Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2021 01 14Article 521156

Siasa of Thursday, 14 January 2021

Chanzo: HabariLeo

CCM Iringa wawatega wabunge, madiwani

CCM Iringa wawatega wabunge, madiwani

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) katika Mkoa wa Iringa kimeweka utaratibu mpya wa kupima utendaji wa wabunge na madiwani wake wote unaotaka kila mmoja kutoa taarifa yake ya kazi zake kwa wananchi kila baada ya miezi mitatu.

Taarifa hiyo ilitolewa jana mjini Iringa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Dk Abel Nyamahanga katika kikao maalumu cha chama hicho kilichowakutanisha wabunge na madiwani hao.

Alisema ili chama kiweze kufuatilia kwa karibu utendaji wa wabunge na madiwani hao kimeweka utaratibu utakowalazimisha viongozi hao kutoa taarifa zao za kazi za kila baada ya miezi mitatu.

Dk Nyamahanga alisema hatua hiyo itakiwezesha chama hicho kufuatilia utekelezaji wa ahadi za viongozi hao na kushughulikia changamoto zitakazojitokeza ili kurudisha imani kwa wananchi na kujiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.

Akiongoza kikao hicho, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda (pichani) aliwataka wabunge na madiwani hao kuwa karibu na wananchi na kwamba, hali hiyo itakawawezesha kujua changamoto za wananchi na kuzifanyia kazi kwa maslahi ya taifa.

Kuhusu umuhimu wa viongozi hao kupewa semina ili kuyajua na kukumbushwa majukumu yao kwa wananchi, Pinda aliwataka kuzingatia maadili ya uongozi na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuchafua heshima yao, chama na serikali.

“Rushwa na ufisadi ni adui mkubwa wa maendeleo. Acheni pia siasa za udini na ukabila. Sisi wote ni Watanzania na wananchi wanataka kusikia habari ya maendeleo yao na taifa,” alisema.

Katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, CCM kilishinda katika majimbo yote saba ya Mkoa wa Iringa pamoja na kata zote katika halmashauri tano za mkoa huo.

Kwa mujibu wa taarifa, kikao hicho kilimpongeza Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Asas kwa mchango mkubwa alioutoa wa fedha na vifaa vya kampeni katika uchaguzi mkuu uliopita.

Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Brown Mwangomale alisema; “Tusipomtaja Asas katika ushindi wa wabunge na madiwani wote wa Mkoa wa Iringa tutakuwa hatutendi haki.

Katika mkoa wetu amechangia kila jimbo na kila kata kufanikisha ushindi tuliopata.”

Akizungumza katika kikao hicho, Asas alishukuru kwa ushirikiano aliopata kutoka kwa watendaji, viongozi na wanachama wote wa CCM uliomwezesha kutekeleza ahadi yake wakati akichaguliwa kuwa M-NEC ya kuhakikisha Mkoa wa Iringa, unarudi CCM.

“Miaka 10 iliyopita CCM ilipoteza Jimbo la Iringa Mjini na baadhi ya kata katika halmashauri mbalimbali. Leo mkoa wetu mzima ni wa kijani, tuna kila sababu ya kujipongeza,” alisema huku akiwataka viongozi hao kutobweteka.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi aliwataka viongozi hao wa kisiasa kuacha kugombana na watendaji wa serikali na hata inapotokea tofauti baina yao watumie vikao au taratibu rasmi kuweka mambo sawa.

Join our Newsletter