Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2020 11 30Article 516647

xxxxxxxxxxx of Monday, 30 November 2020

Chanzo: habarileo.co.tz

Bashiru akaribisha akina Mdee CCM

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally amewakaribisha kujiunga kwenye chama hicho, wabunge wa viti maalumu kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliofukuzwa uanachama akiwemo Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (BAWACHA), Halima Mdee na wenzake 18.

Alisema hayo jana mjini hapa wakati akifungua semina ya wajumbe wa sekretarieti ya taifa ya halmashauri kuu na kamati ya utekelezaji wa jumuiya za chama.

Alisema wabunge wa upinzani wapewe haki ya uwakilishi bungeni kwani uwakilishi hauna mwanamke au mwanaume na kusisitiza: "Tunawakaribisha wapinzani CCM, milango iko wazi".

Alisema chama cha siasa kinachogharamiwa na watu wa nje hicho sio chama."Unaweza kuwa na wabunge wengi wa upinzani wasio na tija, miaka mitano hawakuwahi kupiga kura ya bajeti ya serikali ndio maana hawana uchungu wa kufanya kazi ya uwakilishi wa kupitisha bajeti ya serikali hata wakati wa virusi vya corona walikimbia bungeni."

Dk Bashiru alisema tija ya uwakilishi ni muhimu kuliko idadi yao. Alisema wabunge wachache wa upinzani wanaweza kuwa na tija kuliko wabunge wengi wa CCM wanaoweza wasiwe na tija, cha muhimu ni kufanya kazi kwa maslahi ya wananchi.

"Malengo ya chama ni pamoja na kuongeza idadi ya wanachama na kuwa na takwimu sahihi juu ya wanachama na jumuiya zake. CCM sio chama cha wateule ni chama cha umma,"alisema.

Alisema katika uchaguzi mkuu uliopita wanawake wengi walijitokeza kugombea huku wanawake 24 walijitokeza kugombea kwenye majimbo na kati yao 23 walishinda kwa kishindo huku mbunge mmoja Hawa Ghasia akishindwa.

"Tulipoteza majimbo ya Mtwara vijijini ambapo Hawa Ghasia alikuwa akïgombea na jimbo la Nkasi kaskazini ambapo mgombea wa CCM, Ally Kessy alishindwa,”alisema.

Baada ya kukamilika kwa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu vyama vya CCM na Chadema ambavyo vilishiriki katika uchaguzi mkuu ndio vilikuwa na sifa za kupata wabunge wa viti maalumu.

Idadi ya wabunge wa viti maalumu hutokana na idadi ya kura za wabunge wote wa chama husika, ambapo chama kinatakiwa kupata asilimia tano ya kura zote halali za ubunge.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, CCM ilipata kura za ubunge milioni 8.3, Chadema milioni 4.6 na CUF milioni 1.2. kutokana na kura hizo CCM ilipata viti maalumu 64, Chadema 36 na CUF 10.

Novemba 24 mwaka huu, Wabunge 19 wa viti maalumu Chadema wakiongozwa na Mdee walikula kiapo cha uaminifu mbele ya Spika Job Ndugai.

Hata hivyo Chadema iligoma kuteua wabunge wa viti maalumu wakidai hawatambui matokeo ya uchaguzi uliopita kutokana na kuwa na kasoro nyingi.

Wabunge waliokula kiapo ni Mdee, Grace Tendega, Ester Matiko, Cecilia Pareso ,Ester Bulaya, Agnesta Kaiza, Nusrat Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga, Tunza Malapo, Felister Njau na Naghenjwa Kaboyoka

Wengine ni Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stela Fiayo, Anatropia Theonest, Salome Makamba, Conchesta Rwamlaza na Asia Mohammed.

Baada ya wabunge hao kuapishwa, Chadema ikawataka wabunge hao kufika mbele ya kamati kuu ya chama hicho ili kujieleza kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa dhidi yao.

Katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika, alisema kamati kuu ya chama hicho ina dhamana ya kupokea maombi, kupitia na kufanya uteuzi wa wabunge wa viti maalumu haikufanya mchakato huo.

Alisema kutokana na Chadema kutangaza hadharani kutoyatambua matokeo ya uchaguzi uliomrejesha madarakani Rais John Magufuli na kupita kwa idadi kubwa ya wabunge kutoka CCM.

Mnyika alisema utaratibu mzima haukuzingatiwa na kuhoji utaratibu uliotumika kabla ya kuwaapisha wabunge hao, ambao walisema wana baraka zote za chama na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Kwa upande mwingine Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikasema ilipokea barua zenye majina ya mapendekezo ya wanawake wabunge na madiwani wa viti maalumu kutoka Chadema.

NEC ilisema imepokea majina hayo Novemba 19 mwaka huu kutoka Chadema huku CCM walikuwa wametuma majina yao Septemba 26.

Pia Novemba 20, kikao kilikaa kuteua wabunge hao 19 kutoka katika chama hicho kwa mujibu wa katiba na sheria ya Tanzania.

Licha ya kauli hiyo ya NEC, Mnyika aliendelea kusisitiza kuwa Chadema haijafanya uteuzi wa wabunge hao na juzi Kamati Kuu ya Chadema katika kikao chake kilijadili masuala mbalimbali na ajenga mojawapo ilikuwa ya wabunge hao wa viti maalumu ambapo ilifikia uamuzi wa kuwafukuza uanachama.

Hata hivyo ilitoa nafasi kwa wabunge hao kuandika barua ya kuomba msamaha au kukata rufaa kwa mujibu wa utaratibu wa chama hicho.

Mpaka sasa wabunge wamekaa kimpya licha ya kutafutwa na gazeti hili mara kadhaa kujua hatua watakayochukua baada ya kufukuzwa.

Join our Newsletter