilivyosajiliwa na Mfuko ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kifurushi hiki kinatoa fursa ya kusajili mtu zaidi ya mmoja katika familia kulingana na mahitaji ya mchangiaji. Kupitia kifurushi hiki, Mfuko unawahakikishia wanufaika kupata huduma bora za matibabu kwa gharama nafuu zinazopatikana kupitia mtandao mpana wa vituo vya afya vilivyosajiliwa nchi nzima.

MWANACHAMA WA TIMIZA AFYA ATANUFAIKA NA NINI?

Mwanachama wa Mfuko kupitia kifurushi cha TIMIZA AFYA atapata huduma katika vituo vyote vya umma, binafsi na vya mashirika ya dini vilivyosajiliwa na Mfuko nchi nzima hadi ngazi ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Mwanachama atahitaji barua ya rufaa ili kupata huduma katika ngazi ya Hospitali za Kanda na Hospitali ya Rufaa ya Taifa. Katika ngazi zote za vituo, mwanachama wa TIMIZA AFYA atanufaika na mafao yafuatayo:-

 1. Kulipiwa ada ya kumuona daktari.
 2. Kulipiwa huduma ya kulazwa hadi siku 60 kwa mwaka,
 3. Kulipiwa dawa zilizosajiliwa na kuruhusiwa hadi ngazi ya hospitali ya mkoa
 4. Kulipiwa huduma za kinywa na meno kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa,
 5. Kulipiwa zaidi ya aina 50 ya huduma za upasuaji mdogo na zaidi ya aina 80 za upasuaji mkubwa,
 6. Kuanza kulipiwa huduma za uzazi baada ya mwaka mmoja (1) wa kuchangia,
 7. Kulipiwa zaidi ya aina 223 ya huduma za vipimo vikiwemo CT SCAN, MRI, Ultrasound, X-Ray, ECHO na EEG kwa kuzingatia vigezo na masharti yaliyowekwa.

JINSI YA KUJISAJILI NA VIFURUSHI HIVI NA MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA

 • Mwanachama anatakiwa kujaza fomu ya kujiunga ambayo inapatikana katika ofisi zote za Mfuko nchi nzima, au kupitia katika tovuti ya Mfuko www.nhif.or.tz.au kupitia katika mfumo wa kieletroniki;
 • Mwanachama atapewa namba ya malipo (control number) ambayo ataitumia kufanya malipo kupitia benki au mitandao ya simu.
 • Mwanachama anatakiwa kuwa na kitambulisho kimojawapo kati ya kitambulisho cha Taifa, kitambulisho cha mpiga kura, leseni ya udereva au hati ya kusafiria.
 • Mwanachama atafanya malipo yote kwa mkupuo au kwa awamu kupitia utaratibu maalum wa benki.
 • Mwanachama atapaswa kuwa na picha moja ya rangi ya ukubwa wa passport size.
 • Mwanachama atapatiwa kitambulisho cha matibabu na kuanza kupata huduma zilizoainishwa katika kifurushi alichokichagua kwa kuzingatia vigezo na masharti yaliyowekwa.
 • Mwanachama anayemwandikisha mwenza atahitaji kuambatanisha picha moja ya mwenza ya rangi, nakala ya cheti cha ndoa, pamoja na kitambulisho kimojawapo cha mwenza kati ya kitambulisho cha Taifa, kitambulisho cha mpiga kura, hati ya kusafiria au leseni ya udereva.
 • Mwanachama anayemwandikisha mtoto kama mtegemezi atahitajika kuambatanisha picha ya mtoto na nakala ya cheti cha kuzaliwa cha mtoto. Tangazo la kuzaliwa linaweza kuwasilishwa kama mbadala wa cheti cha kuzaliwa endapo mtoto ana umri wa chini ya miezi 6.

Kwa maelezo zaidi fika ofisi yoyote ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya au wasiliana nasi kupitia simu ya huduma kwa wateja bila malipo 0800 110063.