Uko hapa: NyumbaniHabariHealthTakwimu za Afya

Takwimu za Afya

HALI YA HUDUMA ZA AFYA NCHINI (1990-2007)


Huduma za afya nchini zimeendelea kutolewa kwa kiwango cha kuridhisha kutokana na mabadiliko endelevu yanayofanyika katika Sekta ya afya kwa lengo la kuleta uwiano katika upatikanaji wa huduma bora za afya mijini na vijijini. Kiasi cha asilimia themanini ya watanzania kufikia miaka ya tisini, tayari wana fursa ya kupatiwa huduma katika umbali wa kilomita kumi. Hata hivyo, hali ya afya ya wananchi wengi imeendelea kuwa ya wastani kutokana na changamoto zinazoendelea kujitokeza kabla na baada ya uhuru katika mfumo wa huduma za afya. Hali hii imesababisha kupungua kwa kasi ya kufikia malengo yaliyotarajiwa na serikali.


2.1 Huduma za Afya Kabla na Baada ya Uhuru


Kabla ya Uhuru, huduma za afya nchini zilikuwa zinatolewa zaidi kwenye maeneo ya shughuli za kiuchumi kama miji na mashamba makubwa. Baada ya uhuru, Serikali iliweka msukumo zaidi katika kupanua huduma za afya ili kuwafikia wananchi wengi hasa walioko vijijini. Ili kufanikisha azma hii, Serikali iliweka mfumo wa rufaa wa huduma za afya. Kwa mfumo huu, zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, hospitali za mikoa, maalum, kanda na taifa zilianzishwa.


Aidha, Serikali ilihamasisha na kuwezesha hospitali za mashirika ya kidini kushirikiana nayo kutoa huduma kwa wananchi. Kipaumbele kilikuwa katika utoaji wa huduma za tiba zaidi kuliko kinga.
Katika kipindi chote hicho hadi miaka ya tisini, huduma za afya zilitolewa bila malipo. Kutokana na hali mbaya ya kiuchumi, Serikali ilianzisha mabadiliko katika Sekta ya Afya ikiwa ni pamoja na ushirikishwaji wa wananchi katika kuchangia gharama za huduma za afya mwaka 1993. Hata hivyo, makundi maalum ambayo ni; wazee wasiojiweza, watu wenye ulemavu, watoto wenye umri chini ya miaka mitano na wanawake wajawazito hawachangii. Serikali imeendelea kuimarisha huduma za afya kwa kushirikisha sekta binafsi.


Hali ya afya ya wananchi wa Tanzania imeendelea kuboreshwa baada ya Uhuru. Hata hivyo kuna baadhi ya makundi ya wananchi ambayo yanahitaji kupewa kipaumbele ili kuendelea kuboresha afya zao kwa kuimarisha mfumo wa utoaji huduma. Wastani wa maisha ya Mtanzania ni miaka 51, yaani miaka 50 kwa wanaume na 52 kwa wanawake. Juhudi zilizopo zitaendelea kuboresha wastani huo.


Watanzania wanakabiliwa na magonjwa makubwa ya kuambukiza ambayo ni UKIMWI, malaria na kifua kikuu. Aidha, afya ya uzazi na mtoto bado hairidhishi. Vile vile, magonjwa yasiyo ya kuambukiza yameanza kujitokeza kwa wingi kutokana na mabadiliko ya mienendo na tabia ya kuishi. Magonjwa haya ni kama saratani, shinikizo la damu, kiharusi na kisukari.


2.2 Utekelezaji wa Sera ya mwaka 1990


Sera ya mwaka tisini ilitoa kipaumbele katika utoaji huduma za kinga, tiba, uhamasishaji na utengemao. Huduma hizi zilitolewa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Katika kutoa huduma za kinga, Serikali imeelekeza mapambano yake katika kutokomeza magonjwa yanayosababisha vifo vya watoto wenye umri chini ya mwaka mmoja na miaka mitano na wanawake wajawazito. Katika utoaji wa huduma hizo, msisitizo umeelekezwa katika utoaji wa chanjo, elimu ya afya na kuruhusu upatikanaji huduma hizo bila malipo. Aidha, Serikali inaendelea na jitihada za kudhibiti na kuzuia magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.


Huduma za tiba zimeendelea kutolewa katika ngazi zote. Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa; dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi vinapatikana na kusambazwa katika vituo vyote vya kutolea huduma. Serikali pia, kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya katika ngazi zote. Katika kuboresha huduma, mafunzo mbalimbali yamekuwa yakitolewa kwa watumishi kufuatana na taaluma zao na mahitaji. Vilevile, Serikali imeendelea kutoa huduma kwa makundi maalum. Aidha, jamii imeendelea kushirikishwa kikamilifu katika kutambua, kupanga na kutekeleza mipango ya afya ikiwemo usafi wa mazingira na usafi wa mtu binafsi.


Serikali imeendelea kupambana na janga la UKIMWI na magonjwa mengine ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza, kwa kuanzisha na kutekeleza mikakati maalum ya kuelimisha jamii ili kupunguza maambukizi mapya, kujikinga na kuchukua hatua ya matibabu sahihi mapema. Serikali pia, imekuwa inaendeleza huduma za utengemao kwa kutoa vifaa vya kujimudu, elimu ya kuwawezesha watu wenye ulemavu kujitegemea na kutoa huduma za tiba na kinga.

Mafanikio


Utekelezaji wa mipango na mikakati ya huduma za afya na ustawi wa jamii umeleta mafanikio katika maeneo mbalimbali hapa nchini kama ifuatavyo: -

 1. Wananchi wameelimishwa juu ya umuhimu wa huduma za afya na kuhamasishwa kutumia huduma hizo, hali ambayo imechochea mahitaji makubwa kwa kila ngazi na kila sehemu ya nchi;
 2. Ushirikishwaji wa wananchi katika huduma za afya umewezesha kuongezeka kwa vituo vya Serikali na binafsi na kuchochea mahitaji makubwa ya watumishi na kupanua vyuo ili kuongeza idadi ya wanaojiunga;

 3. Uwezo, uzoefu na mifumo ya kutoa huduma ya mama na mtoto na ya kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza yakiwemo maradhi makuu kama vile malaria, kifua kikuu na UKIMWI umejengwa na kuimarika;

 4. Sheria mbalimbali zimetungwa na nyingine kufanyiwa mapitio kutokana (iv) na mabadiliko katika Sekta ya Afya kwa lengo la kuboresha usimamizi wa huduma za Afya nchini na kulinda afya za wananchi.

Upungufu


Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, katika utekelezaji wa sera ya 1990 bado kuna upungufu katika kufikia malengo yaliyokusudiwa kama ifuatavyo: -

 1. Sera hiyo haikuweza kuweka mifumo ya kutosheleza mahitaji ya huduma za afya kwa ngazi mbalimbali katika maeneo mengi ya nchi yetu, kwa mfano usambazaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba;

 2. Uhaba wa wataalam wa kada mbalimbali, vifaa, dawa, vitendanishi na vifaa tiba katika sekta ya Afya;

 3. Kukosekana kwa vivutio maalum kwa wataalam, vya kuwahamasisha kubaki katika vituo vya huduma na maeneo mbalimbali ya nchi;

 4. Changamoto ya maendeleo na mabadiliko ya tabia na mwenendo wa maisha imebadili sura ya magonjwa. Aidha, hali hii imesababisha kuanza kujitokeza kwa magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza na yanayotokana na ajali na majanga, ambayo kwa huduma zilizopo haziwezi kukidhi;

 5. Wananchi wengi wanaendelea kusumbuliwa na magonjwa ambayo hayakupewa umuhimu, kwa mfano matende, ngirimaji, kichocho na vikope. Wakati huo huo, magonjwa mapya yameanza kujitokeza kwa nguvu, kwa mfumo wa milipuko, mfano; homa ya bonde la ufa, homa ya mafua ya ndege ambapo mfumo wa huduma uliopo haukidhi mahitaji;

 6. Baadhi ya magonjwa yaliyojitokeza kwa mfano; UKIMWI, yameibua mahitaji maalum katika dhana ya lishe bora na huduma za utengemao.

Changamoto
Changamoto ambazo sekta ya afya inakabiliana nazo katika kutoa huduma ni kama ifuatavyo:

 1. Namna ya kuongeza watumishi, ili kukidhi mahitaji ya sekta ya afya katika ngazi zote;
 2. Jinsi ya kuongeza bajeti ya sekta ya afya katika ngazi zote hadi kufikia kiwango kisichopungua asilimia 15 ya bajeti yote ya Serikali, kama ilivyopitishwa na Azimio la Abuja;
 3. Kasi ya maambukizi mapya na athari za UKIMWI katika jamii ikizingatiwa kuwa asilimia 7 ya Watanzania wameambukizwa virusi vya UKIMWI;
 4. Kuhakikisha kuwa vifo vya watoto wachanga, wenye umri chini ya mwaka mmoja, vinapungua zaidi ya 68 kwa watoto 1000 waliozaliwa hai;
 5. Kupunguza viwango vya utapiamlo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano;
 6. Kupunguza viwango vya vifo vya wanawake vinavyotokana na uzazi;
 7. Kupunguza ongezeko kubwa la watoto yatima na walio katika mazingira magumu;
 8. Kupandisha ari ya utendaji kazi wa watumishi wa sekta ya afya kutokana na mishahara midogo, ukosefu wa motisha na upungufu wa vitendea kazi;
 9. Kudhibiti athari za utandawazi na kasi ya mabadiliko ya teknolojia ya sayansi ya afya;
 10. Kudhibiti ongezeko kubwa la bei za dawa, vifaa na vifaa tiba;
 11. Kudhibiti ongezeko la vimelea vya magonjwa kuwa sugu kwa dawa zinazotumika;
 12. Kudhibiti ongezeko la magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza yakiwemo kisukari, magonjwa ya moyo, saratani na ajali;
 13. Kuzuia kuibuka kwa magonjwa ya kuambukiza yaliyoonekana kudhibitiwa huko nyuma;
 14. Kuongeza ushiriki wa wananchi katika usafi wa mazingira, kama njia ya udhibiti wa magonjwa ya kuambukizwa;
 15. Kupambana na kuzuka kwa magonjwa mapya duniani kama vile; ugonjwa wa Kichaa cha ng’ombe unaoathiri binadamu, homa ya Mafua ya ndege, Ebola na SARS;
 16. Kukidhi matarajio ya wananchi kwa kuwa na huduma bora za afya;
 17. Udhibiti wa vitendo vya rushwa kwa baadhi ya watumishi wa afya na ubinafsi katika utoaji wa huduma;
 18. Utendaji na uwajibikaji unaogongana katika ngazi mbalimbali za kutolea huduma na maamuzi;
 19. Mfumo thabiti wa kuhudumia wastaafu, wategemezi wao na wazee;
 20. Kupunguza utegemezi wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kutoka nje ya nchi;
 21. Mfumo madhubuti na endelevu wa kuendeleza watumishi katika sekta ya afya;
 22. Usimamizi bora na endelevu wa Sekta binafsi zinazoongezeka kwa kasi nchini;
 23. Kuongezeka kwa ugonjwa wa malaria na usugu wa vimelea vya ugonjwa huo ambao unachangia zaidi ya asilimia 40 ya wagonjwa wote wa nje na asilimia 38 kwa wagonjwa wote wanaolazwa;

UMUHIMU WA SERA
Sera ya mwaka 1990, ambayo imekuwa ikitumiwa hadi sasa haikidhi mahitaji ya sekta ya afya kutokana na mabadiliko yaliyojitokeza na yanayoendelea kujitokeza ya kiuchumi na kijamii, kuongezeka kwa magonjwa mapya na yanayojirudia kama; UKIMWI na Kifua Kikuu, uanzishaji wa utaratibu wa mfumo wa wananchi kuchangia huduma za afya na kuanzishwa kwa utaratibu wa wananchi kuwa na madaraka ya kushiriki katika kutoa maamuzi na kumiliki raslimali za sekta ya afya. Sababu nyingine zilizochangia Sera ya mwaka 1990 kutokidhi mahitaji ya sasa na wakati ujao, ni pamoja na kuwepo kwa maendeleo mapya ya sayansi na teknolojia, utekelezaji wa dira na mikakati ya taifa na utekelezaji wa mikataba ya kimataifa ikiwemo Malengo ya Milenia.
Sera hii iliyopitiwa, inazingatia masuala yote yaliyotajwa hapo juu na pia, ni mwendelezo wa utekelezaji wa malengo yalioanishwa katika Sera ya mwaka 1990. Aidha, Sera hii ni muhimu kwani inatoa maelekezo ya jinsi ya kuanzisha, kuendesha na kutoa huduma za afya nchini kwa lengo la kuhakikisha kwamba kila mtu anapata huduma za afya zilizo bora na zenye uwiano na haki. Serikali inatambua kwamba wananchi walio na afya bora ni raslimali kubwa katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini. Aidha, sera inalenga katika kuwezesha ushirikishwaji wa wananchi na wadau katika utoaji wa huduma za afya.