Uko hapa: NyumbaniInfosSiasa2020 12 09Article 517787

xxxxxxxxxxx of Wednesday, 9 December 2020

Chanzo: habarileo.co.tz

Chadema yapamba madiwani wakiapishwa Mbarali

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wilayani Mbarali mkoani Mbeya, juzi walifurika katika ukumbi wa mkutano uliopo kwenye ofisi za Bonde la Maji la mto Rufiji kushuhudia madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo wakiapishwa.

Madiwani hao waliapishwa kwenye kikao cha kwanza cha Baraza kilichofanyika kwenye ukumbi huo ulipo katika

Mamlaka ya mji mdogo wa Rujewa na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali.

Kati ya madiwani 27 waliokuwa wakiapishwa kwenye kikao hicho cha Baraza, 26 walitokea Chama Cha Mapinduzi(CCM) na mmoja pekee Charles Kiswaga wa kata ya Ubaruku ndiye aliyekuwa akitokea Chadema.

Kuhudhuria kwa wingi kwa wafuasi hao kulizua maswali mengi kwa wadau kuwa ilikuwaje wafuasi wa chama hicho wakawa na hamasa kubwa namna hiyo ya kuja kuhudhuria shughuli ya uapisho huo wakati wana diwani mmoja tu katika baraza hilo.

Kwa mgeni ambaye hakujua nini kilikuwa kikiendelea ilikuwa rahisi kwake alipopita maeneo ya jirani na ukumbi huo au kwenye maeneo ya jirani kunakopatikana huduma kama za vyakula kama chai na supu ikiwemo maeneo ya stendi ya Rujewa, kujua chama hicho kilikuwa na mkutano wake kutokana na wanachama kutapakaa maeneo hayo kabla ya kuanza kikao.

Kwa mtu mwingine ambaye hakuwa na taarifa sahihi za matokeo ya madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mbarali basi kwa hamasa ya wafuasi wa Chadema ya juzi angejiridhisha pasi na shaka kuwa chama hicho ndicho kilichojizolea madiwani lukuki kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu.

Chadema wakiwa wamevalia sare za chama chao ndiyo walikuwa wa kwanza mapema asubuhi kufika kwenye viunga vya ukumbi huo wakati shughuli za upangaji viti na mapambo vikiendelea na hivyo kuwalazimu kwa muda kukaa nje au kurandaranda maeneo ya jirani.

Kunako majira ya saa tano asubuhi baada ya wahusika wachache wa kikao kuingia ukumbini wafuasi wa Chadema nao waliamua kuingia ukumbini humo na kuufanya ukumbi kujaa hata kabla wahusika wote hawajaingia hatua iliyowashtua wafuasi wa CCM wachache waliohudhuria kutaka nao wawe ndani ya ukumbi lakini baadaye wote wakatakiwa watoke kwanza nje.

Ushiriki wa wafuasi wa Chadema sambamba na wanaCCM wachache kwenye kikao hicho uliendelea kwa wanachama hao kukaa milangoni na madirishani hata wakati shughuli ya uapishwaaji madiwani ikiendelea chini ya Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbarali, Aliko Mwandumbya aliyekuwa akisaidiwa na mwanasheria wa Halmashauri hiyo, Jackline Njaize.

Hata baada ya kuapishwa na baadaye wajumbe kufanya uchaguzi wa kumpata Mwenyekiti wa Halmashauri na makamu wake bado wafuasi hao waliendelea kuwepo na kushuhudia namna mwenyekiti mpya na baraza lake lililosheheni madiwani wa CCM likianza kufanya kazi zake kwa kuchagua Kamati za kudumu na pia kupokea taarifa ya utekelezaji wa mambo yaliyofanyika katika kipindi tangu baraza lililokuwepo la madiwani kuvunjwa.

Katika uchaguzi wa viongozi uliofanyika kwenye kikao hicho, Diwani wa Itamboleo, Twalibu Lubandamo alishinda nafasi ya uenyekiti wa Halmashauri kwa kupata kura za ndiyo 26 dhidi ya moja ya hapana na Makamu Mwenyekiti akachaguliwa Chuki Jeremiah aliyepata pia kura 26 za ndiyo na moja ya hapana.

Jambo lililokuwa la kuvutia hakukuonekana kuwepo kwa msukumano wowote baina ya wanachadema na wanaccm licha ya kuwa kila upande ulikuwa na sare zao walionekana kujitenga lakini ilipolazimu walijikuta wamekaa au kusimama kwenye eneo moja wakifuatilia klichokuwa kikiendelea ndani ya ukumbi.

"Hapo tu wana diwani mmoja je wangepata hata watatu ingekuwaje humu ndani....lakini yawezekana wamekuja kuhakikisha kama kweli madiwani wa CCM wataapishwa na diwani wao huyo mmoja....Mmmh watakuwa wamekuja kushinikiza diwani wao asitoe kura ya ndiyo kwa wagombea wa uenyekiti ndiyo maana umeona kura ya hapana imekuwa moja kwenye nafasi zote mbili..." walisikika wakijadili baadhi ya wafuasi wa CCM.

Kwa upande wao wafuasi wa Chadema walisema kuhudhuria vikao vya baraza ni haki ya kila mwananchi hivyo wameitumia nafasi yao kufika kujionea baraza hilo kwakuwa pia linalo jukumu la kuwatumikia wananchi wote wilayani hapa pasipo kujali itikadi za vyama.

Join our Newsletter