Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2020 12 08Article 517667

Siasa of Tuesday, 8 December 2020

Chanzo: HabariLeo

Asas: Wanaochafua viongozi kwa Whatsapp wakamatwe

Asas: Wanaochafua viongozi kwa Whatsapp wakamatwe

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Salim Asas amekiomba chama hicho kuanza kuchukua hatua kali kwa wanachama wake wanaotumia mitandao mbalimbali ya kijamii yakiwemo makundi ya whatsapp kuchafua viongozi wao mbalimbali.

“Baadhi ya wanachama walioko katika mitandao hiyo, wamesahau kanuni na taratibu za chama chetu kwa kuifanya mitandao hiyo kama majukwaa rasmi ya kuwajadili na kuwachafua baadhi ya viongozi,” alisema.

Aliyasema hayo juzi wakati akifungua kikao maalumu cha Halmashauri Kuu ya CCM ya Wilaya ya Mufindi, iliyokutana mjini Mafinga kupongezana kwa kuongoza mkoani Iringa, kwa kumpa kura nyingi za urais Rais John Magufuli katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu na kushinda viti vyote vitatu vya ubunge na kata zote 36 za udiwani katika wilaya hiyo.

Asas alisema wakati vikao vya maadili vya chama hicho, vikianza kujipanga kuwajadili baadhi ya wanachama wake wanaotuhumiwa kwa usaliti wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, visisahau kuanza kukusanya taarifa za wanachama wanaochafua viongozi wao mitandaoni na kuchukua hatua stahiki.

Katika mitandao hiyo, ikiwemo iliyoanzishwa na baadhi ya wana CCM imekuwa ni jambo la kawaida kwa baadhi ya wanachama, kuanzisha malumbano na mapambano ya maneno ya kashfa dhidi ya viongozi wao bila kuchukuliwa hatua zozote.

Akitoa mfano wa mitandao hiyo, Asas alisema baadhi yake ni ile iliyoanzishwa na baadhi ya wanaCCM wa mjini Iringa, ambayo awali ilidhaniwa kazi yake ni kusaidia kukijenga chama hicho kwa kunadi sera zake na utekelezaji wa Ilani ya chama hicho.

Kwa kuwa chama kimekuwa kimya dhidi ya wanachama hao, baadhi yao wanaendelea kuvimba vichwa, wakiamini chama na viongozi wanaokashifiwa wanawaogopa.

“Hata mimi nimekuwa nikikatishwa sana tamaa na wana CCM hao, katika makundi yao hawafurahi kuona natimiza wajibu wangu kama kiongozi wa chama hiki, kwa kutoa msaada wa hali na mali kuhakikisha chama chetu kinazidi kuimarika,” alisema.

Katika mazingira ya kusikitisha, Asas alisema baadhi ya wanaCCM hao wamekuwa wakishirikiana na baadhi ya viongozi na wafuasi wa vyama mbalimbali vya upinzani na wakati mwingine wakitumia mbinu hiyo kuwatisha ili wajipatie fedha.

Ili kuwaonesha kwamba chama kipo juu yao na kwamba watu hao hawaogopwi Asas alisema: “Muda umefika wa kuanza kuchukua hatua na kwa kufanya hivyo wana CCM wataanza kuzingatia kanuni, taratibu na katiba katika kushughulikia mambo yao, zikiwemo hisia zao zozote tofauti dhidi ya viongozi au wanachama wenzao.”

Akiipongeza CCM wilaya ya Mufindi yenye kata 36 kwa kumpa kura nyingi Dk Magufuli, Asas alisema atatoa zawadi ya Sh 100,000 kwa kila kata.

Aliahidi kuwa Kata ya Kiyowela iliyoongoza kwa kumpa Rais Magufuli asilimia 100 ya kura zote ataijengea ofisi ya mfano.

“Mufindi hamjawahi kuiangusha CCM, ni wilaya tunayojivunia kwa kuzoa kura nyingi katika kila chaguzi. Na mimi nimeona niwaunge mkono kwa kazi nzuri mliyofanya kwa kutoa zawadi hii kidogo,” alisema baada ya chama wilayani humo kutoa vyeti na zawadi ya Sh 200,000 kwa kata tatu zilizoongoza zaidi kwa kumpa kura Magufuli.

Akimshukuru Asas kwa msaada wake ulifanya pia Mbunge wa Mufindi Kusini, David Kihenzile na Mbunge Mufindi Kaskazini, Exaud Kigahe ambaye pia ni Naibu Waziri mteule wa Viwanda na Biashara kwa pamoja kuahidi nao kutoa zawadi ya Sh 100,000 kwa kila kata.

Awali Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mufindi, Daudi Yasin alimpongeza Rais John Magufuli kwa ushindi mkubwa alioupata na akaahidi chama kumsaidia kusimamia utekelezaji wa Ilani yake.

Akizungumzia wasaliti waliobainika wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba, Yasin alisema vikao vya maadili ya chama, vitakutana hivi karibuni kwa lengo la kuwajadili na kuwachukulia hatua wanachama nane wanaotuhumiwa kwa makossa hayo.

Join our Newsletter